Habari za Punde

KOFDO Yaiomba Serikali Kuangalia Upya Sheria ya Uvuvi

Na Faki Mjaka-Maelezo

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeombwa kuiangalia upya Sheria ya Uvuvi ya Mwaka 2010 kutokana na kutokukidhi hali halisi ya uvuvi wa Zanzibar jambo ambalo limepelekea matatizo mengi kwa wavuvi

Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Wavuvi wa Kojani KOFDO Omar Mohammed Ali wakati alipokuwa akichangia mada katika semina ya mafunzo ya mpango mkakati wa jumuiya hiyo iliyofanyika ukumbi wa Elimu mbadala Raha leo Zanzbar na kufadhiliwa na jumuiya ya Foundation for Civil Society.


Amesema sheria hiyo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikisababisha sintofahamu kati ya Idara ya Uvuvi na Wavuvi kutokana na kutotekelezeka kwani wavuvi wengi wanadai imekuwa na kasoro nyingi

Omar amezitaja baadhi ya kasoro katika sheria hizo kuwa ni pamoja na kuzuia matumizi ya Chupa za Gesi zinazotumiwa na wavuvi ili kusaidia hewa katika shughuli zao lakini sheria hiyo haiwazuii Watalii kuzitumia katika kuogelea

Ameongeza kuwa Sheria hiyo pia inazuia matumizi ya Mkuki(bunduki) kwa kuvulia Pweza lakini inashindwa kuainisha zana mbadala ya kumvulia Pweza jambo ambalo hupelekea tafrani kwa wavuvi wa Pweza

Aidha Sheria hiyo inakataza matumizi ya Nyavu zenye macho madogo zinazotumika kuvulia Samaki aina ya Dagaa lakini haioneshi mtego mbadala wa kuvulia samaki wa aina hiyo

Mwenyekiti huyo wa KOFDO amedai kuwa kwa vile wavuvi wa Zanzibar kwa ujumla wao hawakushirikishwa katika utungwaji wa sheria hiyo kumepelekea Serikali kuwa na mgogoro na wavuvi wengi wa Unguja na Pemba kutokana na Sheria hiyo kutotekelezeka.

Ameiomba Serikali kufanya maamuzi magumu ya kuiangalia upya sheria hiyo ambayo imepelekea tafrani kubwa ya kukamatwa kwa wavuvi wengi na zana zao jambo ambalo limepelekea ongezeko la ukosefu wa ajira na umaskini kwa ujumla.

Amesema Sheria hiyo imekuwa kikwazo si tu kwa wanajumuiya yake lakini pia wavuvi kwa ujumla wao wakiwemo wavuvi wa Uroa, Chwaka,Pwani Mchangani Matemwe na Pongwe nao wamekuwa wakiathirika vibaya na sheria hiyo

Kwa upande mwengine Mwenyekiti huyo amesema Jumuiya yao iko bega kwa bega katika kutunza mazingira ya baharini sambamba na kulaani wale wote wanaotumia zana haramu za kuvulia kama vile madawa ya kuleweshea samaki (Utupa) uvuvi wa bomu, Vyandarua, Korokoro na Juya

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina hiyo Salama Kombo Ahmed ambaye pia ni Mwenyekiti wa ANGOZA alisema kuwa sheria hiyo ya Uvuvi ya mwaka 2010 haikupitia katika mwamvuli wa Jumuiya yao na kusema kwamba kuna haja ya Serikali kuyafanyia kazi maombi hayo

Aidha Salama aliwataka wanajumuiya hiyo kufanya kazi kwa mashirikiano kwani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana ikiwa kutakuwa na mgawanyiko katika jumuiya hiyo.

Jumuiya ya Maendeleo ya Wavuvi wa Kojani KOFDO yenye Makao makuu yake Mtoni Unguja ilisajiliwa Zanzibar mwaka 2008 ambapo kwa sasa ina zaidi ya wanachama 100 ikiwa na malengo mbali mbali yakiwemo kusimamia maslahi ya wavuvi

MWISHO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.