Habari za Punde

Maalim Seif Azindua Jengo la Mfuko wa Barabara

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika ufunguzi wa jengo la mfuko wa barabara Zanzibar huko Maisara mjini Zanzibar. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Mheshirimiwa Omar Yussuf Mzee. 
Jengo la Mfuko wa Barabara Zanzibar lililozinduliwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Mshauri mwelekezi wa ujenzi wa jengo la Mfuko wa Barabara Zanzibar Bwana Yasser De Costa akitoa maelezo ya ujenzi huo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad baada ya ufunguzi rasmi wa jengo hilo.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikata utepe kuashiria kulifungua rasmi jengo la Mfuko wa barabara Zanzibar lililoko Maisara ikiwa ni katika shamra shamra za maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

(Picha na Salmin Said. OMKR).

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea haja kwa majengo ya kisasa ya serikali kuwa mfano katika kuwajali watu wenye ulemavu nchini.

Amesema majengo mengi yanayoendelea kujengwa bado hayajatoa umuhimu kwa watu wenye ulemavu na kuwafanya kushindwa kuyatumia kwa shughuli mbali mbali za kijamii ambazo zinapaswa kuwafikia wananchi wote.



Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa changamoto hiyo leo wakati akifungua jengo la ghorofa tatu la mfuko wa barabara Zanzibar lililoko Maisara ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ameitaka kampuni ya Rans Limited kutoka Zanzibar ambayo ndio mkandarasi wa ujenzi huo kuangalia uwezekano wa kulifanyia marekebisho jengo hilo ili watu wenye ulemavu wa aina mbali mbali nao waweze kulitumia.

Licha ya kasoro hiyo, Maalim Seif amesifu umakini uliooneshwa na wakandarasi hao wazalendo katika ujenzi huo na kutaka wasisite kuomba tenda za ujenzi wakati zinapotolewa ili kuendeleza fani hiyo ambayo inaleta faraja kwa taifa.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa barabara, Maalim Seif amesema zinasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi, kwa vile wakulima hupata fursa ya kusafirisha mazao yao kwa urahisi sambamba na kurahisisha shughuli za utalii.

Amesema kuwepo kwa mfuko wa barabara ulioanzishwa mwaka 2001, kutasaidia kutatua kero mbali mbali za uharibifu wa barabara na kuutaka uongozi wa mfuko huo kutafuta nji za kuongeza vyanzo vya mapato ili kuepuka utegemezi kutoka kwa wafadhili.

“Katika bajeti ya mwaka huu, sekta ya ujenzi wa miundombinu ya barabara imetengewa shilingi 33.830 bilioni, hizi ni kwa ujenzi wa barabara nane. Kati ya fedha hizo SMZ itachangia shilingi 5.5 bilioni tu, zilizobaki zaidi ya shilingi bilioni 28 zinatarajiwa kuchangiwa na wafadhili ambao nao wanakabiliwa na matatizo mengi” alieleza Maalim Seif.

Pia ameelezea haja kwa mfuko huo kurejesha utamaduni wa kuwepo kikosi kazi cha utunzaji wa barabara ili kuzifanya barabara ziwe katika hali nzuri wakati wote.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa mfuko huo Bwana Abdi Khamis amesema mfuko wa barabara una nia thabiti ya kulitunza jengo hilo ili liweze kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma zinazostahiki.

Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Bwana Khamis Mussa Omar amesema lengo la serikali kuanzisha mfuko huo kwa lengo la kutunza barabara ambazo zilionekana kuwa katika hali mbaya mnamo miaka ya 90.

Amesema tangua kuanzishwa kwa mfuko huo mwaka 2001, mafanikio makubwa tayari yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa bajeti ya mfuko huo kutoka serikalini.

Takriban shilingi milioni mia saba zimetumika kwa ajili ya ujenzi huo.

Hassan Hamad (OMKR).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.