Na Salum Vuai, MAELEZO
WAHITIMU wa Chuo cha Afya kilichoko Mbweni, wametakiwa kufanyakazi
kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao pindipo wanapoajiriwa, na kwamba lazima
nyoyo zao ziwe nyeupe kwa wagonjwa kama zilizvyo
sare zao.
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Malik Abdallah Juma
alieleza hayo akiwamukilisha waziri wa wizara hiyo kwenye mahafali ya 19 ya Chuo
hicho yaliyofanyika katika viwanja vya chuo hicho huko Mbweni.
Wahitimu kwenye mahafali hayo wa kati ya miaka miwili na
minne katika fani za uuguzi/ukunga, afya ya akili na wakunga wa vijijini ambapo
walitunukiwa vyeti na stashahada.
Dk. Malik alisema haitakuwa busara kuwaona wahitimu wao
wakinga'ra kwa sare nyeupe wakifurahia kumaliza mafunzo, au wanapoajiriwa,
lakini wakashindwa kufuata maadili yanayoongoza taaluma zao.
Aidha alieleza wananchi wamekuwa wakiwalalamikia kutokana
na tabia mbaya walizonazo baadhi ya wauguzi, kwa kukiuka maadili, na kuwatolea
ujeuri, ujuvi wagonjwa wanaowahudumia, hivyo kuipaka matope fani hiyo.
"Mimi nakerwa sana
na kauli iliyozoeleka kwamba mtu akitaka kushuhudia ujeuri 'first class'
(daraja la kwanza), basi aende hospitali ya Mnazimmoja. Nafahamu wauguzi wengi
wanatelekeza vyema majukumu yao,
hawa wachache wenye tabia mbaya wasipewe nafasi kutuharibia", alisema
Mkurugenzi huyo.
Aliwataka wahitimu watakaobahatika kuajiriwa katika
hospitali kuu ya Mnazimmoja na nyengine nchini, kuleta mapinduzi kwa kuwa
waadilifu na kutoiga tabia mbaya za wauguzi wachache wanaotajwa kuwa ni
wakorofi.
Mkurugenzi huyo alisisitiza kwamba viapo walivyotoa
wahitimu hao visiwe kauli za midomoni bali vitoke nyoyoni, ili kuipa taaluma yao hadhi na heshima
inayostahili mbele ya jamii na pia kumridhisha Mwenyezi Mungu.
Kwa upande mwengine, aliwashauri kuwa kuhitimu kwao chuoni
hapo kusiwe mwisho na kujiona wamemaliza elimu, bali wajiendeleze kwani
kumekuwa na mabadiliko ya kisayansi na kila siku kuna kitu kipya cha kujifunza.
Aliahidi kuwa, serikali kupitia wizara ya Afya kwa
kushirikiana na Baraza la Chuo hicho, watachukua juhudi kuzipatia ufumbuzi
changamoto zinazokikabili chuo na wanafunzi ili kuwajengea mazingira mazuri ya
kufanya kazi na kushughulikia masomo yao.
Mapema, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Rukia Rajab, alisema
wahitimu hao ni mchango wa chuo kwa serikali, na hivyo kuiomba ihakikishe
inawatumia ipasavyo kwa kuwaajiri kwenye hospitali na vituo mbalimbali vya afya
Unguja na Pemba.
Alifahamisha kuwa, mwaka huu utakuwa wa mwisho kwa Chuo
hicho kutoa taaluma kwa miaka minne, na kitaanza kufuata mtaala wa miaka
mitatu, mpango ambao unatambuliwa na umeridhiwa na nchi za Afrika Mashariki.
Aliishukuru serikali ya Zanzibar
kwa kuendelea kukisaidia chuo, sambamba na ile ya Oman ambayo inaendelea kukiimarisha
kwa mambo mbalimbali baada ya kufadhili ujenzi wake.
Alitaja miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana, ni pamoja na
ukarabati wa ukumbi wa mikutano, kufungua tovuti, kukamilika kwa ujenzi wa
dakhalia na nyumba ya walimu kutoka Norway, walimu wanne kwa msaada wa Benki ya
Maendeleo Afrika (ADB).
Katika risala yao wahitimu, walisema ulinzi chuoni hapo
hautoshi kulingana na ukubwa wa eneo hilo, ukuaji wa ongezeko la wanafunzi
kutoka ndani na nje ya Zanzibar, na kutaka nguvu zaidi ziongezwe katika ili
ujenzi wa ukuta unaozunguka chuo hicho umalizike kwa haraka na kuwahakikishia
usalama wao.
Jumla ya wahitimu 173 walikabidhiwa vyeti na stashahada
zao, ambapo 66 wanakwenda kuwa wauguzi/ wakunga, 33 wamesomea fani ya afya ya
akili na 74 ni wakunga wa vijijini.
No comments:
Post a Comment