Habari za Punde

Balozi Seif Alitaka Jeshi la Polisi Kuimarisha Ulinzi Sehemu za Fukwe

Na Yussuf Simai-Maelezo Zanzibar.


Kamishna Wa Polisi Zanzibar Bwana Mussa Ali Mussa akimpa maelezo ya ujenzi wa nyumba za polisi paje Makamu Wa Pili Wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kuweka jiwe la msingi.
Kikundi cha utamaduni cha jeshi la Polisi kikitoa burdani katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msini na ufunguzi wa nyumba za polisi paje ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kusherehekea miaka 48 ya Mapinduzi Ya Zanzibar

Makamu Wa Pili Wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kuifungua rasmi nyumba ya kulala askari polisi paje mkoa kusini unguja ikiwa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za mapinduzi kutimia miaka 48.


Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi amelitaka jeshi la Polisi kuimarisha Ulinzi Zaidi katika sehemu za fukwe za Zanzibar ili kuondosha Uhalifu unaofanywa na watu wanaojifanya ni mapapasi wa Watalii.

Makamo ameyasema hayo huko Paje mkoa wa kusini Unguja alipofungua Nyumba za Askari Polisi pamoja na kuweka jiwe la Msingi katika nyumba nyengine zinazoendelea kujengwa katika sehemu hio.

Balozi Seif amesema kuwa hivi sasa kuna vikundi mbalimbali vya watu wanaojifanya mapapasi wa Watalii na kupita katika Fukwe na kuwanyang’anya watalii ambao hukaa katika Fukwe na kujipumzisha.

Amezitaja fukwe za Nungwi, Bwejuu na Paje kuwa ndizo zinazopendelewa sana na wahalifu hao hivyo amelitaka jeshi hilo kuimarisha Ulinzi zaidi ili kuona wananchi pamoja na Watalii wanakuwa na utulivu na salama katika sehemu hizo.


Akizungumzia suala la Makaazi Balozi amesema,malengo ya Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ni kuwapatia maisha bora na makaazi mazuri wananchi wake wote na hivyo itaendelea kujenga makaazi zaidi kila itakapokuwa na uwezo.

Nae Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa ameahidi kuchukua hatua zaidi za usalama katika maeneo yaliotajwa na maeneo mengine ili kulinda maisha ya Raia pamoja na Mali zao.

Kadhalika amewataka wananchi wote kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuwafichuwa wale wote wanaojishughulisha na vitendo vibaya vya Unyang’anyi na Uporaji kwa Watalii na wananchi kwa jumla.

Ufunguzi wa Nyumba hizo za Polisi umekwenda sambamba na utowaji wa Vyeti kwa Wawekezaji wawili ambao ndio wadhamini wa Ujenzi huo,ambao ni Ivan Koden anaemiliki Hoteli ya Cystal Resort ya Paje na Hussen Alhashim anaemiliki Hoteli ya Grand Property ya Paje.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.