Habari za Punde

Netiboli Tz Yala Mweleka

Yalala kwa Uganda, leo zamu ya wanaume

Na Mwajuma Juma

WENYEJI Tanzania, wameyaanza vibaya mashindano ya netiboli kwa timu za wanawake Afrika Mashariki na Kati kuwania Kombe la Mapinduzi, kwa kusalimu amri mbele ya Uganda ikichapwa mabao 38-33.

Pazia la patashika hizo zinazofanyika kwenye uwanja wa Gymkhana, lilifunguliwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Bihindi Hamad Khamis, aliyekuwa mgeni rasmi.


Mapema, wachezaji wa timu zinazoshiriki mashindano hayo, walipita mbele ya mgeni rasmi na waalikwa wengine, kutoa salamu zao.

Kwa ujumla mabanati wa timu hizo ambazo wanajuana vyema, walicheza kwa ushindani mkubwa na kuwafanya mashabiki waliojimwaga uwanjani hapo kushindwa kukaa kwenye viti vyao.

Uganda iliwatumia wachezaji wake mahiri kuisambaratisha Tanzania, ambapo Peace Proscovia alimudu kumimina mabao 14, huku Amono Florence, akipachika mabao 24.

Nayo Tanzania iliweza kufunga magoli kupitia kwa Asha Ibrahim na Pili Peter walipachika mabao 14 kila mmoja, Mwanaidi Hassan (9) na Nelly Kazinje (6).

Katika mfululizo wa mashindano hayo, leo Uganda wanaume ambayo ndiyo timu pekee iliyowasili, itaoneshana kazi na Tanzania.

Taarifa zilizotolewa na Kamati ya Mashindano hayo, zimefahamisha kuwa, timu za Kenya, Msumbiji, Zambia, na Zimbabwe zinatarajiwa kuwasili nchini leo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.