HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI
NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO (MB), WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI, KUHUSU MAPENDEKEZO YA
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
______________________
I. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi ya
Upinzani, ninatoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Bajeti ya Nchi ya mwaka wa
fedha 2012/2013 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo la Mwaka
2007.
Mheshimiwa Spika, Natoa pongezi za dhati
kabisa kwa Ndugu William Augustao Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani
Iringa kwa kuteuliwa na Rais kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi. Vile vile
nawapongeza Ndugu Saada Mkuya na Ndugu Janeth Mbene kwa kuteuliwa kwao kuwa
Wabunge na baadaye kuwa Manaibu Mawaziri katika Wizara hii nyeti sana. Ninawapa pole pia maana Wizara ya Fedha sio
Wizara lelemama. Kambi ya Upinzani itaendelea kuisimamia Wizara hii kwa ukaribu
sana kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Mtakapofanya
vizuri tutawapongeza ili muongeze juhudi, mtakapoharibu tutawawajibisha.
Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba Mwaka
wa Fedha uliopita ulikuwa mwaka mgumu sana kwa Watanzania. Ni mwaka ambao
gharama za maisha zilipanda kwa kasi kubwa sana na juhudi za Serikali
kuwakwamua wananchi na hasa wananchi wanyonge kutoka kwenye lindi la ufukara
ziligonga mwamba. Kambi ya Upinzani inawapa pole Watanzania kwani hili ndilo
walilochagua. Muhimu ni kuvumilia mpaka uchaguzi ujao na kufanya mabadiliko ya
Serikali ili kuweka Serikali itakayoongozwa na CHADEMA na itakayoweza kukabili
changamoto za sasa na za baadaye.
Mheshimiwa Spika, naomba tufanye mapitio kidogo ya Bajeti
inayomaliza muda wake.
- UTEKELEZAJI WA BAJETI
ILIYOPITA
Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani ni vema kufanya
tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali iliyopita ili kuona ni kwa namna
gani Serikali inathamini fedha za walipa kodi, na dhamira yake ya kuleta
maendeleo ya kiuchumi katika Taifa. Katika kufanya hivyo, tutapitia baadhi ya
maeneo ambayo Kambi ya Upinzani tunaona kuwa hayakutekelezwa katika bajeti
iliyopita.
Kupunguza Makali ya Maisha
Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali ilitangaza
nia yake ya kupunguza makali ya maisha. Hatua mbali mbali zilichukuliwa ikiwamo
kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya Dizeli na Petroli, kuanza kutekeleza
mpango wa dharura wa umeme na kutoa fedha za kununua chakula kwa Wakala wa
Chakula. Serikali ilitumia shilingi bilioni 296 na dola za
Marekani milioni 183 kwenye Umeme. Vilevile Serikali ilitumia shilingi bilioni
27 kununua Mahindi na kusambaza kwenye masoko.
Mheshimiwa Spika, licha ya hatua hizo zilizochukuliwa Mfumuko wa Bei
uliongezeka maradufu kutoka wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani
wa asilimia 17.8 mwaka 2011/12. Serikali imefeli katika lengo lake la kupunguza
makali ya maisha kwa wananchi. Sio tu kwamba Serikali imeshindwa kudhibiti
upandaji holela wa gharama za maisha bali pia hatua za Serikali zimeongeza kasi
ya kupanda kwa makali ya maisha.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni katika Hotuba yake
mbadala ya mwaka 2011/12 iliitaka Serikali kushughulikia msingi wa mfumuko wa Bei hapa
nchini ambao ni uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula. Tumeelezwa na Waziri
Kivuli wa Mipango na Uchumi kwamba Chakula peke yake ni asilimia 48 ya kapu la
bidhaa na huduma ambazo mwanachi anatumia. Mfumuko wa Bei ya Chakula
kinacholiwa nyumbani na kwenye migahawa ilikuwa asilimia 25 mwezi Aprili 2012
(BoT monthly Economic Review, May 2012). Vile vile mfumuko wa bei wa nishati
inayotumika nyumbani na mafuta ya Dizeli na Petroli ulifikia asilimia 25 pia
mwezi Mei mwaka 2012. Ni dhahiri kwamba iwapo tutadhibiti mfumuko wa bei ya
chakula tutaweza kushusha mfumuko wa bei kurudi kwenye tarakimu moja.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza hatua zilezile ilizofanya
mwaka wa fedha unaokwisha kwa kutoa vibali kwa Wafanyabiashara vya kuagiza
Mchele na Sukari. Katika hotuba yake Waziri wa Fedha anasema ‘….Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari
bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani 200,000 ili kukabiliana na uhaba
na kupanda kwa bei ya Sukari…’(uk 9 ibara ya 15). Baada ya hatua hii bei ya
Sukari ilipanda kutoka tshs 1700 mpaka tshs 2800 kwenye maeneo mengi nchini.
Waziri wa Fedha katika hotuba yake anatoa suluhisho. Ninanukuu. ‘…hatua za haraka
ambazo Serikali itachukua ni pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa Sukari na
mchele kutoka nje….’! Serikali inachukua hatua zilezile kwa tatizo lile lile
ikitegemea matokeo tofauti.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inarejea pendekezo lake
la mwaka jana kwa Serikali kutoa vivutio kwa wakulima wadogo kuzalisha chakula
kwa wingi. Miongoni mwa vivutio hivyo ni:
i.
