Vyama vya ushirika vyatakiwa kujiunga na bima ya majanga
Na Kauthar Abdalla
VYAMA vya ushirika nchini, vimetakiwa kujiunga na bima ya majanga na mikopo ili kuweza kuendeleza na kukuza vyama vyao, kwa lengo la kufanya shughuli zao kwa uhakika.
Mratibu wa mafunzo kutoka Idara ya Ushirika, Faiza Amran, aliyasema hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya uanzishwaji, uendeshaji na usimamizi wa Saccos Bank katika ukumbi wa elimu mbadala Rahaleo Mjini Zanzibar.
Alisema endapo vyama vya ushirika vitajiunga na bima ya mikopo itaweza kuwasaidia wanavikundi wakati wanapopatwa na matatizo katika maeneo yao ya kazi.
Afisa huyo, alifahamisha kuwa, kujiunga na Bima kwa vyama hivyo kutaweza kusaidia kubadilika katika hatua moja kwenda nyengine ikiwa ni pamoja na kujihakikisha shughuli zao za kila siku hasa katika kujiletea maendeleo endelevu kwa wanachama na jamii kwa ujumla.
Nae,Naibu Katibu Wizara ya Kazi,uwezeshaji,Wananchi,Kiuchumi na Ushirika Ali Khamis Juma, alisema umefika wakati sasa kwa vyama vya ushirika kuwa imara ili viweze kupata fursa za ajira za wananchama kupitia ndani ya vyama hivyo na sehemu nyengine pamoja na kuzifanyia kazi ipasavyo.
Aidha alifahamisha kuwa wanachama wawe tayari kupokea na kudai taaluma kutoka katika Wizara hiyo, kwa kuwa wao ndio wanaowajibika kutoa taaluma inayohusiana na shughuli zao.
“Ni vyema kwa vyama vya ushirika kutoa huduma za ziada kwa kila SACCOS ikiwemo huduma za mtandao ili kwa lengo la kujiimarisha zaidi sambamba na kupata taaluma inayohusiana na kazi zao”, alisema.
Hata hivyo, alifafanua kwamba kujiunga katika vikundi vya ushirika ni sehemu moja ya kujikomboa na hali ngumu ya maisha kwani ikitumiwa vizuri fursa hiyo itazidisha maendeleo kwa Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Ushirika, Hamis daudi Simba amevitaka vyama vya ushirika viwe vya ufanisi na wanachama wanapohitaji mikopo wapewe kwa wakati unaostahiki.
Mkurugenzi alisema Serikali imedhamiria kwa dhati kuwa na vyama vya ushirika ili kuwasaidia wanaushirika mbali mbali nchini na kuwa na vyama vichache ambavyo vitakuwa na mwelekeo mzuri.
No comments:
Post a Comment