Habari za Punde

Hamad Rashid Akataliwa kwa ‘Kibwebwe’ Wawi

Na Haji Nassor, Pemba

WANACHAMA na wapenzi wa CUF katika jimbo la Wawi, Chake Chake Pemba, wameyabariki maamuzi ya Baraza Kuu la chama hicho yaliyopitishwa hivi karibuni ya kumvua uwanachama mbunge wa jimbo hilo, Hamad Rashid Mohammed.

Msimamo wa wanachama hao ulibainika juzi jioni huko Vitongoji kwenye risala yao waliyoisoma baada ya kufanya maandamano ya kuunga mkono kutimuliwa kwa mbunge wao huyo ndani ya chama hicho.


WanaCUF hao walisema kutokana na Hamad kukiuka katiba pamoja na kwenda kinyume na maadili, uamuzi wa kufukuzwa uliochukuliwa hawana mashaka nao na kuliomba Baraza hilo kumshughulikia kila atakaye vunja katika na maadili ya chama.

Akisoma risala hiyo kwa niaba ya wananchi wa Wawi, Salha Ali Said, alisema inasikitisha sana na maneno yaliokuwa wakitolewa na Hamad Rashid ikiwa ni pamoja na kuchukia kuwepo kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Walieleza kuwa Hamad alikuwa akiwahutubia mara kwa mara kwenye mikutano ya ndani na kulaumu kwa kutambuliwa Rais mstaafu wa awamu ya sita wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Aman Abeid Karume na hatimae vyama vya CCM na CUF kuafikiana.

“Hamad alionekana kulaumu sana chama taifa kutokana na uamuzi wa Katibu Mkuu wetu kumtambua Rais Karume na kisha kusababisha vyama viwili hivi kuungana na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa”,alieleza.

Kwa upande wake Katibu wa Vijana taifa CUF, Khalif Abdallah Ali, alisema kuwa Hamad Rashid na wenzake waliofukuzwa uanachama kwa sasa hawawatumbui tena na wako huru kwenda chama watakacho.

Alieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya CUF, ukishafukuzwa uwanachama na chombo cha juu cha chama, maana yake sio mwanachama tena na wala hatumbuliki ndani ya chama.

Nae Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Juma Duni Haji alisema uliofikiwa si wa kumuonea Hamad Rashid na wenzake waliofukuzwa uanachama bali kilichozingaitiwa ni sheria na kanuni zinazoongoza chama husika.

Duni ambae awali alipokea maandamano ya wananachama wa CUF Jimbo la Wawi, alizidi kueleza kushangaa kwake kuona vyama vyengine na wanasiasa wanaumwa na Hamad Rashid mara baada ya kuvuliwa uwanachama.

“Jamani CUF kwani ndio chama cha kwanza hapa Tanzania kuwafukuza wanachama wake, mbona mnaumwa bure na maamuzi ya Baraza Kuu la CUF kutokana na uamuzi wake , hebu kama mnampenda mchukue nyie huyu Hamad na wenzake’’,alifafanua Juma Duni.

Aidha alieleza kuwa suala la Hamad Rashid aliekuwa mbunge wa Wawi na wenzake ndani ya CUF kwa sasa limekwisha na wanajipanga na kufanya shughuli za kimaendeleo, sio kujibizana na Hamad kupitia vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa Zanzibar imetoka mbali, kisiasa na kwa sasa imetulia na wananchi wanashirikiana kwa pamoja katika kazi zao mbali mbali hivyo anapojitokeza kiongozi kutaka kuwavuruga wananchi, hatovumiliwa na sheria itachukua mkondo wake.

Katika hatua nyengine Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la CUF taifa Juma Duni Haji ambae pia ni Waziri wa Afya amekitaka chama cha CHADEMA kuacha mara moja tabia ya kukifuata chama chao, kwani hawana uhusiano wowote kwenye siasa zao.

Kwenye mkutano huo wa hadhara ulioambatana na maandamano yaliyongozwa na Jeshi la Polisi na kubeba mabango mbali mbali yenye ujumbe ikiwa ni pamoja na ‘hongera baraza kuu kwa maamuzi makuu’.

2 comments:

  1. Kwa kweli inasikitisha kama kweli Hamad Rashid alikuwa akienda chini chini kupinga maridhiano ya CUF na CCM. Inasikitisha kwamba mtu kama yeye alikuwa haitakii mema nchi yetu. Kwa kuwa wananchi wa jimbo alilokuwa mbunge washatoa msimamo huo, basi sasa Hamad Rashid kwisha!. Mwache aendelee kuwa mbunge wa mahakama na aendelee kuiwakilisha mahakama huko bungeni.

    ReplyDelete
  2. Usanii mtupu! hii ndio raha ya kuongoza watu ambao hawakusoma.
    Naamini Wawi kama zilivyo sehemu nyingine za Z'bar 'people are not informed'..hawana taarifa.

    Njia pekee ya kupata taarifa kwa watu hawa ni kukhadithiwa mambo tu..hawasomi magazeti, hawatembelei mitandao, hawasikilizi redio wala kuangalia televisheni.. kwa hivyo hawawezi kuhoji kitu. naamini hiyo risala pia itakua imeandaliwa na mtu mmja kwa niaba ya wengine kama ilivyo kawaida.

    Wengi waliohojiwa walikiri kwamba wao walikua hawamtaki HAMAD RASHID lakini Maalim alishinikiza
    na hii ndio kawaida yake katika majimbo takriban yote!

    Kuna rafki yangu mmoja iliwahi kuniambia Maalim analipa fadhila,..familia nyingi zenye asili ya kiarabu zenye uwezo zilimsaidia na zile zisizo uwezo zilikua zinamualika angalau kufufatari.

    Kwa hivyo suala la demokrasia katika chama cha CUF lina changamoto nyingi.
    Nakumbuka marehemu Dr. omar aliwahi kusema CUF ni SEFU na SEFU ni CUF sasa ndio hayoo!!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.