Habari za Punde

Mv Maendeleo Yakwama Makoongwe Karibu na Bandari ya Mkoani



Picha hii ni Meli ya Mv. Maendeleo ikiwa katika eneo la bandari ya Mkoani ikiwa inashusha abiria wiki iliyopita. Meli hiyo leo imekwama katika eneo la bandari ya Mkoani Kisiwani Pemba ikiwa na abiria kadhaa wakisubiri kuona khatima yao kwani imegenda karibu na bandari ya Mkoani eneo la Makoongwe Pemba. Meli hiyo iliondoka jana saa 3 usiku na kawaida saa 11:30 huwa imeshafika bandarini na abiria kushushwa saa 1:00 asubuhi lakini kutokana na tatizo abiria wameanza kushushwa saa 5:30 hadi saa 10 bado walikuwa wakiendelea kushushwa


ABIRIA zaidi 400 wamekwama baada ya meli ya Mv. Maendeleo iliyokuwa inasafiri kutoka Unguja kwenda Pemba kushindwa kushusha abiria katika bandari ya Mkoani, Kisiwani Pemba hapo jana. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu waliokuwa ndani ya meli hiyo waliozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu walisema meli hiyo ilipoteza muelekeo na kuingia sehemu ambayo ilipelekea kukwama.

Meli hiyo inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilipoteza mwelekeo wakati inajiandaa kufunga nanga na kusimama kwenye kina kifupi cha maji kilometa kama 100 kutoka bandari ya Mkoani ambayo hutumika kushusha abiria.


Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Abdallah Hussein Kombo alithibitisha kukwama kwa meli hiyo kwenye eneo lenye kina kifupi cha maji ambapo alisema tukio hilo halikuweza hakujasababisha madhara yoyote kwa abiria waliokuwemo ndani ya meli hiyo wala hakuna athari kwa meli yenyewe.

Alisema kazi ya kuwaondoa abiria kwenye meli hiyo na kuwafikisha nchi kavu kisiwani Pemba ilifanyika baada ya serikali kupata taarifa hiyo na kutumwa maafisa wake kushughulikia suala hilo ambapo ilianza kuwashusha abiria ndani ya meli hiyo waliokwama na kuwashusha na kuwaingiza katika meli nyengine ya Mv Jitihada na meli za Jeshi la Wanamaji Zanzibar (KMKM) ambazo zilifanya kazi kubwa ya kuwafikisha bandarini.

“Taarifa zilizopo ni kuwa abiria wote zaidi ya 400 wako salama, na hakuna athari zilizopatikana katika tukio hilo ” alisema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Kaimu huyo alisema meli hiyo iliingia kwenye kina kifupi cha maji wakati inageuza mwelekeo kuelekea baharini baada ya kukaribia bandari ya Mkoani ikiwa ni hatua ya awali ya kujiandaa kushusha nanga na hivyo kuingia sehemu ambayo baadae ilikwama.

“Meli inapokaribia bandarini inaogozwa na boya, lakini inavyoelekea boya lilisukumwa na maji likahamia kwenye kina kifupi na kusababisha meli kwenda huko na kukwama, lakini serikali ndio inajitahidi kuhakikisha wananchi wote waweze kushuka kwa salama” alisema Kombo.

Kepteni wa meli hiyo alikuwa ni Hamad Suleiman Kombo na kwamba mbali na kubeba zaidi ya abiria 400 pia ilikuwa na wafanyakazi 19 wanaifanya kazi ndani ya meli hiyo.

Wakizungumza kwa njia ya simu baadhi ya abiria waliokwama ndani ya meli hiyo walisema walikuwa na khofu kubwa kutokana na kuwa wahusika wa meli hiyo hawajasema lolote kwa abiria wao jambo amablo lilizusha khofu kuwa miongoni mwa abiria.

Walisema tatizo lililokuwemo ndani ya meli hiyo kulikuwa na joto kali, ukosefu wa maji huku chakula kikikosekana jambo ambalo lilizusha zogo kubwa kutokana na wanawake wengi kushishwa na hali hiyo huku watoto wakilia ovyo kutokana na hali ya joto kali lililokuwemo.

“Sijui tulikuwa abiria wangapi lakini kwa kweli naona meli ilikuwa imejaa sana lakini hilo joto na kuwa hakuan chakula na sisi tuliondoka Unguja saa 3 usiku basi tukawa tumechoka sana na hivyo tumefika tukiwa tumechoka pia lakini ndio tukawa tumekaa tu ndani ya meli hatujui chochote kianchoendelea khofu ndio ikazidi maana mtu akitafunwa na nyoka hata ukuti huwa anauogopa…. Na sisi wazanzibari tuhstafunwa na hatujasahau bado” alisema Asha Ahmed Mkaazi wa Machomanne Kisiwani Pemba aliyekuwemo ndani ya meli hiyo.

Aidha wananchi waliokuwepo ndani ya meli hiyo wamelalamikia mamlaka zinazohusika kushindwa kuchukua hatua za dharura wakati inapotokea tatizo katika mmeli hizo na pia kulalamikia hali mbaya iliyokuwa ndani ya meli hiyo.

“Kwa kweli ni shida kubwa sana uiyotupata maana tumetoka huko usiku tunasubiri tushushwe hatushushwi kila mmoja tafrani na humu kuna watoto wadogo wanalia tu, kuna watu wazima ambao wengine ni wagonjwa wa presha basi ni balaa tu” alisema Sabri Abdallah mfanyabiashara wa Unguja aliyekuwa akenda Pemba .

Meli ya Mv. Maendeleo iliondoka juzi usiku majira ya saa 3 na ilitarajiwa kufika saa 11:30 asubuhi na kushusha abiria lakini abiria hao waliokuwemo ndani ya meli hiyo wamekaa zaidi ya saa 6 ndani ya meli hiyo kabla ya meli za Mv. Jitihada na boti za KMKM kutakiwa kwenda kuwashusha abairia hao na kuwapeleka katika bandari ya Mkoani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbali mbali zinasema kwamba meli hiyo aidha ilipoteza muelekeo kutokana na upepo mkali uliovuma jana na kusababisha maboya kusogea mbele na kuchukuliwa na upepo huo au kempteni huyo kuchukuliwa na usingizi na kuipelekea meli hiyo pasipo pahala pake ambapo ilipanda juu ya mchanga.

“Sisi ni wazoefu wa pahala pale, amma ni upepo mkali uliochukua yale maboya na kuyapoteza na kusabaisha kapteni kushindwa kuona njia au kapteni kauchapa usingizi na ndio maana akaipeleka meli kwneye fungu la mchanga…maana pale kukiwa na maji huwezi kuona unaweza ukaona ni sehemu ya kawaida kwa kuwa kuna maji lakini bwana eeeeh ni fungua la mchanga” alisema mzee mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake kazetini ambaye ni mzoefu wa masuala ya usafiri.

Mv Maendeleo ni miongoni mwa meli mbili kubwa zilizonunuliwa wakati wa awamu ya kwanza ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Mv Mapinduzi iliuzwa mwaka 2010 kwa uchakavu na ikawa inapigiwa makelele sana na wajumbe wa baraza la wawakilishi kuwa itasababisha madhara kwa wananchi kutokana na uchakavu huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.