WANACHAMA wa Yanga, jana walichukua uamuzi wa kumng'oa madarakani Mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga baada ya kutimiza zaidi ya watu 500 wa kutia saini ya kumkataa kuendelea kuiongoza timu hiyo.
Wanachama hao walifanya mkutano huo kwenye jengo la klabu hiyo mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo ni tafauti na vikao vyengine vya Yanga ambavyo hufanyika katika ukumbi wa jengo la klabu hiyo, pengine kutokana na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wanachama pamoja na wapenzi wa timu hiyo, mkutano huo ulilazimika kufanyika kwenye uwanja wa nje ya jengo.
Awali kulifanyika zoezi la wanachama wanaompinga Nchunga kutia saini uwanjani hapo ambapo idadi yao ilifikia 556, walioripotiwa kuafiki mpango huo, ambao imeelezwa kuwa umelenga kurejesha heshima na hadhi ya timu hiyo ambayo ni watani wa jadi wa Simba.
Baada ya zoezi hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wazee wa klabu hiyo Ibrahim Akilimali, akitangaza rasmi kumfuta uenyekiti wa timu hiyo, Lyod Nchunga, baada ya kutimiza kolamu ya wanachama 556.
Mbali ya wanachama hao kumvua madraaka Nchunga, pia wajumbe wanane wa kamati ya timu hiyo walijiuzulu nafasi zao hiyo jana.
Mara baada ya Akilimali kutangaza mapinduzi hayo yaliyoendeshwa kikatiba, umati wa wanachama na hata wapenzi wa timu hiyo waliokuwa pembeni kufuatilia mkutano huo, uliripuka kwa furaha na kusikika wakitamka "Nchunga ondoka kazi imekushinda".
Baadhi ya wanachama walikaririwa wakisema kwamba kutokana na hadhi na historia ya timu hiyo, ni lazima kupatikane viongozi wenye mwamko, dira na maarifa ya kimaendeleo, badala ya wababaishaji ambao wametajwa kuendekeza maslahi binafsi.
Hata hivyo, jitihada za gazeti hili kuwasiliana na Nchunga ili aeleza alivyoyapokea mapinduzi hayo, hazikuweza kuzaa matunda kwa siku ya jana.
No comments:
Post a Comment