Na Mwantanga Ame
BAADA ya serikali kutangaza azma ya kupambana na tatizo la mifugo kuranda ovyo katika Mji wa Zanzibar watu wasiojulikana wametawanya vipeprushi kwa ajili ya kuitaka serikali kusitisha utekelezaji wa zoezi hilo.
Vipeperushi hivyo vinapinga uamuzi huo wa serikali kwa kudai kuwa hauwatendei haki wafugaji kwa vile hiyo ni sehemu ya ajira zao.
Akizungumza na Zanzibar Leo, mkuu wa wilaya ya Mjini, Abdi Mahmoud, alisema ni kweli kumekuwa na aina hiyo ya vitisho huku akionesha moja ya kipeperushi hicho.
Alisema imekuwa ni tabia ya baadhi ya watu wanaojishughulisha na ufugaji wa wanyama kutoa vitisho pale serikali inapoandaa zoezi la usafi wa Mji.
Alisema kutokana na hali hiyo msimamo wa serikali bado upo pale pale kusimamia zoezi hilo lifanyike kwani tayari kuna marufuku kadhaa zilizoandaliwa na watu wamekuwa wakaidi kutii amri hizo.
Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo, mkuu huyo wa wilaya alisema hivi sasa kumekuwa na ongezeko la uchafuzi wa mji kutokana na baadhi ya watu kufanya vitendo hivyo kwa makusudi.
Akitoa mfano alisema baadhi ya watu wameamua kuzuia wafanyakazi wa Manispaa kutofanya kazi zao vyema katika majaa, kwa kuanzisha tabia ya kujisaidia haja kubwa nyakati za usiku huku wengine wakiuza samaki kwa muda huo kwa dhamira ya kuona hakuna watumishi wa Manispaa wanaoweza kuwakamata.
Alisema kuendelea kwa vitendo hivyo, viongozi wa wilaya wamemkamata mtu mmoja aliyesadikiwa kufanya vitendo vya kujisaidia haja kubwa katika jaa ambapo wengine hawakuweza kupatikana.
Mkuu huyo wa wilaya alisema watu hao wameamua kuendesha vitendo hivyo kwa dhamira ya kuwafanya wafanyakazi wa Baraza la Manispaa washindwe kufanya usafi.
Hata hivyo, Mkuu huyo alisema serikali itaendeleza zoezi lake la kuona mji wa Zanzibar unakuwa safi ikiwa pamoja na kudhibiti wanyama kuranda ovyo.
Agizo la awali lilitolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akizungumza na uongozi wa Manispaa na Halmashauri katika hitimisho la ziara yake katika mikoa mitatu ya Zanzibar.
Amri hiyo iliendelea kusisitizwa na Makamu wa Pili wa Rais balozi Seif Ali Iddi, pale alipotoa kauli ya kulitaka Baraza la Manispaa na Halmashauri kudhibiti wanyama kuranda ovyo.

No comments:
Post a Comment