Habari za Punde

Fedha za Jimbo zitumike vizuri- Thuwaiba



Na Aboud Mahmoud
WAJUMBE wa kamati ya maendeleo ya Jimbo la Fuoni wametakiwa kuwa waadilifu katika kuhakikisha fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya Jimbo zinatumika ipasavyo.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo hilo, Thuwaiba Edington Kisasi, wakati alipokuwa akiizindua kamati hiyo huko katika skuli ya Kijitoupele.

Mwenyekiti huyo, alisema kuwa ipo haja kwa wanakamati hao kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatumika kwa uadilifu mkubwa ili sifa zitakazopatikana kupitia miradi hiyo itakayoanzishwa iende kwa wote.

Aidha aliwataka wajumbe hao kuhakikisha kwamba miradi watakayoanza nayo kwanza wahakikishe kuwa inaanza na miradi ya kijamii ambayo itaweza kuwaletea maendeleo wananchi wote wa Jimbo la Fuoni.

“Nasisitiza kuwa hii kamati sio ya chama bali ni ya Jimbo zima la Fuoni,hivyo nakuombeni kuwa kamati ilete mafanikio ya jimbo na pia wanakamati wenzangu naomba kuhakikisha kwamba miradi tutakayoianza iwe ya kijamii ili wananchi wote waweze kunufaika nayo,”alisema.

Aidha Mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa matumaini makubwa aliyonayo kuwa, anaamini kuwa miongoni mwa wengi watasaidia kusukuma maendeleo ya Jimbo la Fuoni.

Hivyo, Thuwaiba aliishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuona umuhimu wa Wawalikilishi wanastahiki kupewa mfuko wa maendeleo Majimboni mwao.

“Natoa shukurani za dhati kwa Serikali kwa kuona umuhimu wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia majimboni kuwa wanastahiki kupewa mfuko wa maendeleo majimbo mwao,”alifahamisha.

Akipokea fedha hizo shilingi milioni kumi kwa ajili ya Jimbo la Fuoni, Katibu wa Kamati hiyo Abdallah Mwinyi Hassan,amemuahidi Mwenyekiti huyo kuzilinda na kuzitunza fedha hizo kwa kuzitumia ipasavyo.

Alisema kuwa fedha hizo alizozipokea kwanza wataziazia kwa kuanzisha miradi ya maendeleo ya kijamii ili iweze kupata mafanikio kwa wananchi wote wa jimbo hilo.

Kamati hiyo yenye wajumbe tisa ambapo Mwenyekiti wa kamati hiyo ni yeye mwenyewe Mwakilishi wa Jimbo hilo,amekabidhi jumla ya shilingi milioni kumi ili ziweze kutumika kwa ajili ya miradi mbali mbali ya Jimbo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.