Habari za Punde

Balozi Seif Akamilisha Utoaji Madawati Jimboni

Na Mwantanga Ame

MBUNGE wa Jimbo la Kitope, Balozi Seif Ali Iddi, amesema baada ya kukamilisha zoezi la kuwapatia madawati wanafuzi wa skuli za Jimbo hilo anakusudia kubadili mazingira ya majengo ya madrasa kwa kuyajenga upya kwa mfumo wa kisasa.

Ahadi hiyo aliitoa Mke wa Makamu wa Pili wa Rais ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, Mama Asha Seif Iddi, wakati akiwahutubia wanafunzi, walimu na wazazi wa Madrasa Najah ya Vuga Mkadini wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.


Kwa niaba ya Mbunge huyo Mama Asha, alisema wameamua kulibadili eneo hilo ili kuweza kuwa na mazingira ya kisasa katika kupata elimu ya akhera.

Alisema vyuo vya madrasa ni muhimu katika kuwajenga watoto katika maadili mema jambo ambalo vinahitaji kuwa na mazingira mazuri yataweza kumjenga mtoto kupenda elimu hiyo.

Alisema inasikitisha kuona mengi ya majengo ya vyuo vya Madrasa hayatoi ushawishi wa kuwavutia watoto kupata elimu ya dini, kutokana na kuwa ni madogo jambo ambao husababisha wanafunzi kubanana kwa hali ya juu huku mfumo wa upatikanaji wa hewa safi ukiwa ni mdogo.

Balozi Seif, alisema kutokana na hali hiyo kuanzia sasa uongozi wa Jimbo hilo, utahakikisha unayabadili majengo ya madrasa kwa kuyajenga yakiwa katika mfumo wa kisasa huku yakiwekewa vifaa muhimu vya usafi na vipoza hewa.

Alisema inafurahisha kuona hivi sasa Jimbo hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwaweka mazingira bora wanafunzi wa skuli kwa kuwapatia vikalio na hakuna mwanafunzi anaekaa chini hivi sasa.

Balozi Seif ambaye pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisema haoni haja ya kwanini hatua kama hiyo asiichukue kwa wanafunzi wa vyuo vya madrasa ndani ya Jimbo hilo, kwani nao wanahitaji kupata elimu wakiwa katika mazingira bora.

Balozi Seif, aliwataka wazazi kuacha tabia ya kudharau elimu ya dini kutokana na kuwapa huduma duni watoto wao pale wanapokwenda vyuoni.

Akitoa mfano alisema inasikitisha kuona baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwapa kanga zilizochakaa ama kuchanika watoto wa kike waendapo vyuoni, huku mikoba wanayotumia kuhifadhia Qur-ani ikiwa ni ile ya vipolo vya unga na mchele.

Alisema hiyo ni tabia mbovu inayofaa kukemewa na jamii kwa kuona inaidharau elimu ya dini ilhali wanaofaanya hivyo wakiwa wanawapa mazigira bora watoto wao pale wanapoenda Skuli.

“Utaona mtoto ameachwa akienda chuoni nguo zimechanika ama kanga anapewa ya jikoni huku juzuu yake kaweka katika mifuko ya unga na mchele, huu sio utaratibu mzuri tunaidharau dini yetu, kwa nini akenda skuli nguo anapigiwa pasi na ananunuliwa rasket iweje chuoni hayo asipewe vitu kama hivyo” alisema Mbunge huyo.

Aidha, Mbunge huyo aliwataka wazazi hao kujitolea kulipia ada za masomo kwa walimu wa Madrasa kutokana na hivi sasa baadhi ya wazazi kuacha tabia ya kutoa mchango wa wiki kwa mwalimu.

Hali hiyo alisema inachangia kuwafanya walimu kutowahudumia vizuri wanafunzi wao na kulazimika kutenga muda wa kutafuta mahitaji ya maisha yao tofauti na zamani mwalimu wa madrasa huweza kuendesha maisha yake kwa kutumia michango ya wazazi ambayo huitoa kila siku ya Alkhamis.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.