Kuwekeza kwenye barabara za vijijini ili mazao yao yafike kwenye masoko
na kupata bei nzuri,
ii.
Kuwekeza kwenye Usambazaji wa Maji vijijini ili kina mama wasitembee
mwendo mrefu kutafuta maji na hivyo kutumia muda mwingi kwenye uzalishaji,
iii.
Kuwekeza kwenye Umeme vijijini ili wafanyabiashara wa vijijini waongeze
thamani ya mazao. Kwa mfano, kuuza Unga badala ya Mahindi.
iv.
Kuwekeza kwenye miundombinu ya Umwagiliaji vijijini ili wakulima
wazalishe muda wote wa mwaka.
v.
Kuwekeza kwenye Elimu vijijini na pia Afya vijijini ili wananchi wetu
wawe na Afya bora na waelimike katika mbinu za uzalishaji bora.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa, hakuna mbadala
wa kudhibiti mfumuko wa bei zaidi ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwekeza
kwa wananchi wetu. Serikali inafikiria uzalishaji utaongezeka kwa kusaidia
wakulima wakubwa ambao watageuza wananchi wetu kuwa Manamba na vibarua ndani ya
nchi yao. Tuwekeze kwa watu wetu vijijini ili waongeze uzalishaji na kwa kufanya hivyo mfumuko wa Bei ya chakula utakuwa historia. Hakuna mwarobaini wa kupanda kwa bei za vyakula
isipokuwa Kilimo.
Mhesimiwa Spika, Tunatambua kuwa hatua tunazotaka Serikali ifanye
ni za muda wa kati. Kwa muda mfupi tunataka Bodi ya Mazao mchanganyiko, Wakala
wa Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Sukari zipewe fedha kuagiza Mchele na Sukari
na pia kununua kutoka kwa wakulima na kusagisha Mahindi. Wafanyabiashara
waagizaji wa Chakula washindane na Taasisi hizi za Umma badala ya kuwapa vibali
ambavyo hutolewa kwa rushwa na hivyo kuongeza bei za bidhaa hizo.
Kuwezesha Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira.
Mheshimiwa Spika, Serikali imesema kwamba ilichukua hatua mbalimbali
kukabiliana na tatizo la Ajira kwa kuongeza fursa za ajira. Miongoni mwa hatua
zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza mitaji katika Benki ya Rasilimali, Benki
ya Wanawake, Benki ya Posta na Twiga Bancorp. Pia Serikali imetangaza kwamba
imeajiri walimu, maafisa ugani na watumishi wa Afya. Hatua kama hizi pia
zimetangazwa kwa mwaka wa Fedha wa 2012/13 ambapo pia Serikali imetangaza
kuajiri watumishi 71,756.
Mheshimiwa Spika, Duniani kote Serikali haizalishi ajira bali ajira
huzalishwa na Uchumi mzima ambapo Serikali ni sehemu tu ya Uchumi (Jobs are created by the economy).
Takwimu zinaonyesha kwamba kila mwaka Tanzania inaingiza kwenye soko la Ajira
watu takribani laki saba. Shughuli za Uchumi zikiongezeka ndio Ajira
zinatengenezwa. Serikali inafikiria nini kuhusu vijana takribani milioni nane
walio shule za Msingi hivi sasa, Vijana milioni 1.7 walio katika Shule za
Sekondari hivi sasa, Vijana 200,000 waliopo vyuo vya Ufundi na Wanachuo 180,000
walio katika Vyuo vya Elimu ya Juu (takwimu kutoka kitabu cha hali ya uchumi,
2012 sura ya 19). Serikali ambayo bado inategemea takwimu za Ajira za Mwaka
2006 inajitamba kwa kuajiri watu 70,000.
Mheshimiwa Spika, Jukumu la Serikali ni kujenga mazingira ya
wananchi kupata ajira ama kwa kujiajiri au kwa kuajiriwa na shughuli za uchumi.
Lakini ukweli ni kwamba Serikali imeshindwa kushughulikia tatizo la Ajira na
hasa ajira kwa vijana. Tatizo la Ajira kwa Vijana ni Bomu litakalokuja kutulipukia
vibaya sana kama hatutakuwa makini nalo. Hii ni nchi ya Vijana. Kutoshughulikia
masuala yao ni kutoshughulikia masuala ya nchi.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya ajira kwa vijana Bajeti mbadala
imeiwekea mikakati mipana ya kiuchumi kwa kuanzisha miradi mikubwa ya Umma
itakayomeza vijana waliopo mtaani na kuanzisha kwa makusudi na kwa kasi Vyuo vya
Ufundi stadi na Vyuo vya Ufundi na Mafunzo vingi. Kambi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza Uwekezaji wa Miundombinu Vijijini kama njia ya kupunguza tatizo la
ajira kwa vijana. Vilevile tunapendekeza Miradi mikubwa ya kuongeza mazao ya
Kilimo hasa Pamba, Korosho na Katani ili kupanua Ajira. Kambi ya Upinzani pia
inapendekeza kujenga VETA katika kila Halmashauri ya Wilaya na Chuo cha Ufundi
katika kila Mkoa ili kutoa ujuzi kwa vijana ili waweze kukabili maisha yao.
Badala ya Serikali kukopa kwa ajili ya Matumizi ya kawaida, Serikali ikope
kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi na vyuo vya Ufundi na Mafunzo. Ni Lazima viongozi
sio tu tuwe makini bali tuonekane kuwa makini tunaposhughulikia suala la Ajira
kwa Vijana.
