Habari za Punde

SBL Yajitwisha Tuzo za Wanamichezo Bora.

KAMPUNI ya Bia ya Serengeti imejitolea kubeba udhamini wa tuzo za wanamichezo bora wa Tanzania kwa mwaka 2012 zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).

SBL imetangaza kutoa shilingi milioni 150, kwa ajili ya kugharamia tuzo hizo zitakazotolewa kwa wanamichezo mbalimbali waliofanya vyema mwaka huu kwa michezo tafauti.

Hatua hiyo ilitangazwa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti Teddy Mapunda, alipokuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye klabu ya City Sports Lounge, Dar es Salaam, akiambatana na viongozi wa TASWA.

Mapunda alisema kampuni yake inaona fahari kuendelea kudhamini tuzo za TASWA ikiwa ni mwaka wa tatu mfululizo, ambapo alieleza kuwa, mwaka huu kampuni yake imeongeza udhamini zaidi ili kuziboresha.

Naye Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto akitoa shukurani zake, alisema udhamini huo ni ishara ya namna kampuni hiyo inavyothamini wanamichezo wa Tanzania, ambapo umeongezeka kutoka shilingi milioni 80 za mwaka jana.

Pamoja na kusema kiasi hicho kinatosha, Pinto alisema milango ipo wazi kwa wadhamini wengine kujitokeza kuiunga mkono SBL kwani TASWA ilipanga bajeti ya tuzo hizo kuwa shilingi. milioni 370.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema, kamati maalum ya tuzo hizo, inaendelea na mchakato wake wa kupata wanamichezo hao na kwamba kadiri watakavyokuwa wanapiga hatua watatoa taarifa kwa wanahabari.

Hafla ya kutunuku tuzo hizo, imepangwa kufanyika Juni 14 mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee (VIP) jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.