Habari za Punde

TBS Yawafunda Wafanyabiashara

Na Fatuma Kitima, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeanza kuelimisha wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nchi mbalimbali kuanza mpango wa ukaguzi wa bidhaa katika nchi zinakotoka kabla hazijafikishwa nchini Tanzania (PVoc).

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa semina kuhusu mpango huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania, Charles Ekelege alisema kuwa lengo la kufanya semina hiyo ni kulinda soko la Tanzania dhidi ya bidhaa duni na bandia zinazoingizwa kutoka nchi mbalimbali.

Ekelege alisema chini ya mpango huo shehena za bidhaa zilizoagizwa nje ya nchi hukaguliwa na huchukuliwa sampuli na kupimwa kasha kuthibitisha ubora kama zinafaa kuingia nchini.

“Mfumo huu wa udhibiti umefanikiwa kupunguza kiasi cha bidhaa duni zinazoingizwa nchini”, alisema Ekelege.

Hata hivyo alisema kuwa hawakufanikiwa kwa asilimia 100 kuilinda nchi na bidhaa duni hivyo hawana budi kuchukua hatua za ziada ili kulinda nchi isiwe jalala labidhaa zisizofaa kwa matumizi.

Alisema bidhaa duni huathiri uchumi wa Taifa kwa namna mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuikosesha serikali mapato pamoja na kupunguza ajira za wananchi kwa sababu ya kukosesha viwanda ya kukua.

Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora Shirika la Viwango Tanzania, Kezia Mbwambo alisema kuwa wafanyabiashara wakielimishwa kuhusu mpango huo kutawasaidia kupunguza hasara.

“Awali kulikuwa na njia ya kudhibiti bidhaa mbovu kwa kuchoma moto ambapo tumeona wafanya biashara wanaathirika baadhi yao wanakuwa wamekopa benki hivyo wanatakiwa kulipa mkopo huo”, alisema Mbwambo.

Hata hivyo alisema kuwa mfumo huo kuteketeza bidhaa duni hawataendelea nao kwa kuwa unaharibu mazingira pamoja na kumpa hasara mfanyabiashara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.