Hatuna Nia Kujenga Hospitali Kubwa Zaidi ya Mnazimmoja-Waziri
Husna Mohammed
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema haioni haja ya kujengwa hospitali kubwa nyengine baada ya ile ya Mnazimmoja.
Waziri wa Afya, Juma Duni, aliyasema hayo jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea mjini hapa, wakati alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi Mbarouk Wadi Mtando, aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kujenga hospitali nyengine kubwa itakayoweza kukidhi majhitaji ya wenyeji na wageni wanaoishi hapa.
Waziri huyo alisema kwa sasa Serikali haioni haja ya kujenga kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutaka kuzipandisha daraja hospitali za vijiji na kuwa hospitali za Wilaya zitakazotoa huduma zote za matibabu.
Sababu nyengine alizozitaja ni pamoja na kuvifanyia ukarabati mkubwa vituo vya afya Unguja na Pemba na kuweka mahitaji ya vituo kwa ajili ya uchunguzi na vifaa vya kisasa.
Aidha Waziri huyo alisema Serikali inakusudia kujenga nyumba za madaktari kwenye hospitali na vituo vyote na kuhakikisha dawa zinazohitajika kulingana na magonjwa ya pahala husika zinapatikana.
Kuhakikisha kunakuwa na utaratibu mazuri wa rufaa ya wagonjwa ambao utadhibiti watu kwenda hospitali ya Mnazimmoja ila kwa watakaopewa rufaa.
Waziri Duni, aliongeza kuwa kama hayo yatawezekana basi utafuata utaratibu wa rufaa kama inavyotakiwa ama kupunguza idadi ya wagonjwa kurundikana na kuwapunguzia adha za kutafuta matibabu mjini.
Hata hivyo, Waziri huyo alisema eneo la kujengwa hospitali kubwa ya kufundishia madaktari ambayo itakuwa na huduma na vifaa vyote vinavyohitajika imeshatengwa ambapo mipango ya Serikali ikikamilika hospitali hiyo itajengwa.
‘Kliniki Nyingi Mnazimmoja Kuhamishiwa Kiwanda cha Dawa’
WIZARA ya Afya Zanzibar, imesema ina mpango wa jengo lililokuwa kiwanda cha dawa kuweka kliniki za magonjwa mbalimbali.
Akijibu swali la Mbarouk Mussa Mtando (Mkwajuni), aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuanzisha au kujenga hospitali nyengine badala ya kiwanda hicho.
Waziri wa Afya Juma Duni Haji, alisema Serikali haina tena mpango wa kutengeneza dawa na badala yake jengo hilo litabadilishwa ambapo utanuzi wa hospitali ya Mnazimmoja utaendelezwa huko.
Alifahamisha kuwa hivi sasa jengo hilo linatumiwa na mradi wa kupunguza vifo vya mama na mtoto, bodi ya Chakula, dawa na vipodozi, mradi wa dawa wa DANIDA na kitengo cha marekebisho ya viungo na mifupa.
“Hivi sasa mipango inakaribia kukamilika, kliniki nyingi za hospitali ya Mnazi mmoja zitahamishiwa kwenye jengo hilo kupitia ufadhili wa Norway”, alisema.
Kutokana na maelezo hayo Waziri Duni, alisema Serikali imeona ni bora kununua dawa kuliko kuendelea kuzalisha dawa katika kiwanda hicho kutokana na gharama kubwa ya kukiendesha.
Oman Yapatiwa Eneo Jipya Ujenzi Ofisi Zake
UBALOZI mdogo wa Oman utajenga ofisi zake za kudumu eneo la Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi Omar Shehe (Chakechake), aliyetaka kujua Serikali inafanya juhudi gani kuwapatia kiwanja kingine ubalozi wa Oman baada ya ile ya awali iliopo Shangani kuwa na harakati nyingi za kitalii.
Naibu Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Haji Mwadini Makame, alisema eneo la awali lililotengwa halifai kujenga nyumba yenye hadhi ya kidiplomasia kwa kuwa eneo hilo lina harakati nyingi za kibiashara na kitalii, hivyo linaweza kuathiri shughuli za usalama.
“Baada ya makubaliano hayo Serikali ya Zanzibar iliwapatia kiwanja chengine ubalozi huo katika eneo la Mazizini NA 34, kiwanja Nambari 120 Mei 2009 kwa kupatiwa mkataba nambari 936/2008 ili kuendeleza kiwanja hicho.
Naibu Waziri huyo alisema kuwa sehemu hiyo ina usalama na utulivu na pana sifa zote stahiki kwa shughuli za kidiplomasia, sambamba na kukuza mawasiliano baina ya nchi mbili hizo.
Miundombinu Kuzuia Mmog’Onyoko Bwawani
WIZARA ya Miundombinu na Mawasiliano, imesema itazuia mmong’onyoko unaosababishwa na maji ya bahari katika eneo la hoteli ya Bwawani hadi Msikiti mabuluu.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Issa Ussi Gavu, alisema hayo barazani jana alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbarouk Mussa Mtando (Mkwajuni) aliyetaka kujua lini ukarabati wa njia hiyo utafanyiwa marekebisho ili kuepuka mmong’onyoko katika eneo hilo.
Gavu, alisema Wizara yake itarekebisha miundo mbinu hiyo mara baada ya hatua za tahadhari za kuzuia mmong’onyoko huo na taasisi nyengine zitakapokamilika.
Serikali Yasaka Mfanyabiashara Kiwanja cha Ndege Pemba
WIZARA ya Miundombinu na Mawasiliano imesema inatafuta mfanyabiashara mwengine kwa ajili ya kuendeleza biashara katika kiwanja cha ndege Pemba.
Akiuliza suali la nyongeza katika kikao cha baraza la Wawakilishi, Hija Hassan Hija, (Kiwani), alietaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuendeleza sehemu ya duka la vinywaji baridi vilivyopo uwanja wa ndege Pemba.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Issa Gavu, alisema mmiliki wa duka la vinywaji baridi katioka eneo hilo ni Kampuni ya Pemba Aviation Ltd, ambayo kwa sasa imekodishwa zaidi ya miaka 10 sasa.
Alisema Serikali ina mpango wa kuendeleza duka hilo lakini kwa sasa kiwango cha malipo ambayo ni shilingi zaidi ya 200,000 kwa mwaka kiwango ambacho ni kidogo sana.
Hata hivyo, Gavu alisema Serikali ina mpango wa kukiimarisha kiwanja cha ndege Pemba na kuwa cha kisasa kwa ufanisi na huduma nzuri.
No comments:
Post a Comment