Habari za Punde

Maalim Seif Aanza Kutembelea Ofisi za Serikali

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akichukua dondoo wakati mkurugenzi wa mipango, sera na utafiti Bi Fauzia Mwita (kulia) akiwasilisha muhtasari wa majukumu yake.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akipata maelezo kutoka kwa mkurugenzi wa uendeshaji na utumishi Bw. Ali Bakar, wakati alipofanya ziara ya kutembelea ofisi mbali mbali za Ofisi hiyo. (Picha, Salmin Said, OMKR).

Na Hassan Hamad (OMKR)

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad leo ameanza rasmi ziara za kutembelea ofisi za serikali na kuwataka wakuu wa Idara kuwa na usimamizi endelevu wa majukumu kwa wafanyakazi wao, katika kuhakikisha kuwa utekelezaji wake unakwenda kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi.

Maalim Seif ambaye ameanza ziara hiyo katika ofisi yake kwa kutembelea na kusikiliza utekelezaji wa majukumu katika Idara ya utumishi na uendeshaji pamoja na Idara ya Mipango, Sera na Utafiti, amewataka watendaji wa ofisi hiyo kuwa na mikakati imara ya utendaji kazi, ili iwe kigezo kwa ofisi nyengine.


Amewataka wafanyakazi hao kuendelea kufanya kazi kwa mashirikiano na kubadilika kiutendaji, kulingana na mabadiliko na mahitaji ya ofisi, ili kwenda sambamba na hadhi ya ofisi hiyo.

Katika mazungumzo yake na wafanyakazi hao, Makamu wa Kwanza wa Raisi amewaagiza wakurugenzi na maofisa wa Idara hizo kuachana na muhali katika kusimamia majukumu yao, huku wakizingatia haki na utu wa wafanyakazi, kwa lengo la kuepuka manyanyaso katika sehemu za kazi.

Katika mazungumzo hayo, Maalim Seif pia alihoji juu upatikanaji wa malipo ya muda wa ziada “Overtime” kwa wafanyakazi, na kutaka wafanyakazi wapatiwe malipo hayo kwa mujibu wa kazi wanazozifanya.

Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais amemtaka muangalizi wa ofisi hiyo kuwasiliana na wataalamu wa baraza la manispaa ili kuimarifa bustani ya eneo hilo.

Mapema akitoa muhtasari wa majukumu na utekelezaji wa ofisi yake, Mkurugenzi Idara ya Mipango, Sera na Utafiti bibi Fauzia Mwita, amesema pamoja na kuratibu shughuli hizo, idara hiyo imeweza kuandaa miradi nane ya maendeleo ukiwemo mradi wa kukabiliana na maambukizi ya UKIMWI kwa watumiaji wa dawa za kulevya.

Miradi mengine ni pamoja na mradi wa kuangamiza kunguru, mradi wa maji machafu msingini, mradi wa kunyanyua kiwango cha elimu ya mazingira na mradi wa kujenga kituo cha kurekebisha tabia, miradi ambayo kwa pamoja imepangwa kutekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.

Nae Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi Bw. Ali Bakar amesema licha ya changamoto mbali mbali zinazoikabili Idara hiyo, wanafanya kazi zao vizuri ikiwa ni pamoja na kushughulikia maslahi ya wafanyakazi wanapostaafu, ambapo hupatikana muda mfupi tu baada ya kustaafu.

Shughuli nyengine za Idara hiyo ni pamoja na kupanga mipango ya ajira kulingana na mahitaji pamoja na kushughulikia mafunzo ya muda mfupi na mrefu ndani na nje ya nchi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dr. Omar Dadi Shajak kwa upande wake amesema ofisi hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbali mbali katika utendaji wake ikiwa ni pamoja na uhaba wa sehemu za kufanyika kazi, hali inayopelekea msongamano wa wafanyakazi katika baadhi ya ofisi.

Hata hivyo amesema wako njiani kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo kwa kutafuta jengo jengine ambalo litakidhi haja hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.