Uhaba wa nishati ya mafuta unaoikabili Zanzibar umeongeza ukali wa maisha baada ya nishati hiyo kuuzwa shilingi 6,000 kwa lita moja.
Mafuta ya petroli kwa wiki ya pili sasa yameadimika hali inayosababisha msongamano mkubwa wa gari katika vituo vya mafuta na katika baadhi ya vituo hivyo yakiuzwa kwa njia ya ulanguzi.
Walanguzi hao wanaouza mafuta hayo yakiwa kwenye madumu huuza lita moja kati ya shilingi 3,500 na 6,000 kwa lita moja hali ambayo imewasababishia wananchi kuwa katika wakati mgumu.
Kuadimika kwa nishati hiyo kumesababisha kuzorota kwa harakati mbali mbali za kimaisha, huku watu wengi wakishindwa kuutumia vyema muda wa uzalishaji wakishinda kwenye vituo wakisubiri mafuta.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tafauti, baadhi ya wamiliki wa gari walisema tatizo hilo linaendelea bila ya kupatiwa ufumbuzi wowote huku kimya kimetawala wananchi wakiendelea kuteseka.
Mmoja ya wananchi hao aliejitambulisha kwa jina la Abdalla Ali alisema kuwa alilazimika kununua mafuta kwa walanguzi kwa shilingi 6,000 kwa lita moja, na ilimlazimu kuyanunua kutokana na kuwa na mgonjwa, aliyelazwa hospitali.
Nae Meneja Kijangwani Petrol Station, Howingekao alisema tatizo la kuadimika kwa nishati ya mafuta ni kuisha kwa nishati hiyo katika hifadhi ‘Depot’ ya Mtoni.
Alisema kuwa katika sheli yake anapewa lita 15,000 ambazo hazitoshelezi mahitaji na ndio sababu inachangia wananchi kuona wanauziwa watu wachache mara huelezwa mafuta yamemaliza.
Hata hivyo alisema meli ya mafuta tangu Februari 15 mwezi huu ipo kwenye foleni Dar es Salam ikisubiri ipakie nishati hiyo ilete Zanzibar.
No comments:
Post a Comment