Habari za Punde

Waya Mpya wa Umeme Zanzibar kutandikwa Agosti


Na Rajab Mkasaba, Ikulu


WATENDAJI na Viongozi wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati wameeleza kuwa utengenezaji wa waya wa umeme unaopita chini ya bahari umekamilika na uko njiani kuletwa Zanzibar waya ambao utalifanya tatizo la umeme linalosababishwa na ule uliopo kuwa historia katika kisiwa cha Unguja.

Maelezo hayo yametolewa na watendaji na viongozi hao katika mkutano kati yao na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika muendelezo ya mikutano yake ya kukutaa na watendaji na viongozi wa Mawizara yote ya SMZ katika kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011-2012 pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka 2012-2013.

Mkutano huo umefanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Wizara hiyo ilieleza kuwa utengenezaji wa waya wa baharini wenye kilomita 39.5 umekamilika na hivi sasa uko njia.

Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar Hassan Ali Mbarouk, aliyasema hayo katika kikao hicho na kueleza kuwa ulazaji wa waya huo wa pili wa chini ya bahari kutoka Ras Kiromoni hadi Ras Fumba unatarajiwa kufanywa Agosti mwaka huu.

Alieleza kuwa kazi hizo zote zimegharamiwa na MCC, ambapo kwa upande wa matayarisho tayari ukamilishaji wa uwekaji wa transfoma mbili kubwa zenye uwezo wa 60MVA kila moja tayari umeshafanywa.

Uongozi huo ulieleza kuwa ziara ya utafiti katika eneo la mradi kutoka Ubungo hadi Ras Fumba na Ras Fumba hadi Mtoni umeshakamilika kazi ambayo inatekelezwa na Kampuni ya Kalpataru kutoka India.

Kampuni ya VISCAS CORPORATION ya Japan ndio inayotengeneza waya huo pamoja na kuulaza baharini mara utakapofika, ambapo Kampuni ya SYMBION ya Marekani ikishirikiana na Kampuni ya 

ALSTOM ya Ufaransa ndizo zinazotengeneza vituo vya kupokea umeme.
Uongozi huo ukiongozwa na Waziri wake, Ramadhan Abdalla Shaaban ulieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha umeme katika kisiwa cha Unguja ili kwenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.