Sera ya Mapato
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni ilitangaza vipaumbele
katika sera ya Mapato ambavyo ni pamoja na kukusanya Mapato ya Serikali mpaka
zaidi ya asilimia 20 ya Pato la Taifa ili kuwezesha kujitegemea kupata fedha za
miradi ya maendeleo. Pia Kambi ya Upinzani inakusudia kufanya marekebisho
mbalimbali ya sheria za kodi ili kulinda viwanda vya ndani vinavyotumia
malighafi za kilimo na mifugo za hapa nchini, kupanua wigo wa Mapato kwa
kutunga sheria ya kulazimu kila Mtanzania kujaza fomu za marejesho ya kodi na
kurekebisha viwango vya kodi ya Mapato (PAYE). Vile vile tunapendekeza kufanya
marekebisho ya sheria za kodi kwenye sekta za madini na mawasiliano ili
kuongeza mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha 2011/12 Serikali ilichukua
hatua mbalimbali katika masuala ya Kodi. Katika Bajeti mbadala pia
tulipendekeza hatua mbali mbali ambazo tuliona zitaongeza mapato ya Serikali na
hivyo kutuwezesha kuendeleza nchi yetu. Baadhi ya hatua mbalimbali
tulizopendekeza Serikali imetangaza kuzitekeleza.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani katika Bajeti Mbadala ya mwaka 2011/12 ilipendekeza
masuala yafutayo ili kuongeza mapato ya Serikali.
- Hatua zifuatazo zilipendekezwa ili kuweza
kukabiliana na ukwepaji wa kodi unaofanywa na makampuni makubwa ya
kimataifa (Multinational Corporations) na hatimaye kulipunguzia taifa
mapato:
(i)
Kutunga sheria kwa kuimarisha zaidi sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka
2004 kwamba, mikopo ya makampuni kwenye uwekezaji, kwa sababu za kikodi,
isizidi asilimia 70 ya mtaji wote uliowekezwa na hii ianze mara moja bila
kujali mikataba iliyopo.
(ii)
Kutunga sheria kuhakikisha kwamba riba kwenye mikopo kutoka Makampuni
yanayohusiana (sister companies) haitaondolewa kwenye kutoza kodi (not tax
deductible).
(iii)
Kuhakikisha kwamba mauziano ya Kampuni yoyote ambayo mali zake zipo
Tanzania yanatozwa kodi ya asilimia 30% kama ‘ongezeko la mtaji’ (‘capital
gains’).
Mheshimiwa Spika, katika mapendezo haya ni pendekezo moja tu ndilo limechukuliwa na
Serikali katika Bajeti ya mwaka 2012/13 nalo ni pendekezo la ‘capital gains
tax’. Hata hivyo Pendekezo la Serikali lina makosa makubwa sana ya kifundi.
Waziri wa Fedha Mhe. Mgimwa amesema, ninanukuu ‘Kuanzisha kodi itokanayo na
uuzaji wa rasilimali ya uwekezaji (capital gains tax) kwenye uuzaji wa HISA za
kampuni mama ya nje ya nchi’
Mheshimiwa Spika, Ukisoma pendekezo letu kwa haraka utaona kama Serikali imelichukua
lilivyo, lakini kwa jicho la kiuchumi pendekezo la Serikali na lile la Kambi ya
Upinzani ni mambo tofauti sana. Pendekezo la Serikali linazungumzia HISA.
Mamlaka ya Mapato Tanzania haitakuwa na mamlaka (jurisdiction to tax) kutoza
kodi kwa Kampuni mama (as a source or even residence). Mamlaka ya Mapato
Tanzania ina mamlaka na Mali (assets) zilizopo Tanzania za Kampuni mama. Kwa
mfano, wakati kampuni ya Barrick inanunua mgodi wa Bulyanhulu haikuinunua
Kampuni ya Kahama mining ltd bali ilinunua hisa zote za Kampuni ya Sutton
Resources. Vile vile, wakati Zain inanunua Celtel, haikununua Celtel Tanzania
ltd bali Celtel Africa BV ambayo ilikuwa inamiliki Celtel Tanzania BV ambayo ilimiliki
Celtel Tanzania ltd. Hivyo hivyo ilikuwa kwa AirTel ilipoinunua Zain. Kukwepa mitego hii ya Mashirika ya
Kimataifa (MNCs) sheria itaje kwamba Kodi hii itozwe kwa Mali zilizopo Tanzania
na sio kwa HISA kama alivyopendekeza Waziri wa Fedha. Hata hivyo Kambi ya
Upinzani inatambua hatua hiyo ya Serikali kuchukua wazo hili ili kuongeza
Mapato ya nchi.
Misamaha ya Kodi
Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali iliahidi kupunguza misamaha ya
Kodi mpaka kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa. Ahadi hii haikutekelezwa na
Serikali na badala yake imerejea kuahidi tena. Waziri wa Fedha ameliambia Bunge
katika hotuba yake, nanukuu ‘kuendelea
kufanya mapitio ya sharia mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la
kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo’ (uk.39). Badala ya Serikali kutuambia
hivi sasa misamaha ya kodi imefikia asilimia ngapi, imeendelea kutoa ahadi
isizoweza kutekeleza.
