Habari za Punde

Klabu Ligi Kuu Zaishtukia TFF

Zadai zimedanganywa kuhusu kampuni ya Ligi Kuu

Na Mwandishi Maalumu

VIONGOZI wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kesho watakuwa na kikao kizito mjini Dar es Salaam, kujadili ‘changa la macho’ walilopigwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kwa mujibu wa habari za ndani zilizonukuliwa kutoka blogi ya ‘bongostaz’ ambayo imezipata kutoka kwa umoja wa klabu za VPL, kikao hicho kinafuatia TFF kuwahadaa kuhusu suala la kampuni ya Ligi Kuu.

Kiongozi mmoja wa klabu, ameiambia ‘bongostaz’ jana, kwamba Kamati ya Ligi Kuu iliyoundwa na TFF haikuwasilisha hoja ya Kampuni katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika Februari 12, mwaka huu.
Kiongozi huyo, alisema mtu ambaye anaingia kwenye Kamati ya Utendaji ya TFF kutoka kwenye Kamati yao ni Mwenyekiti wao pekee, Wallace Karia.


“Karia pekee ndiye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ambaye kutoka kwenye Kamati ya Ligi Kuu iliyoundwa na TFF anaingia kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji, lakini ajabu, habari ambazo tumezipata ni kwamba hajawasilisha hoja hiyo na hakuna mtu aliyehoji kuhusu suala la kampuni,” alisema kiongozi huyo.

Kiongozi huyo, alimlalamikia Rais wa TFF pia, Leodgar Chillah Tenga, kwamba aliziahidi klabu kuwa yeye mwenyewe atasimamia hadi kuhakikisha suala la kampuni linaingia kwenye Kamati ya Utendaji, lakini ajabu ameendesha kikao cha Kamati ya Utendaji bila kujadili kampuni.

“Mbaya zaidi ni kwamba, sasa wanakwenda kwenye Mkutano Mkuu (utakaohusisha uchaguzi Mkuu pia) bila ajenda ya kampuni,” alilalamika kiongozi huyo.

Akiizungumzia Kamati ya Ligi Kuu, kiongozi huyo alisema kwamba ipo kama kivuli na haihusiki na uendeshaji wa Ligi Kuu

“Karia anaishi nje ya Dar es Salaam, Ofisa waliyesema ataajiriwa, hadi leo hajaajiriwa. Kazi zote zinafanywa na ofisi ya Saadi Kawamba kama zamani,” alisema.

Kamati ya Ligi Kuu inaundwa na Wallace Karia (Mwenyekiti), Said Mohamed (Makamu Mwenyekiti), Damas Ndumbaro, Yahya Ahmed, Meja Charles Mbuge, Steven Mguto, Geoffrey ‘Kaburu’ Nyange, Seif Ahmed, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hemedi Msangi na Henry Kabera (Wajumbe).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.