YWCA yaomba nguvu za Mama Salma Kikwete
Na Thompson Mpanji, MBEYA
CHAMA cha Vijana,Wanawake wa Kikristo Tanzania (YWCA) kimetoa wito kwa Mama Salma Kikwete na Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda, kuonesha mfano wa kuwasaidia na kuwawezesha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa YWCA tawi la Mbeya, Tabitha Bughali muda mfupi baada ya kukamilika kwa zoezi la kuwapima afya watoto yatima na wanaoishi katika magumu zaidi ya 100 wanaolelewa na YWCA,msaada uliotolewa na hospitali ya Aga Khan Mbeya, alisema chama hicho hakina vyanzo vya mapato zaidi ya kutegemea michango kutoka kwa wanachama
.
Tabitha alisema YWCA Mbeya inapokea kila kukicha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi lakini kutokana na maisha duni ya akina mama wajane na vikongwe wanaojitolea kuleta watoto hao hali imekuwa ngumu kwao hivyo wanahitaji msaada kutoka kwa wazazi hao wa kitaifa ili waoneshe njia kwa jamii ya watanzania.
“Wanachama wa YWCA Mbeya wengi wetu ni wajane na vikongwe tumekuwa tukijitoa kutoka mifukoni mwetu na pesa hazitoshi…tunawashukuru wasamaria wema kujitolea kuleta misaada mbalimbali lakini tunaona upo umuhimu wa kuwakaribisha wazazi wetu hawa wa Taifa ili jamii iweze kutambua mahitaji na kujitoa”, alisema.
Katibu huyo alisema kuwa hadi sasa YWCA Mbeya ina zaidi ya watoto yatima 100 ambao baadhi yao wameshasomeshwa hadi kufikia kiwango cha vyuo vya ufundi stadi na vyuo vikuu na wengine wakiwa katika elimu ya sekondari na Msingi.
Jopo la madaktari, wauguzi na wataalamu wa maabara liliongozwa na uongozi wa hospitali ya Aga Khan ambao ni Clement Kezimana, Mwenyekiti wa bodi Sultan Thawer,Neelam Babul na Mganga mkuu Dk.Herman Kimanago.
Jopo hilo limesema licha ya kujitolea kutoa huduma ya vipimo kwa watoto hao lakini wameahidi kuendelea kuwatibu bure watoto watakaogundulika kuwa na maradhi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment