Na Salum Vuai, Dar es Salaam
LICHA ya kufungwa na Rwanda mabao 2-1, timu ya taifa ya soka ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, imezawadiwa kitita cha shilingi milioni tano na kampuni ya Future Century Limited, kwa kuonesha kiwango kizuri siku ya pambano hilo.
Zanzibar Heroes ilichapwa mabao hayo katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya ‘Tusker Challenge Cup’ uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Disemba 5, mwaka huu.
Pamoja na kampuni hiyo kuahidi kutoa zawadi hiyo endapo Zanzibar Heroes ingeshinda na kuingia nusu fainali, lakini imeamua kuitekeleza kwa kufurahishwa kwake na soka safi lililotandazwa na vijana hao.
Akikabidhi fedha hizo wakati wa hafla ya kuwapongeza wanandinga hao iliyofanyika usiku wa siku hiyo kwenye hoteli ya Rambo Green View, Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo Hellen Masanja, alisema kiwango kilichooneshwa na timu hiyo, kimedhihirisha ubora wake, na kwamba wengi wamewasifia wachezaji hao.
“Kufungwa na kushinda ni sehemu ya mchezo, lakini mmeonesha kuwa nyinyi ni timu nzuri ambayo ikiwa na mikakati endelevu inaweza kuwa tishio baadae na kufanya makubwa kwa heshima ya Zanzibar”, alisema Masanja.
Aliwapongeza wachezaji wa timu hiyo, kwa moyo wa kizalendo na kujituma, licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa wakati wa kambi pamoja na ushiriki wa mashindano hayo yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Aidha, alisema ingawa kampuni yake si mdhamini wa timu hiyo kama baadhi ya watu wanavyodhani bali ni mratibu wa kuitafutia udhamini, itaendelea na jitihada zake za kuisimamia na kitafutia wadhamini wengi zaidi watakaoweza kuiimarisha kwa ajili ya mashindano yajayo na mengine.
Akitoa shukurani kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema pamoja na uzuri wa kikosi hicho, lakini mamlaka zinazosimamia michezo, zinapaswa kuiandalia mikakati endelevu ili iendelee kuwa pamoja na kucheza mechi za kila mara za majaribio.
“Badala ya kungoja wiki mbili au tatu kabla mashindano ndio tukusanywe, sasa ni lazima tuandaliwe progamu ya kudumu ili tuweze kukutana kila baada ya kipindi na kufanya mazoezi ya pamoja sambamba na kupata mechi za kirafiki ndani na nje ya nchi”, alishauri nahodha huyo.
Zanzibar Heroes ilikuwa ikishiriki michuano ya Chalenji inayoelekea ukingoni jijini Dar es Salaam, ambapo ilitinga robo fainali kama ‘best looser’ na kutolewa na Amavubi ya Rwanda kwa magoli 2-1 juzi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment