Haijui wapi itarudiana na Yanga
CAIRO, Misri
HATUA ya Shirikisho la Soka la Misri (EFA) kufuta mechi za kimataifa na za kirafiki za timu ya Taifa kwa kipindi cha mwezi mmoja, kimeushtua uongozi wa klabu ya Zamalek inayoshiriki Ligi ya Mabingwa
Afrika mwaka huu.
Taarifa zilizopatikana katika tovuti ya klabu ya Zamalek, zimefahamisha kuwa, uamuzi huo, umewaweka mabingwa hao wa Misri katika njia panda, wakishindwa kujua wapi watalipeleka pambano la marudiano
kati yao na Yanga ya Tanzania.
Uamuzi huo wa EFA ulioelezewa umetokana na kutokuwepo kwa hali ya usalama wa uhakika nchini humo, umekuja huku Zamalek ikiwa imepanga kucheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa ili kujipima kabla
mchezo wa marudiano dhdi ya Yanga, kwa kucheza na timu za taifa za Kenya na Uganda.
Wawakilishi hao wa Misri, walipanga mchezo huo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Yanga, ufanyike Machi 3, katika dimba la Arab Contractors jijini Cairo.
Ismail Youssef, Meneja msaidizi wa timu hiyo, amekaririwa na tovuti ya Zamalek akisema kitendo hicho cha EFA kinachohofia hali ya kutokuwepo usalama wa kutosha nchini humo, kinatia shaka ya kutokufanyika kwa
pambano lao na Yanga nchini humo.
"Kufutwa kwa mechi za timu ya taifa za kimataifa, ndio kusema Misri haiko tayari kuandaa mechi, hivyo mechi yetu na Yanga iliyopangwa kuchezwa Machi 3, hapa Cairo, iko katika wasiwasi wa kutochezwa,"
alisema kiungo huyo wa zamani wa Zamalek na Pharaohs.
"Hadi wakati huu, hatujawa na uhakika kama tutacheza mechi ya marudiano Misri au la, nafikiri katika hali kama hii, hakuna haja kuwaruhusu wachezaji wetu wajiunge na timu ya Taifa,", alifahamisha.
Alisema kutokuwapeleka wachezaji hao kwenye kikosi cha Pharaohs, kutasaidia katika maandalizi ya Zamalek inayojiandaa na mchezo dhidi ya Yanga.
Hapo kabla, Zamalek ilipinga ombi lililowasilishwa kwao na Yanga, ambayo ilitaka timu hizo zicheze mechi moja tu kufuatia tukio la ghasia lililosababisha vifo vya watu 74 kwenye mji wa Port Said baada
ya mechi ya Ligi Kuu ya Misri kati ya klabu za Al Masry na Al Ahly

No comments:
Post a Comment