Na Mwantanga Ame
WAKATI Tume ya Uchaguzi Zanzibar, ikiwa imepuliza kipenga
cha kuanza kwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu, Vyama vya Siasa Zanzibar,
vimeanza kujitapa kushinda uchaguzi huo huku Chama Cha CCM kikisema hakitakuwa
tayari kulitoa jimbo hilo
mikononi mwake.
CCM imeeleza hakitakuwa tayari kuliachia Jimbo hilo kuingia katika mikono ya upinzani na kinakusudia
kulinyakuwa tena Jimbo hilo
ili kuona linarudi katika mikono ya CCM.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu unafanyika baada ya
aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo
Mohammed Ali Mtondoo, kupitia tiketi ya CCM kufariki dunia mapema mwaka huu
baada ya kuuguwa maradhi ya kupooza mwili.
Kutokana na kifo hicho Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),
tayari imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo Septemba 16, mwaka huu ambapo
wananchi wa Jimbo hilo
watapiga kura.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, akizungumza na Zanzibar Leo, jana Mjini
Zanzibar alisema uchaguzi huo utakuwa ni wa aina yake kwani CCM itahakikisha
jimbo hilo
linabakia katika mikono yake.
Alisema tayari hivi sasa Chama hicho kimeanza kufanya
maandalizi ya kushinda uchaguzi huo, ikiwa pamoja na kuandaa mazingira bora
kupata wagombea ambao wataingia katika kinyang’anyiro hicho kitapoanza.
Akifafanua kauli hiyo, Naibu huyo alisema mazingira hayo
yatakuwa mapya ndani ya Chama cha Mapinduzi, kwa lengo la kuepusha kutokea kwa
vurugu, chuki na hasama katika upatikanaji wa mgombea katika kura za maoni za
ndani ya Chama.
Akifafanua zaidi alisema utaratibu wanaokusudia kuutumia ni
majina ya wagombea yatayojitokeza kuomba nafasi hiyo kabla ya kuwasilishwa kwa
wananchi kupigiwa kura za maoni, yatafikishwa katika vikao vya Mkutano Mkuu wa
Majimbo ambao utawashirikisha mabalozi wa matawi na watapiga kura kutoa majina
matatu.
Alisema baada ya kutoa majina hayo matatu Mkutano huo
utayashusha kwa wanachama kuweza kuyapigia kura ya maoni ili kupata chagua lao
badala ya mfumo wa zamani wa majina hayo kuwasilishwa yote kwa wananchi.
Aidha, alisema kwa vile jimbo hilo lilikuwa chini ya CCM, hawatakubali
kuona linawatoka mikononi mwao na hivi sasa tayari wameanza maandalizi ya
kushinda.
Alisema huo ni mmoja wa mkakati uliouweka Chama cha
Mapinduzi, kuona majimbo yote yaliokuwa ngome ya CCM na yaliochukuliwa na upinzani yanarudi mikononi
mwa Chama hicho.
Hata hivyo, alisema Chama hicho kitahakikisha mchakato
mzima wa uchaguzi huo unaendeshwa katika mazingira bora kwa kufanya kampeni za
kistaarabu hadi kupatikana mshindi.
Kuhusu suala la kupata mgombea alisema tayari hivi sasa
kuna wanachama wengi wa CCM katika Jimbo hilo
wameanza kuonesha nia ya kutaka kuwania nafasi hiyo.
Nae Katibu wa Chama cha TADEA Zanzibar,
Juma Ali Khatib, akizungumzia juu ya suala hilo alisema hawana sababu ya kutoshiriki
uchaguzi huo kwani tayari kuna wanachama wengi wanaotaka kuwania nafasi hiyo na
kushinda.
Alisema ndani ya Chama hicho tayari kuna wanachama zaidi ya
watano wakiwemo wanawake wawili ambao wameonesha nia kutaka kuwania nafasi
hiyo.
Alisema hivi sasa bado hakuna vikao vilivyokaa kwa ajili ya
kutoa ratiba ya Chama hicho katika namna ya kupata mgombea huyo.
Hata hivyo, Katibu huyo, alisema Chama hicho kinajiandaa
kufanya vikao vya chama kuweza kutoa mgombea huyo ndani ya mwezi ujao.
Mkurugenzi wa Sera wa Chama cha Wakulima na Wafanyabishara Zanzibar (AFP), Rashid Yussuf Mchenga, akizungumzia
msimamo wa Chama hicho juu ya hilo,
alisema tayari Chama chao kimeshafanya
uteuzi wa Mgombea ataewania nafasi hiyo na wanahakikisha kuwa atashinda.
Alisema aliyeteuliwa kuwania nafasi hiyo kwa Chama hicho ni
Mussa Ali Mussa, na hivi sasa wameanza maandalizi ya kukamilisha taratibu za
Tume ya Uchaguzi.
Upande wa Chama cha CUF kupitia msemaji wake Mkurugenzi
Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma, Salum Bimani, akizungumza na Zanzibar
Leo, alisema chama chao kitahakikisha uchaguzi huo unakuwa huru na haki na
chama chao kitaibuka na ushindi.
Alisema Chama chao tayari hivi sasa kimeshaanza mchakato wa
kupata mgombea wa kuwania kiti hicho na kitahakikisha kinaenda katika uchaguzi
huo kwa kushirikiana na vyama vyengine katika hatua zote.
Hata hivyo, Bimani alisema watachohakikisha wanakizingatia
katika uchaguzi huo ni kuwahimiza wanachama wao kushiriki uchaguzi huo kwa
amani.
Kwa mujibu wa ratiba ya Chama cha Mapinduzi iliyotolewa na
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye,
imeeleza kuwa kazi ya uchukuaji wa fomu na urejeshaji kwa ajili ya kuomba
nafasi hiyo ya uongozi zinatarajiwa kuaanza Julai 26, 2012 na Julai 30 mwaka
huu na utafanyika mkutano Mkuu wa Jimbo ambao utaweza kupendekeza majina
matatu.
Kampeni ya matawini kwa Chama hicho inatarajiwa kufanyika
Julai 31, mwaka huu na kura ya maoni itafanyika matawini Agosti 5, mwaka huu.
Baada ya kupatikana kwa jina la mgombea kutoka matawini
jina lake litafikishwa
katika Kamati ya siasa ya Wilaya ya Magharibi Unguja Agosti 6, 2012 itakutana
na Kamati ya siasa ya Mkoa huo inatarajiwa kukaa Agosti 7, mwaka huu.
Agosti 9, mwaka huu ratiba hiyo imefahamisha kuwa
kutafanyika kikao cha Sekretarieti ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa
na Agosti 11, 2012, Kamati Maalum ya
halmashauri Kuu ya Taifa, Agosti 13,2012 ni kikao cha Sekreterieti ya
Halmashauri Kuu ya Taifa itakaa na Agosti 15, mwa mwaka huo kamati Kuu ya CCM
itakutana kufanya uteuzi wa mgombea.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar imepanga kazi za uchukuaji na
urejeshai wa fomu zitaanza Agosti 22, 2012 hadi Agosti 30, mwaka huu na uteuzi
wa wagombea utafanyika Agosti 30, mwaka huu huku kampeni zinatarajiwa kuanza
Agosti 31, 2012 hadi Septemba 15, 2012 na uchaguzi utafanyika Septemba 16,
2012.
No comments:
Post a Comment