Mheshimiwa Spika, Katika Taarifa ya Utafiti uliofanywa na Jopo la Taasisi za dini hapa
nchini waliyoiita ‘The One Billion Dollar Question’ imeonekana kwamba Tanzania
inapoteza takribani shilingi trilioni 1.7 kutokana na misamaha ya kodi,
ukwepaji wa kodi, utoroshaji wa mitaji nje na udanganyifu katika biashara ya
kimataifa. Fedha hizi ni zaidi ya jumla ya Bajeti za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Nishati na Madini. Fedha hizi ni zaidi ya Mkopo ambao Serikali itadhamini
kwa TPDC ili kujenga Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Fedha
hizi zinazopotea kutokana na misamaha ya kodi ni zaidi ya gharama za Ujenzi wa
Gati mpya katika Bandari ya Dar es Salaam. Kambi ya Upinzani inawapongeza
Viongozi wa Dini kwa kufanya kazi hii nyeti sana lakini tunampongeza zaidi
Mtafiti Mtanzania Dokta Prosper Ngowi kwa kushiriki katika utafiti huu.
Tunaishauri Serikali kusoma Taarifa hii na kutekeleza mapendekezo yake ili
kuongeza mapato ya Serikali. Lugha za kufanya mapitio kila mwaka hazisaidii,
wananchi wanataka kuona misamaha ya kodi imepungua mpaka kiwango kinachostahili
cha asilimia 1 ya Pato la Taifa.
Kurekebisha mfumo wa Kodi ya Mapato
Mheshimiwa Spika, Bajeti mbadala ya mwaka 2011/12 ilipendekeza kuifanyia marekebisho
sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004. Tunarejea pendekezo letu na kuongeza
pia kwamba sehemu ya kodi ya Mapato inayotoa fursa (grandfathering) kwa Kampuni
za Madini kutumia sheria ya kodi ya Mapato iliyofutwa ya mwaka 1973, ifutwe.
Pendekezo letu lina lengo la kutaka kuweka mfumo wa ‘straightline method of
depreciation’ ya asilimia 20 badala ya sasa ambapo Kampuni za Madini hufanya
‘100% depreciation’ kwenye Mitambo yao mwaka wa kwanza na hivyo kuchelewesha
kulipa ‘Corporate Tax’.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kupandisha kiwango cha chini cha kipato ili kutoza
kodi ya Mapato (PAYE) kutoka tshs 135,000 mpaka tshs 170,000 bila kushusha kodi
yenyewe. Hii haitamsaidia mwananchi hata kidogo kwani bado kiwango cha
kodi cha asilimia 14 kipo juu sana. Vile
vile kiwango cha chini cha pato litakalotozwa kodi kitawaathiri wafanyakazi wa
Serikali maana ndio ambao Serikali ina mamlaka ya kutangaza kima cha chini cha
Mshahara wao na kuwaacha wafanyakazi wa Sekta Binafsi ambao wengi hulipwa
kiwango kidogo sana cha mishahara. Kimsingi kutokana na tangazo lake, Waziri wa
Fedha ametangaza kima kipya cha chini cha mshahara kuwa kitakua tshs 170,000.
Mheshimiwa Spika, tunarejea kauli yetu kwamba kupanda kwa gharama za maisha kumepunguza
uwezo wa matumizi ya wananchi walioajiriwa na kulipwa mishahara ambayo inakatwa
kodi (PAYE). Tunapendekeza kwamba PAYE ianzie asilimia 9 kutoka asilimia 14 na
kiwango cha chini cha kutoza kiwe tshs 150,000. Tunatambua kuwa kodi hii ni
chanzo kikubwa cha Mapato kwa Serikali ambapo kwa mwaka huu wa Fedha
kinatarajiwa kuingiza takribani shilingi bilioni 1,437 (asilimia 18 ya Mapato
yote ya kodi yanayokusanywa na TRA) kutoka Idara ya Kodi za Ndani (Wafanyakazi
wa Serikali tshs 115bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma tshs 47bn na
Wafanyakazi wa Sekta binafsi tshs 312bn) na Idara ya Walipa kodi wakubwa
(Wafanyakazi wa Serikali tshs 450bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma Tshs108bn
na Wafanyakazi wa Sekta Binafsi tshs 406bn). Hata hivyo wananchi wanapobakia na
pesa za matumizi kodi nyingine kama VAT na Ushuru wa Bidhaa huongezeka na hivyo
kupunguza kiwango cha Mapato ya Serikali ambayo yangepotea kutokana na uamuzi
huu.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo bado kuna haja ya kuangalia upya ‘tax brackets’ na kuzirahisisha kwa kuzipunguza na kuongeza kiwango
cha kodi ya Mapato kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.
Mheshimiwa
Spika, ili kuongeza mapato
kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa kambi ya Upinzani inapendekeza mabadiliko
katika viwango vya juu vya kodi ya Mapato ambapo tunapendekeza kupandisha
kiwango cha juu kabisa cha kukokotoa kodi ya mapato (PAYE) kiwe shilingi
milioni kumi na kodi iwe asilimia 42 kutoka asilimia 30 ya sasa.
Mheshimiwa
Spika, Tunapendekeza kwamba
mtu yeyote anayepata mapato ya zaidi ya shilingi 10,000,000 alipe kodi ya
Mapato ya shilingi 500,000 kujumlisha na asilimia 42 ya tofauti ya shilingi
10,000,000 na shilingi 3,200,000 kama inavyoonekana kwenye jedwali hapa chini.
Lengo la mapendekezo haya ni kuwafanya watu wenye kipato kikubwa walipe kodi
zaidi kulingana na kipato wanachopata maana hivi sasa masikini wanalipa kodi
nyingi zaidi kuliko wenye nacho.
