Habari za Punde

Walimu Waipiga Kufuli ofisi ya Mkurugenzi

Washindikiza awalipe mshahara, mafao yao

Na Jumbe Ismailly, SINGIDA

WALIMU wapya wa skuli mbalimbali za sekondari waliopangiwa kufanyakazi katika halmashauri ya wilaya ya Singida, wamemfungia mlango mkurugenzi mtendaji na wasaidizi wake kwa takribani saa mbili wakishindikiza kulipwa fedha zao.

Walimu hao wapatao 76 walichukua hatua ya kuufunga mlango mkuu wa kuingilia kwenye ofisi za mkurugenzi huyo, ambapo mlango huo ulifungwa kuanzia saa 6:30 hadi saa 8:37 mchana.

Mkurugenzi mtendaji huyo wa Halmashauri hiyo pamoja na wasaidizi wake, walionja adha ya kudaiwa na walimu hao wapya wa sekondari baada ya ya kufungiwa ofisini kwake kwa zaidi ya saa mbili na nusu.

Hata hivyo kutokana na hatua hiyo iliyochukuliwa na walimu hao ndipo katika kipindi cha muda huo jitihada zilifanywa na ofisi ya Mkurugenzi mtendaji za kufungua mlango mkuu wa kuingilia ofisini uliokuwa umefungwa.

Jitihada hizo zilizaa matunda baada ya jeshi la polisi kwa kushirikiana na ofisa usalama wa taifa kufika na kufanikiwa kufungua mlango huo.

Walimu hao wenye wa vyeti, stashahada na shahada kutoka skuli za sekondari mbalimbali za halmashauri hiyo walikuwa wakidai mishahara yao ya mwezi wa pili na wa tatu mwaka huu, ikiwemo madai ya kurudishiwa fedha za nauli walizotumia katika safari za kutoka makwao hadi Singida.

Aidha walimu hao walikuwa wakidai pia warudishiwe fedha walizotumia kulipia gharama za usafirishaji wa mizigo yao kutoka makwao hadi Singida.

Hata hivyo jeshi la polisi walipofika kwenye eneo hilo la tukio kwa ushirikiano wa pamoja na ofisa usalama wa taifa na ofisa elimu wa Mkoa, Yusufu Kipengere walifanikiwa kuwashawishi walimu hao kuacha jaziba na kukubali wafanye kikao cha pamoja ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.

Katika kikao hicho walimu hao walielezwa kwamba siyo kusudi la ofisi ya Mkurugenzi huyo kuchelewesha kuwalipa walimu hao ikiwemo mishahara, bali tatizo liko nje ya ofisi hiyo.

Mweka hazina wa Halmashaurin hiyo, Bertha Mugwe aliadai kuwa pamoja na hazina kuwatengea shilingi milioni 54, lakini hadi sasa fedha hizo hazijapokelewa katika ofisi ya halmashauri.

Akizungumzia kuhusu kurejeshewa nauli zao, mweka hazina huyo alisema kuwa mara tu watakapokuwa wamepokea fedha na kuhakiki uhalali wake, hawatasita kuwarejeshea madai yao hayo.

Kwa upende wake afisa elimu wa Mkoa wa Singida, Kipengere aliwataka walimu hao kuwa watulivu wakati huu halmashauri ikiendelea kufanya taratibu za kumaliza matatizo yao.

Akizungumza kwa niaba ya walimu wenzake, mwalimu George Wambura alisema pamoja na tatizo la madai yao lakini pia huduma wanazopata kutoka ofisi ya Mkurugenzi huyo siyo za kuridhisha na ndizo zinazowakatisha tamaa kufanya kazi katika halmashauri hiyo.

Hata hivyo walimu hao walikubali kwamba wakati taratibu za kulipwa madeni ya mishahara yao na nauli isipokuwa gharama za usafiri wa mizigo zikiendelea, wataendelea kuchapa kazi ila taratibu hizo zisiwe za muda mrefu.

Hata hivyo walimu hao kila mmoja alilazimika kupozwa kwa kulipwa shilingi 150,000/= kama sehemu ya madai yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.