Habari za Punde

Balozi Seif Afungua Semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Kuhusiana na MKUZA

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wanaoshiriki Semina ya Siku Moja inayohusu utekelezaji wa Mkuza wakisikiliza Hotuba ya Ufunguzi iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo Pichani huko kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Neptune Pwani Mchangani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Picha pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar baada ya kuifungua Semina ya Utekelezaji wa Mkuza nje wa ukumbi wa Hoteli ya Neptune Pwani Mchangani.

Juhudi za kupambana na Umaskini hapa Nchini ni vyema zikajikita zaidi katika kuimarisha Uchumi sambamba na huduma za Kijamii kwa lengo la kustawisha maisha bora ya Wananchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema hayo wakati akiifungua Semina ya siku mbili ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar inayohusu utekelezaji wa Mpango wa Kupunguza  Umaskini Zanzibar { MKUZA } inayofanyika katika Hoteli ya Neptune Pwani Mchangani.

Balozi Seif alisema wimbi la umaskini hushamiri iwapo jamii itakosa huduma za Elimu, ongezeko la uzazi katika umri mdogo, ukosefu wa usawa wa kijinsia pamoja na uchumi duni kwa akina mama ambao ndio wengi katika familia.


Balozi Seif alisema Umoja wa Mataifa umepitisha Azimio la utekelezaji wa Malengo la Milenia ili Dunia iondokane na umaskini ifikapo mwaka 2015 na kuzitaka Nchi Wanachama hasa zinazoendelea kujipangia mikakati ya kuuondoa Umaskini kwa kupitia utekelezaji wa Mipango yao ya maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba Serikali imo katika hatua za kupambana na umaskini kupitia utekelezaji wa Mkuza ingawa Wananchi waliowengi bado hawajaelewa Mpango huu.

Alieleza kwamba yapo mafanikio makubwa yamepatikana katika huduma za Kijamii zikiwemo Elimu, Afya na huduma za Maji safi mafanikio yanayoonekana zaidi kwenye kupunguza umaskini usio wa kipato.

Akizungumzia changamoto zilizojichomoza wakati wa utekelezaji wa Mkuza Balozi Seif alisema Mfumko wa bei umekuwa bado tatizo kinyume na lengo la chini ya asilimia 10% ukiathiriwa zaidi na ongezeko la bei ya mafuta na chakula katika soko la Dunia.

Akigusia Ukuaji mdogo wa Sekta ya Kilimo wa asilimia 4.6 Balozi Seif alisema unaonekana kushusha mchango wa Sekta hiyo katika pato la Taifa wakati Sekta ya Kilimo bado ni muajiri Mkuu wa nguvu kazi ya Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba hali hiyo imechangia kuwa na mafanikio madogo katika kuhakikisha kuwepo kwa usalama wa chakula.

Semina hiyo ya siku mbili inahusisha Mada kadhaa ikiwa pamoja na Mipango ya Maendeleo, Mapitio ya Dira 
ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020, Matokeo muhimu katika uchagumbuzi wa matumizi ya kaya pamoja na maandalizi ya Bajeti na mahusiano na Mkuza.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.