Mapato ya kutozwa kodi kwa mwezi
|
Kodi (PAYE)
|
Mapendekezo ya mapato ya kutozwa kodi kwa mwezi
|
Kiwango kipya cha Kodi (PAYE)
|
Mapato
yanayozidi shilingi 720,000
|
Sh. 112,500
ongeza 30% ya kiasi kinachozidi sh. 720,000
|
Mapato yanayozidi 720,000 lakini hayazidi sh. 3,199,199
|
Sh.112,500 ongeza 30% ya ziada ya sh. 720,000
|
|
|
Mapato yanayozidi sh. 3,200,000 lakini hayazidi
sh.9,999,999
|
Sh.190,000 ongeza 38% ya ziada ya 3,200,000.
|
|
|
Mapato kuanzia sh. 10,000,000 na kuendelea
|
Sh. 500,000 ongeza 42% ya mapato yake.
|
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo haya hayatapunguza Mapato ya Serikali kwani wigo wa kodi
utakuwa umeongezeka kwa kuwagusa wafanyakazi katika sekta binafsi na pia kupata
kodi zaidi kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, vile vile Kambi ya Upinzani inaendelea kupendekeza kuwa mchakato uanze
ili kila Mtanzania mwenye umri wa miaka
18 na zaidi awe anajaza fomu za kodi (tax returns) kila mwaka. Suala hili
ni muhimu sana na litangazwe mwaka huu ili tuwe na mwaka mzima wa kujitayarisha
ili lianze Mwezi Julai mwaka 2013. Mtanzania yeyote, awe na kipato au asiwe na
kipato ajaze Tax Returns. Mfumo huu utatoa takwimu muhimu sana kwa Mamlaka ya
Mapato Tanzania na utasaidia sana hapo baadaye kupanua wigo wa Mapato.
Tunapendekeza marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Mapato ili mfumo huu uwepo
kisheria ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa.
Mheshimiwa Spika, Vile vile, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuanzishwa kwa Real Estate Regulatory Authority kama
tulivyofanya kwa mwaka uliopita na kwamba kila mwenye nyumba ya kupangisha
lazima atambuliwe na kulipa kodi inavyostahili. Lengo ni kuhakikisha Sekta ya
Nyumba inatoa mapato ya kutosha kwa Serikali na kuzuia mianya ya ukwepaji kodi
inayofanywa na wenye nyumba.
Presumptive Tax
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza mwaka 2011/12 kwamba ushauri
wa Mradi wa kuboresha mfumo wa kodi (Tax Modernisation Project) ambao ulishauri
kwamba ipo haja ya kuainisha Kodi ya VAT na Presumptive Tax, utekelezwe. Tunashauri
kuwa kodi anayotozwa mfanyabiashara ndogondogo kabla hajaanza kufanya biashara
ifutwe kabisa. Uamuzi huu utapunguza mapato ya Serikali (Shilingi bilioni 21.6
kwa mujibu wa Kitabu cha Bajeti Vol. I) katika kipindi cha muda mfupi lakini
itakuwa ni chanzo kikubwa sana cha mapato katika kipindi cha muda mrefu.
Vyanzo vipya vya Mapato
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kupitia vyanzo
vya mwaka jana na kulinganisha na mapendekezo ya Serikali, Kambi ya Upinzani
bado inapendekeza vyanzo vya ziada mwaka huu ili kuboresha Mapato ya Serikali.
Kupanua wigo wa Skills Development levy
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunapenda kushukuru kuwa wazo letu la kutoza kodi ya
skills development levy
tuliyopendekeza katika hotuba yetu ya mwaka uliopita lilifanyiwa kazi na
serikali lakini kwa mwaka ujao wa fedha tunaitaka serikali kuipitia upya kodi
kwa kuongeza wigo wa wachangiaji ili kuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya
kugharamia elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, tunapendekeza kiwango cha tozo ya kuendeleza stadi (skills development levy – SDL) kishuke
kutoka asilimia 6 ya sasa mpaka asilimia 4. Tunapendekeza kuwa Waajiri wote
walipe kodi hii ikiwemo Serikali na Mashirika ya Umma. Lengo ni kupunguza mzigo
kwa Waajiri na kuondoa ubaguzi kwani wanaofaidika na tozo hii (wanafunzi wa
elimu ya Juu) pia huajiriwa na Serikali na Mashirika ya Umma. Serikali ilipanga
kukusanya tshs 161bn kutoka katika tozo hii kwa mfumo wa sasa.
Mheshimiwa Spika, Marekebisho ambayo Kambi ya Upinzani inayapendekeza yataongeza mapato
ya Serikali mpaka tshs 320bn.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha katika tozo hii amesema Serikali ‘itapitia upya
maudhui ya viwango vya tozo’ hii. Kambi ya Upinzani imetamka maudhui na viwango
na tunaiomba Serikali itekeleze pendekezo hili.
Mheshimiwa Spika, Tunapendekeza mgawanyo wa tozo hii urekebishwe kwa kuongeza mapato
yatakayokwenda kwenye Vyuo vya Ufundi mchundo.
Mheshimiwa Spika, kama wanafunzi wetu watasomeshwa na kodi hii basi tuangalie upya mfumo
wa Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Fedha inayopatikana kwenye Kodi hii
itumike kusomesha kwa ‘grant’ wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi darasani na
kuwapunguzia mzigo wa mikopo. Vile vile tuangalie kama tunaweza kukopesha
wanafunzi malazi na chakula tu na kutoa bure ada na mafunzo kwa vitendo pamoja
na vitabu.
