Habari za Punde

Mwananchi Anayo Haki ya Kumuuliza Kitambulisho Mwandishi --Mkurugenzi Maelezo.

Na Maelezo Pemba.

Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kuhakikisha kuwa kila mmoja wao anakitambulisho cha ruhusa yakuandika habari Zanzibar kichotolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar kama sheria inavyowataka.

Akizunngumza na Waandishi wa Vyombo mbali mbali vya Habari vya Serikali na Binafsi katika kikao kilichofanyika leo katika ukumbi wa Ofisi ya Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Chake Chake Pemba, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Yussuf Omar Chunda amesema kuwa kitambulisho hicho ni kwa ajili ya ruhusa yakuandika habari nchini na kwa maslahi na faida ya mwandishi mwenyewe.


Amesema kuwa na Kitambulisho hicho kunamsaidia mwandishi wa Habari kupata habari kwa njia ya urahisi na kutoweza kubughudhiwa na mtu yoyote yule katika kazi yake.

Chunda amesema kuwa Kiongozi yoyote yule anayo haki yakumdai mwandishi wa Habari Kitambulisho cha ruhusa yakuandika habari Zanzibar kabla yakumpatia habari anayoitaka,hivyo kutokuwa nacho kitambulisho hicho kwa muandishi wa Habari ni
kukosa haki yakupata habari na wahusika wasije kulaumiwa ikiwa habari hizo hawajazitowa.

Aidha amewaomba waandishi wote wa habari waliopo Zanzibar wa vyombo mbalimbali vya Serikali na Binafsi kuhakikisha kuwa wanavitambulisho vya ruhusa vya kuandika habari nchini ili kuondokana na kutopata habari kwani vitambulisho hivyo vipo kisheria kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya magazeti

Mapema Mkurugenzi huyo wa idara ya habari Maelezo Zanzibar Yussuf Omar Chunda amewapongeza Waandishi wa Habari wote wa Zanzibar ,Unguja na Pemba kwa kazi nzuri walioifanya kwa kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa zao la Karafuu.

Amesema kuwa bila ya waandishi kuandika habari mbali mbali zihusianazo na zao hilo basi kazi ingekuwa nzito kidogo lakini juhudi zao ndio zilizosaidia kupunguka kwa Magendo ya karafuu kutokana na Wananchi kuelimika juu ya umuhimu wa zao hilo.

Chunda amewaomba waandhishi kuzidi kutowa ushirikiano wao katika msimu ujao wa uchumaji wa zao la karafuu ili kuhakikisha kuwa mafanikio zaidi yanaendelea kupatikana.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO PEMBA

19/4/2012

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.