Habari za Punde

Wafanyakazi Bandarini Wafanya Mgomo Baridi

Uongozi kuwalipa mishahara mipya, malimbikizo mwezi huu

Na Hafsa Golo

WAFANYAKAZI wa shirika la Bandari kitengo cha upakizi na upakuaji wa mizigo katika gati ya Malindi, wameingia kwenye mgomo baridi wakishindikiza kuongezewa mshahara na posho zinazolingana na majukumu yao ya kazi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa mgomo huo baridi unaotekelezwa na wafanyakazi umesababisha meli zilizotarajiwa kushusha na kupatia mizigo katika gati hiyo, zimeamua kuondoka na kwenda kufunga gati katika bandari za Tanga na Dar es Salaam.

Meli hizo zimelazimika kuondoka baada ya kuwepo baharini kwa muda wa siku kadhaa zikisubiri kupakia na kupakuliwa mizigo iliyokuja, ambapo kazi hiyo imekuwa ikifanyika taratibu mno kutokana na mgomo huo baridi.

Kwa kawaida kitengo hicho kilikuwa kikishusha kontena 30 kwa muda wa saa moja kabla ya kuingia kwenye mgomo baridi, ambapo hivi sasa mgomo huo ukiendelea wanashusha kontena tano kwa shifti moja inayodumu kwa masaa manane.

Wakizungumza na Zanzibar Leo, kwa sharti la kutotajwa majina yao, wafanyakazi hao walithibitisha kuwepo kwa mgomo huo, huku kilio chao kikubwa kikiwa ni kuongezewa mshahara pamoja na posho.

Mmoja kati ya wafanyakazi alisema wanachojiuliza ni kwanini shirika hilo lishindwe kuwaongezea mshahara katika kitengo chao huku ikizingatiwa kuwa katika idara nyengine za shirika hilo wafanyakazi wameongezewa mshahara na maposho.

“Hii inaonesha dharau, sisi ndio waingizaji wakubwa wa mapato ya shirika, lakini hatuna thamani yoyote pamoja na kazi ngumu tunayoifanya kila siku”…

“Hatuna thamani baada ya machofu ya kila siku tunayoyapata na tumekuwa tukinyimwa haki zetu hapa hatupewi pesa za matibabu, pesa za likizo hamna, kikubwa zaidi hata mishahara wameshindwa kutupandishi kama walivyowapandishia wenzetu”, alisema.

“Hii ni hatari serikali lazima iwadhibiti hawa mabosi wetu ambao wamekuwa hawajali maslahi ya wafanyakazi wa chini, wapo wengine wanafanya shirika hili kama milki yao”, alisema mmoja kati ya wafanyakazi hao.

Walisema wao kama wafanyakazi watarudi kuendelea kazi zao kama kawaida endapo wataongezewa mishahara, posho kupatikana kwa wakati, warejeshewe pesa za matibabu kama aambavyo huduma hizo zimekuwa ikipatikana kwa wafanyakazi wengine ndani ya shirika hilo.

“Sisi ni wazalendo katika nchi hii na tunafanyakazi kwa mapenzi ya nchi yetu, lakini tunawashangaa viongozi wetu hawana utu, hisani na hata hawaoni thamani yetu”, walieleza kwa hisia.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Msanif Haji Mussa, alisema mara baada ya kurejea safarini Pemba, alibaini kudorora kwa kazi katika kitengo hicho na kujaribu kufuatilia tatizo liko wapi.

Akizungumzia juu ya mishahara mipya, Kaimu huyo alisema shirika hilo lilipanga kuilipa tangu mwezi Januari mwaka huu na kwamba hivi sasa italipwa mwishoni mwa mwezi Aprili pamoja na madeni (areas) ya tangu Januari.

Alisema dosari zilizojitokeza katika utolewaji wa mishara hiyo zimesharekebishwa na kwamba ni vyema wafanyakazi hao wakavuta subira.

Alisema katika mishahara mipya zimejumuishwa stahili kadhaa zikiwemo chakula na sabuni hasa ikizingatiwa kuwa ni utaratibu uliokubaliwa na wafanyakazi wenye kuwa mshahra ushanganywe na posho.

Akizungumzia juu huduma za matibabu, Msanif alisema utaratibu huo ni wa hisani unaotolewa na shirika hilo, lakini imebainika kuwa wapo baadhi ya wafanyakazi wanatumia fursa hiyo kupata matibabu kwa watu walio nje ya familia zao.

Aidha pamoja na jitihada hizo zinazochukuliwa na shirika hilo, Kaimu huyo alisema ameunda kamati ya kuchunguza malalamiko ya wafanyakazi hao ambayo inaongozwa na Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji Mohammed Salum Ali, Mhasibu Mkuu na Ofisa wa Idara ya Ukaguzi.

1 comment:

  1. kuna watu wanaona raha kuvimba matumbo kwa kutumia jasho la wenzao wanasahau kesho ni moto mbele ya ALLAH

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.