HATUA ya Serikali kuondoa ada za huduma kwa mama wajawazito baadhi ya wanawake wamepongeza serikali kwa kutangaza kuziondoa gharama hizo kwani itawaondolea usumbufu wananchi kupata huduma hizo.
Wanawake hao walieleza kuwa mpango huo wa serikali ni ukombozi utaowashushia mzigo wa gharama za huduma kwa wajawazito kwa sababu wengi wao walikuwa hawamudu jambo ambalo liliwasababishia kupata matatizo wakati wa kujifungua.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi mmoja wa wanawake hao Samira Kombo, mkaazi wa Bububu Mjini Unguja, alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kuthamini wanawake wajawazito na kuona umuhimu wa kuwaondolea ada za huduma hiyo.
Alisema mpango wa serikali kuondoa ada hiyo umezingatia hali ya umasikini waliokuwa nao wanawake wengi hasa wanaoishi vijijini na utasaidia kuwapunguzia adha waliyokuwa wakiipata kwani baadhi yao walishindwa kutumia huduma za kulea mimba zao katika vituo vya afya.
Aliongeza kuwa pamoja na serikali kuwaondolea ada hiyo lakini bado anaiomba serikali kuona inakuwa makini katika hilo, ili kuhakikisha wanapewa huduma kwa usahihi pasipo uonevu wowote ikiwa ni pamoja na kuweka ulinzi katika hili.
“Mimi binafsi wakati najifungua wanangu wa kwanza nilifanyiwa uzembe, ambao mpaka sasa mwanangu ni mlemavu na nilitoa ada ya huduma hiyo sasa serikali wasipokuwa makini katika hili watatumiza wengine”,alisema mama huyo.
Naye Mariamu Ramadhani mkaazi wa Rahaleo akizungumzia suala hilo aliipongeza serikali kwa uamuzi huo mzuri na ameomba serikali kuzungumza na kuwashauri madaktari watoe huduma nasio kuwafanyia vitu visivyostahiki wakati huduma hizo zikianza kutolewa bure.
Alisema kuwa anaamini nia ya serikali kuanzisha huduma hizo kutolewa bure serikali inakusudia kutokomeza vifo vya akinamama na itakuwa ndiyo dhamira kuu hata kwa wahudumu watakaowasaidia katika kuwapa huma bora.
Mmoja wa wauguzi katika kituo hicho ambaye hakutaka kutaja jina lake, akizungumzia suala hilo alisema hivi sasa bado ni mapema kwa kituo chao kuzungumzia suala hilo kwa vile bado hawajapata taarifa rasmi kutoka Wizarani inayoelezea muongozo wa kufanya kazi hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania, Asha Bakari Makame, akizungumzia juu ya suala hilo alisema anampongeza Rais wa Zanzibar na Mwekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa hatua yake hiyo kwani ameonesha upendo kwa wanawake wa Zanzibar kuweza kustawisha afya zao.
Alisema kwa muda mrefu wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wamekuwa wakilipigia kelele suala hilo, lakini kutokana na serikali ya awamu ya saba kuwa sikivu imeweza kujali kilio cha wanawake wa Zanzibar.
Alisema jambo la msingi ambalo litahitajika kufanyika hivi sasa, ni kuona watendaji wa Wizara ya Afya kulifanyia kazi vyema suala hilo ili liweze kuwa na manufaa kwa wananchi wa Zanzibar.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti huyo, aliuomba uongozi wa Wizara ya Afya, kujiandaa vyema kulifanyia kazi suala hilo, kwa kutambua uamuzi huo wa Rais utatekelezwa kisheria na watahitajika watendaji kuwa waaminifu ili wasivunje sheria hiyo.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Dimani Mwinyihaji Makame, alisema hatua aliyoichukua Rais kutangaza kuondolewa kwa ada hizo ni ya msingi, kwani itaweza kuwaondolea usumbufu wananchi pamoja na viongozi wa majimbo.
Akitoa mfano alisema hivi sasa baadhi ya wananchi wamkuwa wakishindwa kupata huduma hizo hulazimika kukimbilia kwa Wabunge na wawakilishi wao kutaka kupatiwa fedha msaada wa kujifungulia.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh, Salmin, akizungumzia suala hilo alisema yeye binafsi na wananchi wa Jimbo lake wamelifurahia sana suala hilo na amempongeza Rais kwa uamuzi wake huo.
Alisema suala hilo yeye binafsi alishalizungumza ndani ya kikao cha serikali ya awamu ya sita na kikao kilichopita wiki tatu nyuma ambapo aliiomba serikali kuhakikisha inafuta ada hizo.
“Nimefurahi sana, sana, sana, na mpongeza Rais wetu kuwa msikivu kusikia kilio chetu hili mimi nilishalisemea sana katika ripoti zetu tangu katika kamati za Baraza zilizopita za Ustawi wa Jamii” Alisema Mwakilishi huyo.
Akiendelea alisema inawezekana watendaji wa Wizara ya Afya lisiwapendeze suala hili kutokana na kuwa ni mwanya waliokuwa wakiutumia kupata fedha, lakini bado watapaswa kuuheshimu uamuzi wa Rais.
Alisema kinachohitajika ni kuona viongozi wa Wizara hiyo wanajiandaa kuweka utaratibu bora utaowafanya kila mwananchi kuhudumiwa vyema hasa wakizingatia wanaowapa huduma ni wanawake wenzao.
Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub, akizungumzia juu ya suala hilo alisema hatua ya Dk. Shein, kutangaza kuondoa ada hiyo imewapa faraja wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuweza kusikiliza kilio chao.
Alisema Wajumbe wengi wa Baraza la Wawakilishi, kwa muda mrefu wamekuwa wakilizungumza suala hilo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi ambapo maisha yao yamekuwa yakiwekwa rehani.
Nae Mratibu wa shughuli za Chama Cha Waandishi wa Habari Tanzania TAMWA kanda ya Zanzibar, Mzuri Issa, akizungumzia suala hilo alisema hatua ya serikali kuondoa gharama hizo itawasaidia wanawake wengi kuwa salama katika hali ya kulea mamba zao.
Alisema Wanawake wengi kwa muda sasa wamekuwa waoga wakati wakiwa katika hali yao ya ujauzito kuufikiria kama watajifungua salama kutokanana kukosa gharama hizo na wasaidizi.
Alisema hali inakuwa mbaya zaidi pale inapotokea familia ya mwanaume mwenye wake zaidi ya mmoja ambapo humlazimu kuwahudumia kwa wasiwasi kwa vile hulazimika kuwa na mahitaji makubwa ya kulea mamba hizo hadi wajifungue.
“Tuone mfano ulio hai wa Mama aliyejifungulia nje ya Hospitali ambaye alikataliwa kupewa matibabu na akaachwa kujifungua hapo ati hana fedha na sasa kuondolewa fedha hizo huu ni ukombozi mkubwa” alisema mratibu huyo.
No comments:
Post a Comment