Habari za Punde

Wasanii Zanzibar Wamlilia Kanumba

Na Aboud Mahmoud

WASANII wa filamu na maigizo pamoja na wanamuziki wa Zanzibar, wameeleza kuwa kifo cha mcheza filamu maarufu Steven Charles Kanumba, kimeinyima tasnia hiyo mtu muhimu katika kuitangaza Tanzania kisanii.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tafauti kufuatia kifo cha ghafla cha msanii huyo kilichotokea usiku wa kuamkia juzi, walisema Kanumba alikuwa kioo na mfano wa kuigwa kwa namna alivyomudu kutawala jukwaa la filamu na kuling'arisha jina la Tanzania nje ya mipaka yake.


Mmoja wa wasanii waliotoa maoni yao, ni Sabrina Gasper ambaye ametamba katika filamu ya 'Deep Secret' iliyoigizwa Zanzibar, amesema msiba huo ni pigo kubwa kwa wasanii wote.

"Kwa jinsi marehemu Kanumba alivyojitoa kuiletea maendeleo ya filamu nchi yake, na tabia ya kutokuwa mchoyo katika kuwasaidia wasanii wanaoinukia, ni wazi tasnia hiyo imeondokewa na muhimili muhimu", alisema Gasper kwa huzuni kubwa.

Aidha alisema itakuwa vigumu kupata msanii wa mfano wake katika kipindi kifupi, kutokana na kipaji cha hali ya juu alichokuwa nacho marehemu, ambacho aliweza kukitumia kikamilifu na kuteka nyoyo za mashabiki wengi nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Mwanakheri Mussa maarufu Bi Mwana, muigizaji na muimbaji wa kikundi cha Culture Musical Club, amemuelezea Kanumba kuwa jinsi alivyokubalika, wapenzi wake watakosa uhondo waliouzoea kutokana na filamu mpya ambazo pengine msanii huyo angetengeneza au kuigiza.

"Marehemu Kanumba hakuwa muigizaji tu, bali pia alikuwa na kipaji cha muziki kwani tulimshuhudia katika baadhi ya filamu zake akiigiza kama mwanamuziki, hali iliyomfanya apendwe na wengi", aliongeza Bi Mwana.

Naye msanii mkongwe Zanzibar Chimbeni Kheir 'Mashaka', akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dar es Salaam alikokwenda kwa sherehe za Pasaka, amesema msiba huo sio wa Watanzania peke yao, bali ni wa Afrika nzima, kwa kuwa kazi zake zilikuwa zinakubalika kwa mataifa yote ya Afrika kutokana uzuri wake na namna zinavyoelimisha.

"Hakika Mungu amemjaalia kipaji kijana huyu ambacho kimeifanya Afrika nzima imuangalie yeye na Tanzania kwa ujumla", alieleza gwiji huyo wa maigizo.

Kifo hicho kimewagusa pia wasanii wa muziki, ambapo Mudathir Masoud wa kundi la Offside Trick, alisifu mchango wa msanii huyo katika kuitangaza Tanzania, hadi kushirikiana na wasanii wengine wa nje wakiwemo wale wa Nigeria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.