Kulinda kazi za Wasanii
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani mara kwa mara tumekuwa tukieleza jinsi wasanii
wanavyoshindwa kunufaika na kazi zao kutokana na kukosekana mfumo rasmi wa
kiserikali unaozuia wizi wa kazi za wasanii. Pamoja na serikali kukubali
kuahidi kuwa na mfumo rasmi wa kuzuia wizi wa kazi hizo, serikali haijaweka
wazi mfumo rasmi utakaokuwa unatumika kuzuia wizi huo na hatimaye wasanii
kunufaika na kazi zao.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani katika hotuba ya Wizara ya Habari Vijana na Michezo
kwa mwaka uliopita tulingumzia suala hili na tulishauri kwamba kuwe na
utaratibu wa kuweka sticker maalumu
zinazotolewa na mamlaka za serikali kuonyesha uhalali wa muuzaji wa kazi za wasanii.
Serikali imetekeleza pendekezo letu. Hata hivyo tuna maoni tofauti kuhusu namna
ya kutekeleza pendekezo hili.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, serikali mwaka 2006 kupitia gazeti
la Serikali Na. 18 la tarehe 10 Mwezi wa Februari, ilianzisha utaratibu wa
HAKIGRAM kama stiker maalumu za kazi halali za wasanii zinazotolewa na COSOTA.
Kambi ya Upinzani tunapendekeza utaratibu huo uendelee na Mamlaka ya Mapato TRA
ihusike kukusanya mapato kwa ajili ya kazi hiyo na COSOTA wataratibu utoaji wa
HAKIGRAM. Hii itaenda sambasamba na kuzuia uchakachuaji wa HAKIGRAM hizo ili
kutopoteza lengo la kuweka mfumo huo. Stiker zisitolewe na TRA bali zitolewe na
COSOTA na TRA isimamie eneo la Mapato tu. Hii itasaidia kwani stiker hizi
hazitatumika kupata mapato peke yake bali pia kuweka kumbukumbu muhimu za kazi
za wasanii.
Mapato kutoka Sekta ndogo ya Mawasiliano ya Simu
Mheshimiwa Spika, serikali imekuja na pendekezo la kuendelea na kutoza ushuru wa bidhaa
kwenye masuala ya huduma ya mawasiliano ya simu, jambo ambalo litamgusa
mtumiaji wa huduma hiyo ambaye ni mwananchi wa kawaida na hivyo kuongeza
gharama za simu. Kambi ya Upinzani inapinga kabisa kuongeza ushuru wa bidhaa
kwenye muda wa Maongezi (airtime) kwenye simu za mkononi.
Mheshimiwa Spika, Hoja ya wananchi hapa ni kwamba Kampuni za Simu za mkononi hazilipi
kodi ya kutosha na hasa kodi ya Makampuni (corporate tax). Waziri Mkuu
alipokuwa anafunga Bunge la Bajeti mwaka 2011 alitangaza Kampuni ambazo ni
walipa kodi wakubwa katika kipindi cha miaka 5 iliyopita. Katika orodha hiyo
kulikuwa na Kampuni moja tu ya Simu za Mkononi (Kampuni ya AirTel).
Mheshimiwa Spika, wakati wananchi wanataka kodi zaidi kutoka Kampuni za simu, Serikali
inapendekeza kuongeza kodi kwa mwananchi anayetumia simu. Kampuni zilipe kodi
ya Mapato na sio kukandamiza wateja kwa ushuru wa bidhaa ilihali huduma zenyewe
za simu hazina ubora.
Mheshimiwa Spika, vilevile wananchi wanalalamika kwamba Kampuni za simu za Mkononi
hajiweki wazi mapato yake yote hali iliyopelekea Kamati ya Bunge ya POAC
kuiagiza TCRA kufunga mtambo utakaoweza kuijulisha TCRA mapato yote ambayo
kampuni za Simu zinapata. Serikali ya Ghana ilifanya hivi na kupandisha
maradufu mapato yanayotokana na sekta ndogo ya simu. Hivi sasa Ghana, nchi
yenye watumiaji wa simu milioni 17 ukilinganisha na Tanzania yenye watumiaji 23
milioni, inakusanya asilimia 10 ya Mapato ya Serikali kutoka kwenye kampuni za
Simu peke yake. Iwapo Tanzania ikifikia kiwango cha Ghana cha asilimia 10 ya
Mapato ya ndani ya Serikali kutoka kwenye kampuni za simu, Tanzania itaweza
kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 860 kutoka kwenye sekta ndogo ya simu peke
yake. Hata hivyo mazingira ya Ghana na Tanzania ni tofauti na hivyo tunapendekeza
kiwango kutokana na hali yetu.
Mheshimiwa Spika, Shirika la TCRA kupitia zabuni nambari AE-020/2010-11/C/04 imetangaza ‘request for expression of interest for
design, development, installation and Management of Telecommunication
monitoring system under build, operate and transfer’ ili kupata chombo cha
kufuatilia Mapato ya Kampuni za Simu. Kwa mujibu wa ratiba zilizotangazwa na
TCRA chombo kitakuwa kimeanza kazi mwishoni mwaka huu wa 2012. Kwa dhati kabisa
napenda kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA na watumishi wote kwa kutekeleza
maelekezo ya Kamati ya Bunge kwa haraka ili kuhakikisha mapato kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kilichotushangaza ni kwamba Waziri wa Fedha na Uchumi hakugusia kabisa
suala hili muhimu sana kwa mapato ya Serikali badala yake Serikali imekimbilia
kukandamiza wanyonge watumiaji wa Simu na kuyaacha Makampuni ya Simu yakilipa
kiduchu kutoka kwenye mapato yao.
