KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania Jan Poulsen, amesema makocha wa soka Zanzibar na Tanzania kwa jumla, wanapaswa kubadilika na kufahamu mbinu za kisasa kama kweli wanataka kupiga hatua kitaifa na kimataifa.
Poulsen ambaye anaendelea kuwapiga msasa makocha wa klabu mbalimbali katika semina inayofanyika kwenye uwanja wa Amaan, amesema soka la sasa linachewa kisayansi zaidi hivyo makocha hawana budi kwenda na wakati ili waweze kujenga timu bora.
"Soka sasa linachezwa kisayansi na teknolojia mpya hata FIFA inahangaika kutafuta njia za kuliimarisha zaidi kwa kubadili kanuni na sheria zake, hivyo makocha na wacheaji nao waalaziika kufuata njia hiyo", alifahamisha.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa makocha hao Saidi Omar Kwimbi anayeinoa Miembeni United inayooongoza ligi kuu ya Zanzibar, alisema mafunzo hayo yana faida kubwa kwao kwa vile yanawaongezea ujuzi maradufu na kuwapa mbinu za kuzibadilisha timu zao.
"Ni mafunzo mazuri kwetu, yanasaidia kuziimarisha timu zetu ili ziweze kuhimili ushindani katika soka la ndani na nje", alieleza.
Alisema mafunzo hayo yanayotolewa kinadharia na vitendo, ni changamoto kubwa kwao na kuwasihi makocha wenzake wasidharau fursa kama hizo kwani ni muhimu sana kwao katika kuongeza sifa katika CV zao.
Semina hiyo ya siku kumi iliyoanza Machi 3, mwaka huu, inaendeshwa kwa pamoja na kocha huyo, Abdelfatah Abbas wa kutoka Misri ambaye anafundisha timu za vijana hapa Zanzibar, pamoja na Sunday Kayuni kutoka TFF.
No comments:
Post a Comment