MASHABIKI wengi wa soka jijini Dar es Salaam, wamesema umefika wakati sasa nafasi nyingi zaidi katika timu ya taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, zitolewe kwa wachezaji wa Zanzibar.
Ushauri huo waliutoa Disemba 5, kwa nyakati tafauti baada ya mchezo wa robo fainali ya michuano ya Chalenji, uliozikutanisha timu za Zanzibar Heroes na Amavubi ya Rwanda kwenye uwanja wa Taifa ambapo Heroes ililala kwa mabao 2-1 licha ya kumiliki mpira kwa asilimia 62.
Wakionesha namna walivyokikubali kikosi cha Zanzibar Heroes, baadhi ya mashabiki, walisema si haki kuona kocha mkuu wa Taifa Stars anag’ang’ania kuifanya timu hiyo kama mali ya Simba na Yanga, wakisema si vyema kuwang’ang’ania wachezaji wa klabu hizo ambao wengi wamechoka.
Shabiki aliyejitaja kwa jina moja la Jumanne, alieleza kuwa mashindano ya Chalenji kwa miaka mitau iliyopita ukiwemo 2011, yameonesha jinsi Zanzibar ilivyo na vipaji vizuri vya soka vinavyoweza kuisaidia Tanzania kuondokana na jina la kichwa cha mwendawzimu.
Naye William Chuma, alidai kuwa, uteuzi wa wachezaji wa Stars, unafanywa kwa misingi ya mapenzi ya viongozi wa TFF ambao kwa kiasi kikubwa wamejaa ushabiki wa timu za Simba na Yanga.
“Umefika wakati hali hii ibadilike, na makocha wanaoajiriwa kuinoa Stars, waandaliwe ziara za kuzunguka Tanzania nzima ikiwemo Zanzibar, ili kuona vipaji vingi vilivyoenea ambavyo vitasaidia kujenga timu bora ya taifa”, alisema.
Sifa hizo kwa timu ya Zanzibar hazikuishia kwa mashabiki pekee, bali hata kocha mkuu wa timu ya taifa ya Malawi Kinnah Phiri, alikaririwa akielezea kukunwa kwake na uchezaji wa timu hiyo, huku akisema kwamba angetamani kucheza nayo hata baada ya mashindano ya Chalenji.
“Mna timu nzuri sana, kwa kuwa hatukupangwa kundi moja wala hatujakutana nanyi kwenye robo fainali, yafaa tuandae utaratibu wa kucheza angalau mechi moja ya kirafiki baadae, ama Lilongwe au Zanzibar”, alisikika Phiri akimwambia kocha wa Heroes Hemed Suleiman ‘Moroko’ ambao timu zao zilipangiwa hoteli moja.
No comments:
Post a Comment