Habari za Punde

Waziri Adai Nyaraka TRA Kutoza Kodi mara mbili

Na Ali Issa, Maelezo

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Samia Suluhu Hassan, amewaagiza wafanyabiashara wa Zanzibar kumpatia vielelezo na nyaraka zinazothibitisha kutozwa ushuru mara mbili wanapoingiza bidhaa zao Tanzania bara.

Waziri Samia alieleza hayo jana katika Bandari ya Zanzibar, baada kufanya ziara bandarini hapo ambapo katika ziara hiyo wafanyabiashara kadhaa walilalamikia kuendelea kwa tatizo hilo.

Samia alisema nyaraka hizo zitampatia ushahidi dhidi ya malalamiko yao na kwamba suala hilo kwa muda mrefu limekuwa likirejesha nyuma juhudi za kiuchumi zinazohusu masuala ya Muungano.


“Huwa nasikia bidhaa ya aina moja mfanyabiashara wa Zanzibar iwapo ataipeleka bara hutozwa ushuru mkubwa wakati bidhaa hiyo huwa tayari ameshailipia Zanzibar, lakini ninapoomba kupatiwa ushahidi wa malalamiko hayo huwa sipatiwi”, alisema Samia.

Alisema endapo atapewa nyaraka hizo zitamthibitishia kuwasilisha vielelezo kunakohitajika ili tatizo hilo liweze kutatuliwa.

Kwa upande wake mfanyabiashara anayeingiza gari visiwani hapa, Issa Kassimu Issa, alimthibitishia waziri huyo kuwepo kwa tatizo la kulipishwa ushuru mara mbili wa gari.

Alisema gari hiyo unapoingia Zanzibar kwa mara ya kwanza inalipiwa ushuru lakini pia unapotaka kuipeleka bara hutakiwa ilipiwe tena ushuru huo kutoka Mamlaka moja ambayo ni TRA.

Mfanyabiashara huyo alisema gari hiyo hiyo unapoishusha bara ikalipiwa ushuru na unapotaka kuiingiza Zanzibar haitozwi kodi jambo ambali alisema linasikitiosha.

“Wanafanya hivi makusudi ili wafanyabiashara wa Zanzibar washindwe kushusha mizigo hapa na waende kushusha bara, lakini waangalie wakifanya hivyo tutashindwa kufanya biashara hapa na hakuna atakayeweza kufanya biashara Zanzibar”, alisema Kassim Issa.

Hata hivyo Waziri huyo alisema anayachukua maelezo hayo yeye na maofisa wake na kuahidi kuyafanyia kazi kwani hiyo ni moja ya kero za Muungano.

Akiwa bandarini hapo alitembelea sehemu ya usafirishaji na uingizaji wa mizigo katika kituo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ili kujionea kero zinazoendelea Bandarini hapo.

Awali, waziri Samia alitembelea Chuo cha Ufundi (JKU) Mtoni na kujionea kisima kilichochimbwa kwa fedha za Mfuko wa wa jimbo na kuridhishwa na hatua hiyo.

2 comments:

  1. Ahh huwo usanii kila siku tunaambiwa eti mnayachukuliwa yakajadiliwe, hizo kero hazimaliziki kwa sababu upande mmoja wa muungano hauna nia nzuri kwa upande mwengine kinachoonekana hapo ni Mkoloni (Tanganyika) dhidi ya koloni lao (Zanzibar) kwa hiyo tutalalamika milelel kero hizo haziondoki. Na wakoloni walivo wajanja waziri wa muungano wote wanakuwa wazanzibari then wajisulubu wenyewe. Mimi nlishamgaa sana kuona eti wanaojadili kero (EPZ) wote ni wazanzibari (Bilali, Samia, Seif Iddi)wakati suala linahusu pande mbili za muungano kwa kweli hapa pana kizungumkuti flani tunafanywa watoto

    ReplyDelete
  2. "Eti wanaojadili kero(EPZ) wote ni Wazanzibari(Bilali, Samia,Seif iddi)"
    Eeeh.., mambo ya mchawi mpe mtoto alee hayoo!

    Ila mimi nadhani tatizo hapa ni wahadimu wenyewe, wanakwenda huko, wanaridhia au wanashindwa hoja wakirudi hapa wanasema uwongo!.."wenzetu wabaya"..wabaya, wakati mnaonekana kwenye runinga na magazeti mnacheka
    watu wasiwokubaliana kweli wanacheka?..ma..weee!!!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.