Habari za Punde

Zanzibar Yatakiwa Kutumia Ofisi za Kibalozi Kujitangaza

Na Mwantanga Ame

KAMATI ya Habari Utalii, Mifugo na Uwezeshaji ya Baraza la Wawakilishi, imesema kuwa uongozi wa Kamisheni ya Utalii unahitaji kubadilika kwa kuutangaza utalii katika balozi za nje.

Kamati hiyo iliyaeleza hayo jana wakati ikifanya majumuisho baada ya kumaliza ziara ya kuzikagua shughuli za wizara ya Habari Utamaduni, Utalii na Michezo, kikao ambacho kilifanyika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi.

Maeneo ambayo iliyatembelea ni pamoja na Hoteli ya Bwawani, Tume ya Utangazaji Zanzibar, Idara ya Makumbusho, na eneo linalojengwa mnara wa kurushia matangazo ya redio huko Tunguu.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohammed Said Dimwa, alisema inasikitisha kutokuwepo kwa taarifa zinazoutangaza utalii wa Zanzibar katika balozi za nje, huku kamisheni hiyo ikiwa haina mawasiliano mazuri na balozi hizo.

Makamu huyo akitoa mfano alisema Ofisi za Ubalozi wa Oman, Zanzibar haina hata bango wala kipeperushi vinavyoutangaza utalii wa Zanzibar jambo ambalo linahitaji kuangaliwa kuzifikia nchi hizo badala ya kuliangalia soko la utalii katika nchi za magharibi pekee.

Dimwa alisema ipo haja kwa viongozi hao kubadilika kwani serikali ya awamu ya tano iliweka sekta ya utalii kuwa ndio kitega uchumi cha Zanzibar kwa kutambua kuwapo kwa vivutio vingi.

Aidha, Makamu huyo pia aliiagiza wizara hiyo, kuliangalia pendekezo la serikali katika suala la kuibinafsisha hoteli ya Bwawani kwani inaweza likapoteza mwelekeo wa dhana ya kilelezo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Marehemu Mzee Amani Abeid Karume.

Nae Mwenyekiti wa kamati hiyo Asha Bakari Makame, aliwataka watendaji wa serikali kuacha kutumia kumbi za mikutano za watu binafsi kuendesha semina na magongamano na badala yake wautumie ukumbi wa hoteli ya Bwawani.

Alisema inasikitisha baadhi ya watendaji kutumia kiasi kikubwa cha fedha kukodi kumbi za watu binafsi wakati wangeliweza kutumia fedha kidogo kulipia ukumbi wa Hoteli hiyo.

Alisema kutotumiwa kwa ukumbi huo kumekuwa kukiifanya hoteli hiyo kukosa mapato ambayo yangeliweza kusaidia kuimarisha utoaji wa huduma pamoja na matunzo ya baadhi ya sehemu za hoteli hiyo.

Kutokana na hali hiyo Mwenyekiti huyo alisema ni vyema suala hilo likaangaliwa kwa umakini na ikiwezekana serikali inapaswa kutoa agizo kwa Wizara yake kuacha kutumia kumbi za watu binafsi na badala yake utumike ukumbi huo.

Aidha aliwataka watendaji wakuu wa wizara hiyo kuwa makini wanapopendekeza kwa Rais watendaji wa kuongoza taasisi zao, ambapo aliwataka wachague wenye uwezo kiuwajibikaji na si vinginevyo.

Alisema hali hiyo imekuwa ikichangia kuwapo kwa watu wasiokuwa na uwezo jambo ambalo husababisha kutokea matatizo huku kukiwa na migongano sehemu za kazi.

Mwenyekiti huyo alionya baadhi ya tabia ya viongozi wa wizara hiyo, kukumbatia safari za nje pekee huku wakiacha maafisa husika kwenda katika safari hizo.

Alisema Kamati yake imekuwa na taarifa nyingi za baadhi ya viongozi kuwa vinara wa safari za nje na kuzuia kuwapa nafasi maafisa wengine wa ngazi za chini hata kama kazi wanazotaka kwenda kuzifanya zikiwa hazihusiani na mtu aliepelekwa na kudai kuwa hiyo ni tabia mbaya.

Nae Mjumbe wa kamati hiyo Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, Salim Abdalla Hamad, akitoa maelezo yake alishauri serikali kuhakikisha watendaji wa taasisi wanautumia vyema ukumbi wa Hoteli ya Bwawani iili kuiwezesha serikali kuongeza mapato.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Dk. Ali Mwinyikai akijibu baadhi ya hoja alisema Wizara hiyo imekuwa ikijitahidi kuwapa nafasi watendaji wa ngazi ya chini ikiwa pamoja na kuwaandalia mazingira mazuri ya kazi.

Alisema hivi karibuni Wizara hiyo imeweza kupeleka watendaji mbali mbali nchini China kwa hatua za kujifunza mambo mbali mbali huku Wizara hiyo ikijibana kutoa safari hizo kwa kuzingatia matumizi ya fedha.

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo alisema bado Wizara hiyo itazingatia kuyatekeleza maagizo mbali mbali ya Kamati hiyo likiwemo suala la kusimamia mfumo wa mabadiliko ya matangazo ya digitali kuhakikisha unafanikiwa na maagizo ya kamati hiyo kwa taasisi nyengine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.