Habari za Punde

Tanzania, Kenya Kujenga Soko Namanga

Na Mustafa Leu, NAMANGA

TANZANIA na Kenya, jana zilisaini makubaliano ya kujengwa soko la kimataifa mpakani mwa nchi hizo katika eneo la Namanga kwa upande wa Tanzania na eneo la Kajiado, kwa upande wa Kenya.

Soko hilo la kimataifa kwa kiasi kikubwa litawawezesha wafanyabiashara kutekeleza majukumu yao kwa uhuru bila kubughudhiwa wala kutumia njia za panya kusafirisha bidhaa kutoka nchi moja kwenda nchi moja kama inavyofanyika hivi sasa.

Waziri wa Ushirikiano wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta kwa pande wa Tanzania, na upande wa Kenya ilisainiwa na waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa nchi hiyo, Mussa Sirima.


Hafla hiyo ilifanyika kwenye uwanja wa skuli ya msingi, Namanga, baada ya kumalizika mkutano wa hadhara wa kuwaelezea wananchi hatua zinazochukuliwa na Jumuia kuondoa vikwazo vya kibiashara.

Mawaziri hao kwa niaba ya Jumuia ya Afrika Mashariki na serikali zao, walisaini makubaliano yenye maeneo 10 ambayo yatawezesha mtu yeyote wa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki ataweza kufanyabiashara bila ya kubughudhiwa.

Kwa upande wake, waziri Sitta alisema kabla ya ujenzi wa soko hilo la kimataifa kuanza jumuia hiyo ya Afrika Mashariki itaanza ujenzi wa minada kwa ajili ya wafugaji ambao watauza ng'ombe katika eneo hilo.

"Kikao cha pamoja kinatokana na makubaliono ya nchi tatu Tanzania, Kenya na uganda ili kuangalia changamoto zilizopo katika maeneo ya mipakani zinazowakabili wafanyabiashara na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu"alisema sita.

Katika makubaliano hayo wakuu wa wilaya za mpakani za Longido na Kajiado, na mipaka mingine ,kuanzisha utaratibu wa ujirani mwema ili wananchi wanaposafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine wasisumbuliwe.

Aidha wakuu hao wa wilaya watapendekeza vibali vitakavyotumika na gharama zitakazotozwa gari zinazopita katika nchi moja kwenda nyingine yakiwemo ya mizigo na watalii.

Jumuia hiyo ya Afrika mashariki imeshaanza kutekeleza maeneo matatu ya ushirikiano ambayo ni Forodha, eneo ambalo limeanza kutekelezwa tangu mwaka 2005, na eneo lingine ni soko la pamoja ambalo limeanza kutekelezwa mwaka 2010 na sasa wanaangalia uanzishwaji wa sarafu moja.

Alisema kuwa Jumuia hiyo inazidi kupanuka na inajianda kuipokea Sudani Kusini mwezi Aprili mwaka huu kuwa mwanachama mwingine wa sita wa jumuia hiyo katika kikao cha wakuu wa nchi za jumuia hiyo kitakachofanyika Nairobi nchini Kenya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.