Habari za Punde

Vijana Makadara Watowa burudani safi kwa Mbunge Mabodi.

MBUNGE wa jimbo la Rahaleo Abdalla Juma Mabodi, amewamwagia pongezi vijana wa shehia ya Makadara kwa jitihada zao za kujijengea umoja na kuibua mambo yanayosaidia kuwaepusha na vitendo viovu.

Mabodi ambaye pia ni Kamanda wa Vijana wa CCM Wilaya ya Mjini, alikuwa akizungumza na vijana hao baada ya pambano la mpira wa miguu kati ya timu ya G. Unit na Polite People lililochezwa kwenye uwanja wa Lumumba.

Mbunge huyo aliwataka vijana hao kuimarisha mshikamano na kuongeza upendo miongoni mwao, ili kubuni njia za kujiletea maendeleo yao na taifa kwa jumla.

Katika mchezo huo, G. Unit iliibuka na ushindi wa mabao 7-6 ambao ulipatikana kwa mikwaju ya penelti, baada ya wanaume hao kuzimaliza dakika 90 wakiwa sare ya bao 1-1.

Kabla kupatikana mshindi, G. Unit ilikuwa ya kwanza kuandika bao lake katika dakika ya 23 ambalo lilifungwa na Khamis Mtumwa, kabla mchezaji Ahmed Kibwengo kuisawazishia Polite People kwenye dakika ya 56.

Kwa ushindi huo, G. Unit ilifanikiwa kunyakua kikombe, kondoo mmoja pamoja na fedha taslimu shilingi 50,000, ambapo Polite People iliramba shilingi 50,000 pekee.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.