Mheshimiwa Spika, uamuzi huu wa kufuatilia mapato ya Kampuni za Simu na Marekebisho
tunayopendekeza ya kujenga uwezo zaidi wa TCRA kwa kuwa na Idara ya ‘Revenue
Assurance’ na kurekebisha sheria ya TCRA kwa kuweka wazi makujumu ya TRA ndani
ya TCRA, utaiingizia Serikali mapato ya takribani tshs 660bn.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili la Sekta ya Mawasiliano ninaomba kurejea kuitaka
Wizara ya Fedha itoe maelezo hapa Bungeni namna ambavyo Hisa za serikali katika
Kampuni ya MIC Tanzania ltd inayomiliki Kampuni ya Tigo zilivyouzwa. Mheshimiwa Spika Serikali
ilikuwa inamiliki hisa asilimia 26 katika Kampuni hii. Kwa mujibu wa kumbukumbu
nilizoziona Hisa hizi zote ziliuzwa kwa thamani ya dola laki saba kwa mwana
hisa mwenza mnamo mwezi Februari mwaka 2004. Kampuni hii leo inapata mapato ya
Tshs bilioni 20 kwa mwezi, tuliuza hisa zetu asilimia 26 kwa dola laki saba!
Laki Saba dola! Kambi ya Upinzani inataka uchunguzi maalumu katika mauzo haya
na Taifa liambiwe nini kilitokea na
hatua gani za kuchukua dhidi ya waliouza mali hii ya Umma bila zabuni wala
kuzingatia thamani ya fedha.
Kuzuia mauzo ya ngozi ghafi nje ya nchi
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imeshangazwa
na hatua ya serikali kuja na pendekezo la kuongeza ushuru kwenye bidhaa ya
ngozi ghafi inayosafirishwa nje kutoka asilimia 40 hadi 90 lengo likiwa ni
kuhamasisha usindikaji wa ngozi hiyo na kuiongezea thamani.
Mheshimiwa Spika, kwa nchi iliyo na mianya
mingi ya rushwa kama Tanzania hatua hii haitakuwa na tija kwa kuwa
wafanyabiashara wengi wa ngozi ghafi wamekuwa na tabia ya kupunguza takwimu za
kusafirisha ngozi ghafi na hivyo kupelekea serikali kukosa mapato mengi sana.
Serikali inafahamu kwamba hata ushuru wa mauzo nje wa asilimia 40 haukuweza
kutatua tatizo la viwanda vya ndani kukosa malighafi. Kambi ya Upinzani
haikubaliani na Pendekezo la Serikali kwani halitatatua tatizo la kukuza sekta
ndogo ya Ngozi nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaitaka
serikali kuzuia kabisa kusafirisha ngozi ghafi kwenda nje na badala yake kuwe
na mpango wa kutumia ngozi ghafi hapa nchini na kuleta tija katika uchumi wa
taifa kwa kutengeneza ajira na kuongeza thamani ya mauzo nje.
Mheshimiwa Spika, hatua ya kuzuia ngozi ghafi
kusafirishwa kwenda nje kwa Tanzania itakuwa sio suala jipya kwa sababu
Ethiopia imezuia na kuwekeza katika kiwanda cha viatu, mikanda na bidhaa za
ngozi. Kutokana na Mpango wa Mendeleo ya Ethiopia (GTP – Growth and
Transformation Plan) sekta ya Ngozi itaingiza fedha za kigeni za thamani ya
dola za Kimarekani bilioni 4 kwa mwaka. Hii ni sawa na fedha za kigeni ambazo
Tanzania inapata kutoka kwenye Dhahabu na Utalii kwa pamoja. Ethiopia nchi
iliyokuwa inatembea na bakuli na kulia njaa leo inakuwa nchi ya kupigiwa mfano
na sisi Watanzania! Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda pia amepiga marufuku
kuuza ngozi ghafi nje. Hata nchi ya Pakistani ambayo ndio ngozi zetu zinakwenda
nayo imepiga marufuku mauzo ya ngozi ghafi nje. Serikali ipige marufuku Mauzo
ya ngozi ghafi nje ya Nchi ili kulinda viwanda vya ngozi nchini, kuoongeza
Ajira na kuongeza mapato ya Fedha za kigeni.
Kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa
za Maziwa
Mheshimiwa Spika, sekta ndogo
ya Maziwa hapa nchini inahitaji kuwekewa maazingira ya kukua ili izalishe ajira
na mapato ya kodi kwa Serikali. Wakati Tanzania ndio nchi ya Afrika Mashariki
inayoongoza kwa kuwa na Ng’ombe wengi lakini inaongoza kwa kuagiza maziwa
kutoka nje yenye thamani ya dola za kimarekani 3.6m. Wakati Kenya imelinda soko
la Maziwa na Bidhaa za Maziwa kwa kuondoa (zero rating) kodi ya VAT kwenye
bidhaa za Maziwa, Waziri wa Fedha hajaonyesha kabisa juhudi zozote za kujengea
uwezo sekta ndogo ya Maziwa hapa nchini na hivyo kuweza kuondolewa kabisa
katika ushindani na kujikuta wafugaji wanakosa kabisa soko la kuuza maziwa yao
hapa nchini. Nchi za Rwanda na Uganda pia zimelinda Maziwa na Bidhaa za maziwa
kwa njia hii. Ni muhimu Serikali kuwianisha kodi hii na Nchi nyingine za Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
inapendekeza kufanya marekebisho kwenye sharia ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
kwa kufanya ‘zero rating’ kwenye Maziwa na Bidhaa za Maziwa zinazozalishwa hapa
nchini kwa kipindi cha miaka 5 ili kufikisha uzalishaji wa angalau lita 500,000
za maziwa kwa siku kutoka lita 123,000 za sasa na kuweza kutoa ajira kwa
watanzania zaidi ya elfu tatu.
