Habari za Punde

Seagull Yazimika Nungwi Yapotelea Tanga

Ilikuwa na abiria 300 ikitokea Pemba

Na Asya Hassan

ABIRIA 300 waliokuwemo katika meli ya MV Seagull wakitokea kisiwani Pemba kuelekea Unguja jana, walipatwa na hofu kubwa baada ya meli hiyo kuzimika katika mkondo wa Nungwi na kubururwa na maji hadi Tanga.

Baada ya taarifa hizo Kampuni inayomiliki MV Seagull ilitoa meli yake nyengine SKAGIT ili kwenda kuisaidia meli hiyo katika namna itayoona inafaa.

Lengo la meli hiyo lilikuwa ni kufika na kuifunga meli hiyo ili kuiburura, kwani ingekuwa vigumu kuruhusu abiria kuingia katika meli hiyo kwa vile hali hiyo ingesababisha hatari zaidi kutokana na watu wengi wangetaka kuingia kwa hofu waliyokuwanayo.


Kabla ya meli hiyo kurudi kulipatikana taarifa kwamba mashine ya MV Seagull imewaka huko Tanga, baada ya kufanyiwa matengenezo hivyo kuweza kurudi Unguja yenyewe na abiria iliyokuwanayo wakiwa salama.

Tukio hilo liliripotiwa mapema jana mchana baada ya abiria waliokuwemo ndani ya meli hiyo kuwapigia simu jamaa zao kuwapa taarifa hiyo, hali ambayo ilizua hofu kwa ndugu na jamaa zao hao.

Kutokana na taarifa hizo wananchi kadhaa walijazana katika bandarini kusubiri jamaa zao baada ya kupata taarifa ya kuzimika meli hiyo. 

Wakizungumzia kuharibika huko, wananchi wamesema kuzimika kwa meli hiyo mara kwa mara ikiwemo safarini na abiria, pamoja na nyengine zenye kufanya safari za Unguja na Pemba ni hatari ambayo inaonekana kueleweka lakini hakuna njia zinazoonekana kuchukuliwa kuondosha tatizo hilo.

Baadhi ya wananchi waliokuwa wakisubiri jamaa zao wamesema kwamba kuna haja ya Serikali kununua meli kubwa ya abiria na mizigo kwa ajili ya kusafirisha wananchi Unguja na Pemba, ambapo usafiri wa baharini ni wa lazima.

Aidha walieleza kushangazwa kwao kuruhusiwa meli hiyo kupakia abiria wakati ni hivi karibuni ilizuiliwa kwa kutokamilisha taratibu za kusafirisha abiria ikiwemo ubovu.

Tokea kuzama kwa MV Spice Islanders Septemba mwaka jana, wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakisafiri kwa hofu katika meli zinazotoa huduma hivi sasa ambapo mara kwa mara zimekuwa zikiharibika.

Katika nyakati tafauti na viongozi tafauti wa kitaifa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imekuwa ikieleza kwamba inaendelea na mpango wa kutafuta meli mpya ya kupakia abiria na mizigo ili kuwaondoshea wananchi usumbufu wa usafiri.

2 comments:

  1. KWA KWELI HALI YA USAFIRI SIKU HIZI KWA VISIWA VYA UNGUJA NA PEMBA NI MBAYA SANA.
    NA SIO KAMA SERIKALI HAWALIJUI HILO BALI VIONGOZI NI WABAYA SANA WANAJALI MASLAHI YAO TU KUTAKA KUTOA ROHO ZA WANANCHI WALIOWACHAGUA KWA MASLAHI YAO BINAFSI.MELI MARA NGAPI ZIMESHAZIMIKA NA WATU WANAKAA SI CHINI YA MASAA KADHA BAHARINI KUSUBIRI KUDRA ZA MUNGU TU.
    HIVI HIZI PESA WANAZOZIJENGEA NYUMBA ZA GHOROFA WANAZIPATA WAPI KAMA SIO KUIBA KWA MISHAHARA YAO HAZITOSHI KUFANYIA HAYO.HEBU WAKAE WASEME WAWACHE KUIBA MWAKA MMOJA TU SIRIKALI HAITOWEZA KUNUNUA MELI KWA AJILI YA WANANCHI WAO HALAFU WAENDELEE KUIBA?

    ReplyDelete
  2. Ahsante ndugu yangu kwa kuwa 'objective' kwa mawazo ya namna hii tunaweza kuondoa uwozo wa serikali yetu na kusonga mbele.

    Naamini ungekua mwana UWAMSHO ungesema ni tatizo la muungano!
    Siku moja nlisema hapa, Z'bar tuna matatizo mengi yanayotokana na uzembe lkn. tumeamua kuwa vipofu, mfano juzi tu hapa mamia ya wanafunzi wa form 6 wamefeli, watu kimyaaa!!!

    Kwa staili hii "tutulie, tugangwe maradhi si kitu"

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.