Habari za Punde

Mwakilishi wa Kiwani Aandaa Hoja Binafsi Kuchunguzwa Shirika la Umeme

Na Ramadhan Ali-Maelezo

Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Kiwani Pemba (CUF) Hija Hassan Hija amekusudia kupeleka Hoja binafsi katika Kikao cha Baraza hilo kitakachoanza Machi 28 mwaka huu ili kulitaka Baraza kuunda Kamati teule ya kulichunguza Shirika la Umeme Zanzibar ZECO kutokana na madai kuwa utendaji wake ni mbovu.

Hija ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo Raha leo Zanzibar kuhusiana na azma yake hiyo na kwamba tayari amekamilisha masharti ya sheria na kanuni za kuwasilisha Hoja hiyo.


Amesema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa Unguja na Pemba kuhusu Shirika hilo ambayo yameendelea kudumu bila kupatiwa ufumbuzi na kwamba amefanya uchunguzi wa kutosha kubaini ukweli wa malalamiko hayo.

Amesema miongoni mwa malalamiko hayo ni kuwepo kwa upotevu mkubwa wa fedha unaosababishwa na mafundi wa Shirika hilo kuwaungia umeme wananchi kiholela bila kufuata taratibu za Shirika ambapo pia wananchi wanaofuata taratibu za Shirika kwa ajili ya kuungiwa umeme hupata usumbufu mkubwa.

Amedai kuwa miongoni mwa malalamiko hayo ni pamoja na ubaguzi katika ajira ambapo watoto wa viongozi wa Shirika ndio wanaoajiriwa pamoja na uuzwaji wa mali za Shirika bila kufuata taratibu za kisheria.

Hija ameongezea kuwa pamoja na matatizo hayo lakini pia Suala la Majenereta 32 yaliyonunuliwa na Serikali kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa huduma ya umeme pale umeme unapokatika lakini haionekani kusaidia upungufu wa tatizo hilo la umeme.

Aidha amebainisha kuwa kuna Kampuni ambayo imeingia mkataba na Serikali kwa ajili ya kuyafanyia matengenezo Majenereta hayo ambayo hugharimu pesa nyingi kila mwezi lakini hayaonekani faida yake kwani Majenereta hayo huwa hayafanyi kazi.

Ameongeza kuwa kuna limbikizo kubwa la deni linalodaiwa Shirika hilo la ZECO na Shirika la umeme la Tanzania TANESCO ambalo ni zaidi ya Bilioni 15 lakini mikakati ya kulipa deni hilo haieleweki.

Mwakilishi huyo ambaye alikuwa na vielelezo mbali mbali vinavyothibitisha malalamiko ya wananchi hao zikiwemo Risiti zisizotambulika kisheria aliongeza kuwa Gazeti la Serikali la Habari Leo miaka mine iliyopita lilindika habari juu ya ufujaji wa pesa katika Shirika hilo lakini pia Shirika hilo la ZECO limeshindwa kukanusha taarifa hizo.

Kutokana na madai hayo Mwakilishi huyo amesema anaimani Wajumbe wanzake wa Baraza hilo watamuunga mkono juu ya Hoja yake na hatimaye kuundwa kwa Tume hiyo ili kuchunguza madai yake hayo.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 21/03/2012

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.