Habari za Punde

Jihad Ajitwisha Udhamini ZFA

Ni baada ya maji kukifika shingoni chama hicho

Na Salum Vuai, Maelezo

BAADA ya maji kukifika shingoni Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan, ameamua kulivalia njuga suala la udhamini wa ligi kuu ya soka Zanzibar.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa soka na ZFA ulioitishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad katika hoteli ya Bwawani juzi, Jihad alisema amefanikiwa kuishawishi kampuni moja kudhamini ligi kuu msimu ujao baada ingawa amedai ni mapema kuitaja kwa sasa.


Waziri huyo alieleza kuwa, amelazimika kujitosa yeye mwenyewe kuzipigia hodi kampuni mbalimbali baada ya kushauriwa mara kadhaa na viongozi wa ZFA, na kwamba hatua hiyo imefikia pahala pa kutia matumaini.

Akizungumzia misuguano kati ya wadau na ZFA, Jihad alisema hiyo ni dalili ya nia ya kutaka mafanikio, na kwamba kuwepo kwake kunasaidia kuharakisha maendeleo, ili mradi wanaotoa mawazo wawe na mitazamo chanya na wasifanye hivyo kwa ajili ya kuwakomoa au kutowapenda watu fulani.

"Hata zile tafauti za TFF na ZFA tumezifanyia kazi kwa kumuita Rais wa TFF Leodgar Tenga na timu yake, tumefanya mazungumzo na kukubaliana juu ya njia bora za kushirikiana kwa kuzingatia ZFA inapata haki zake kutokana na miradi ya FIFA", alifafanua.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Ali Mwinyikai, alisema kimsingi michezo katika karne hii ni fedha, hivyo ili kuwashawishi wadhamini kubeba gharama, ni lazima wanaobebwa wawe wakweli na wawazi na kuepuka ubabaishaji.

Alikumbushia udhamini wa kampuni ya simu ya Zantel miaka kadhaa iliyopita, kwa kusema wadhamini hao walitokwa imani kutokana na ubabaishaji na kukosekana uwazi wa upande wa pili yaani ZFA, hali iliyoirejesha ligi kuu ya Zanzibar katika uyatima.

Aidha alifahamisha kuwa ZFA ndiyo inayopata fedha nyingi kutoka serikalini kuliko vyama vyengine, ambapo mbali na shilingi milioni tano za ruzuku ya kila mwaka, pia serikali imetenga shilingi milioni 100 za kuihudumia timu ya taifa ingawa ZFA haipewi mikononi.

Akijibu hoja iliyoibuliwa na Ofisa Habari wa ZFA Munir Zakaria aliyedai kuwa siasa ndiyo iliyoua soka Zanzibar, Dk. Mwinyikai alisema madai hayo hayana msingi kwani mwaka 1995 wakati Tanzania ilipoingia katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi huku hali ya kisiasa ikiwa tete, ndipo Zanzibar ilipotwaa ubingwa wa Chalenji kwa mara ya kwanza katika historia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.