Na Shifaa Said, MCT
CHUO cha Uandishi wa Habari cha Zanzibar, kinakusudia kuimarisha utendaji wa shughuli zake hususan katika kukiendeleza kwa kuwa na majengo yake ili kuimarisha utendaji na ufanisi wa kutoa mafunzo katika kada ya habari hapa nchini.
Akizungumza na ujumbe maalum uliowashirikisha wataalamu kutoka NACTE na Baraza la Habari Tanzania, Mkuu wa chuo hicho Saleh Mnemo, alisema hadi hivi sasa wanayo madarasa manne ambayo yanatoa taaluma ya habari katika chuo hicho.
Alisema kuwa katika kukabiliana na uhaba wa nafasi, chuo kimefanya juhudi ya kutafuta kiwanja hali itakayokiwezesha kuwa na nafasi ya kutosha ambayo itakuwa ya kudumu ili kuimarisha huduma na kutoa elimu iliyo bora.
“Tayari tunacho kiwanja na michoro ya jengo la ghorofa nne imekamilika katika eneo la Tunguu hapa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kuwa na nafasi ili kuimarisha utoaji wa elimu katika viwango mbali mbali katika kada hii ya habari”, alisisitiza.
Alisema kuwa kwa hivi sasa wanatumia majengo yaliyoko Vuga ambayo hayakidhi haja, hata hivyo mpango mkakati wa chuo ni kufanikisha ujenzi huo ili kwenda sambamba na kukua kwa kada ya habari hapa nchini.
Alifafanua kuwa katika kuimarisha shughuli za chuo hicho pia wamefanikiwa kuwa na chumba cha kompyuta, maktaba, studio na vifaa vyengine kadhaa ili kuimarisha mafunzo ya uandishi wa habari hususan katika kufanya mafunzo ya vitendo ambayo ni muhimu katika kada hiyo.
Naye kiongozi wa ujumbe huo kutoka NACTE, Charles Msirikale alisema kuwa ukaguzi huu uliofanywa ni hatua muhimu ya kutizama uwezo wa vyuo mbali mbali katika kutumia mtaala mpya uliotayarishwa kwa pamoja baina ya Baraza la Habari na NACTE.
Msirikale aliridhishwa na hatua tofauti zilizochukuliwa na chuo katika kuimarisha shughuli zake na pia katika kuhakikisha kuwa kinakuwa ni moja wapo ya vyuo vya habari ambavyo vitaweza kutumia mtaala huo uliopitishwa na NACTE.
“Hatua ya kuimarisha shughuli za chuo cha waandishi wa habari inatupa matumaini kuwa kinaweza kuwemo katika kupata usajili wa kuweza kutumia mtaala huo mpya wa NACTE ambao ulitayarishwa kwa mashirikiano na baraza la habari Tanzania”, alisisitiza.
Naye Ofisa wa programmu wa Baraza la Habari, Alfred Mbogora alisema mtaala wa kufundishia vyuo vya habari ulitayarishwa ili kuwe na utaratibu mzuri ambao utatoa sura halisi ya ufundishwaji katika vyuo vya habari hapa Tanzania.
Alisema kuwa mtaala umepitiwa na wataalamu tafauti na kuidhinishwa na NACTE na hivi sasa wamo katika mchakato wa kuangalia ni vyuo gani vitapata nafasi ya kutumia mtaala huo.
Chuo cha waandishi wa habari cha Zanzibar kimeanzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kuwapa mafunzo waandishi waliopo kazini lakini baadae kikaanzishwa rasmi mwaka 2009 kwa mujibu wa sheria No. 11 ya mwaka 2006.
Chuo kinatoa mafunzo katika ngazi ya stashahada na cheti pia hutoa mafunzo mafupi ya habari pamoja na kufundisha lugha ya Kichina.
No comments:
Post a Comment