Habari za Punde

Selem Rangers Yanusurika Kushuka Daraja

Na Haji Nassor, Pemba

TIMU ya Selem Rangers ya Wete, imejihakikishia kubakia kwenye ligi daraja la kwanza taifa msimu ujao, baada ya kuibamiza Mila kwa kipigo cha magoli 4-2 kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa Gombani.

Selem ilianza kuhesabu mabao yake katika dakika ya 40 kwa goli safi lililonasishwa nyavuni na Sheha Ali, akiunganisha pasi ya Said Suleiman, huku Ali Bakar akifunga mabao mawili mnamo dakika ya 47, na 55 mtawalia.


Licha ya jitihada za Mila kusaka magoli, zilififia katika dakika ya 70 baada ya Ali Bakar tena kuifungia timu yake goli la nne.

Hata hivyo Mila ambayo haina wasiwasi wa kushuka daraja ikiwa na pointi 38, ilijipatia mabao ya kujifariji yaliyofungwa na Abdulrahaman Ali mnamo dakika ya 79, na Khamis Salim aliyezifumania nyavu kwenye dakika ya 81.

Selem Rangers, imejikusanyia pointi 23, na kujihakikisha kubaki katika ligi hiyo, ambapo Mila iliyofikisha pointi 38 ikishika nafasi ya nne.

Wakati huo huo, ngarambe za ligi daraja la pili hatua ya nane bora Wilaya ya Mkoani zimeanza kwenye uwanja wa Mkanyageni, kwa timu ya Danger Boys kuiramba Cossovo ya Wambaa magoli 4-1.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.