Habari za Punde

Waislamu Waaswa Kufuata Mwenendo wa Mtume Muhammad


Na Hasssan Hamad OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Al-hajj, Maalim Seif Sharif Hamad amesema katika kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), waislamu hawana budi kufuata mwenendo wa kiongozi huyo kwa vitendo, hali ambayo itadhihirisha mapenzi ya kweli kiongozi huyo wa kiislamu.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo huko Mtemani Wete alipokuwa akiwahutubia waislamu waliohudhuria hafla ya maulid ya kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa na Al-Madrasat Swiffat Nnabawiyyatil Kariym ya kilimahewa Wete Pemba.


Amesema waislamu wana kila sababu ya kusherehekea ujio wa kiongozi huyo kwa kuwa ndiye kiongozi aliyekuja kuwakomboa waislamu kutokana na madhila waliyokuwa wakiyapata kutoka kwa maadui wa Uislam.

Al-hajj Maalim Seif amewataka waislamu kuongoza juhudi katika kutafuta elimu na kutoa kipaumbele katika kuwapatia watoto elimu bora itakayowasaidia kutekeleza ibada zao kwa usahihi.

Amesema bado waislamu hawajaipa elimu uzito unaostahiki, na kutoa wito kwa waislamu wenye uwezo kuzisaidia madrasa ili ziweze kufikia lengo la kutoa elimu bora kwa vijana.

Katika hafla hiyo Makamu wa Kwanza wa Rais ameahidi kuchangia kompyuta mbili kwa ajili ya maendeleo ya madrasa hiyo.

Katika hatua nyengine Maalim Seif amekemea tabia ya baadhi ya waislamu kushiriki katika kughushi mitihani na kwamba kitendo hicho ni kinyume na maadili ya Uislamu.

Amesema iwapo waislamu na jamii kwa ujumla wataendeleza vitendo hivyo, taifa la baadaye linaweza kuwa na vijana wasiokuwa na elimu bora bali elimu ya kudanganya, jambo ambalo litarejesha nyuma maendeleo ya taifa.

Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Sheikh Jamal Abeid kutoka msikiti mkuu wa Ijumaa Wete, amesema sifa kubwa ya Mtume Muhammad (SAW) ilikuwa ni elimu, na kuwahimiza waislamu kuifuata sifa hiyo kwa vitendo, ili kudhihirisha mapenzi yao kwa kiongozi huyo.

Katika risala yao iliyosomwa na ustadh Mussa Juma, wanamadrasa hao wamesema licha ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa madrasa hiyo mwaka 1996 ikiwa na wanafunzi 10 hadi kufikia wanafunzi 205, inakabiliwa na baadhi ya changamoto zikiwemo uhaba wa madarasa ya kusomea.

Hassan Hamad (OMKR).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.