Habari za Punde

'ZFA Rudisheni Hadhi ya Soka la Zanzibar' - Maalim Seif

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Dr. Ali Mwinyikai akizungumza katika mkutano wa wadau wa michezo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko hoteli ya Bwawani.
Waziri ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Abdillahi Jihadi Hassan akizungumza katika mkutano wa wadau wa michezo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko hoteli ya Bwawani.
Mdau wa michezo kutoka timu ya mpira wa miguu Zanzibar (New Genaration) akitoa maoni yake kwenye mkutano wa wadau wa mpira wa miguu Zanzibar, huko hoteli ya Bwawani.
Wadau wa michezo wasikiliza maoni ya wadau mbali mbali kwenye mkutano wa wadau uliokuwa chini ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko Bwawani.

Na Hassan Hamad OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amekitaka chama cha michezo Zanzibar (ZFA) kufanya kazi za ziada ili kuhakikisha kuwa soka la Zanzibar linarejea katika hadhi yake ya awali.

Amesema Zanzibar imekuwa wasindikizaji wa michezo mbali mbali ukiwemo mchezo wa soka, na kutaka juhudi za makusudi zichukuliwe ili soka la wanaume na wanawake liweze kurejea.

Makamu wa Kwanza wa Rais ameeleza hayo leo katika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar alipokuwa akizungumza na wadau wa mpira wa miguu, katika mkutano maalum wenye lengo la kuinua hadhi ya soka Zanzibar.


Amesema ni lazima Zanzibar ijipange ili kurejesha soka na kuvutia wanasoka wazalendo, badala ya kushabikia soka la Ulaya na kuliwacha la hapa nyumbani.

Ameitaka ZFA kukubali kukosolewa na kuchukua mawazo ya watu wengine ili kukuza soka la Zanzibar ambalo amesema limerudi nyuma.

Sambamba na hilo Maalim Seif amemtaka mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar kuifuatilia katiba ya ZFA ili kuhakikisha kuwa inafanyiwa marekebisho ya haraka ili iweze kwenda na wakati.

Wadau mbali mbali wa mpira wa miguu wanaume na wanawake wamekishutumu chama cha ZFA kuwa kimepoteza mwelekeo na kutaka uongozi wa chama hicho uwajibishwe ili kutoa nafasi ya kuendeleza michezo nchini.

Makamu mwenyekiti wa ZFA Bw. Ali Mohd Ali amesema licha ya shutuma hizo lakini chama hicho kinafanya vizuri na hawawezi kujiuzulu.

Amesema iwapo watakuja viongozi wengine wanaweza kufanya mabaya zaidi kuliko hayo yanayoshutumiwa kufanywa na uongozi uliopo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.