Habari za Punde

Viongozi wa dini watakiwa kuwaelimisha waumini wao kuhusu sensa

Na Mwanajuma Mmanga
VIONGOZI wa Dini mbalimbali wametakiwa kuwaelimisha waumini wao umuhimu wa Sensa ya watu na makaazi, wanapokuwa katika mahubiri kwa lengo la kurahisisha zoezi hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi Unguja, Hassan Mussa Takrima, alisema hayo huko ofisini kwake, Mombasa nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, wakati alipokuwa akizungumza na viongozi
wa dini.

Alisema viongozi hao wananafasi kubwa ya kuhakikisha waumini wao na jamii kwa ujumla wanakuwa na uwelewa wa kutosha wakati wa sensa unapowadia.

Alifahamisha kuwa Serikali inafanya sensa ili kupata mipango endelevu ya kiuchumi hivyo, ni muhimu kwa jamii kushiriki kwa lengo la kuiwezesha serikali kufahamu mahitaji ya wananchi wake.

Takrima, alitoa mfano kwa watu wenye ulemavu hasa kwa viziwi kupata mkalimani kwa ajili ya kujua mambo mbalimbali hasa wakati huu wa kuelekea kwenye sensa.

“Matukio mengi yamekuwa yakijionesha walemavu hususan viziwi wamekuwa wakishindwa kufikiwa kutokana na watendaji kutokuwa na taaluma ya kuwasiliana nao”, alisema.

Mkuu huyo wa Wilaya, alitoa wito kwa ofisi ya mtakwimu mkuu wa serikali kuhakikisha kuwa anachagua watendaji wenye taaluma ya kuwasiliana na watu wa aina mbali mbali katika zoezi la sensa ya watu na makaazi litakapofika.

Nae Kadhi wa Wilaya ya Magharibi Shehe Mussa Hassan Mwinyi akielezea zaidi kuhusiana na imani za dini zao kuhusiana na sensa alisema watahakikisha taaluma walioipata wanafikisha kwa waumini wao na jamii kwa ujumla kwani sensa ni muhimu inamgusa kila mtu.

Pia mchungaji wa Kanisa la Mbweni, Padri Josseph Marunja, aliwaomba kuandaliwe mazingira bora kwa walemavu ili nao waweze kushiriki na kuitumia haki yao ya kidemokrasia ipasavyo.

Sensa ya watu na makaazi hufanyika kila baada ya miaka 10 ambapo inatarajiwa kufanyika siku ya Jumapili ya Agosti 26 Agosti, mwaka huu.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.