Mheshimiwa Spika, hatua zote za kuongeza
mapato tulizopendekeza pamoja na hatua za Bajeti Mbadala iliyopita ambazo
tunarudia kuzipendekeza zitaongeza Mapato ya Serikali kwa takribani shilingi
bilioni 2,885 kama inavyoonyeshwa katika jedwali hapa chini.
NYONGEZA YA VYANZO VYA MAPATO MBADALA 2012/2013
Chanzo cha Mapato
|
Makisio - Bilioni
|
Marekebisho
ya kodi za misitu ikiwemo Mkaa
|
130.8
|
Kupunguza
misamaha ya kodi, kuzuia ukwepaji kodi na udanganyifu wa Biashara ya Nje
|
742.74
|
Mauzo ya
hisa za serikali
|
415.55
|
Marekebisho
ya kodi Sekta ya madini (kodi ya
Mapato, Kodi ya CGT na ushuru mbalimbali) (25% ya Mauzo ya Madini Nje)
|
578.36
|
Marekebisho
ya Kodi na Usimamizi bora wa Mapato Kampuni za Simu
|
502.26
|
Marekebisho
ya Kodi ya SDL
|
243.52
|
Mapato ya
wanyamapori
|
61.64
|
Kuondoa
msamaha wa ushuru wa mafuta- kampuni za madini
|
44.9
|
Usimamizi
wa mapato ya utalii
|
51.75
|
Kuimarisha
biashara katika EAC kwa kuongeza mauzo
|
114.15
|
JUMLA
|
2,885.67
|
Mheshimiwa
Spika, kama nilivyosema hapo
juu, vyanzo hivi vya mapato ni mjumuisho wa vyanzo ambavyo katika hotuba zetu
mbadala za nyuma tumekuwa tukipendekeza, ambapo tumevifanyia marekebisho
kulingana na hali halisi ya uchumi ulivyo kwa sasa, pamoja na kupendekeza
baadhi ya marekebisho ya sheria za kodi ili kuongeza mapato zaidi kwa Serikali.
DENI LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitika kwa serikali kuendelea kutengeneza
madeni kwa Taifa kwa kuendelea kukopa zaidi kwa matumizi ya kawaida ya
serikali. Wakati Serikali inasisitiza kwamba Deni letu linastahmilika, Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anaonyesha mashaka makubwa sana kutokana na kasi ya
kukua kwa Deni la Taifa. Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
inaonyesha kuwa Deni la Taifa linazidi
kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka shilingi trillion 10.5 mwaka 2009/2010 hadi
shilingi trillion 14.4 mwaka 2010/2011. Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha Deni la
Taifa limefikia shilingi trillion 20.3 mpaka ilipofika mwezi Machi mwaka 2012.
Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa
sasa limefikia shilingi trillion 22.
Mheshimiwa Spika, Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali bali ni
kwamba tunakopa kufanyia nini? Bajeti ya Mwaka 2012/13 inayopendekezwa
inaonyesha kwamba Serikali itakusanya shilingi trilioni 8.7 kama makusanyo ya
ndani na itatumia shilingi trilioni 10.6 kama matumizi ya kawaida. Ni dhahiri
kwamba sehemu ya mikopo ambayo serikali inachukua sasa itakwenda kwenye
matumizi ya kawaida. Hatutaki mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho,
kusafiri, magari nk. Tuchukue mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi
na kuzalisha kodi zaidi. Bajeti inaonyesha kwamba Serikali itakopa shilingi
takribani trillion 5 mwaka 2012/13.
Serikali ikubali kutekeleza mapendekezo ya Kambi ya Upinzani ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupanua wigo wa
kodi katika maeneo muhimu kama sekta ya madini na mawasiliano, kuzuia misamaha
ya kodi, kutokomeza ukwepaji kodi, na kuepuka matumizi mabaya ili kuepuka
madeni yasiyo ya lazima.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kusisitiza kwamba Bunge lifanye ukaguzi
maalumu kuhusu akaunti ya Deni la Taifa ili kuweza kubaini ukweli kuhusu
ustahmilivu wa Deni na mikopo ambayo Serikali inachukua kama inakwenda kwenye
Maendeleo na miradi ipi na kama miradi hiyo ina tija. Vilevile tumependekeza
kwamba Mikopo yote ambayo Serikali inachukua iwe inapata idhini ya Kamati ya
Bunge ya Fedha na Uchumi au Bunge litunge sharia ili kiwango cha juu cha kukopa
ambacho Serikali haipaswi kuvuka. Kuiacha Serikali inaendelea kukopa bila
mpango ni kuliweka Taifa rehani na kupeleka mzigo wa kulipa madeni haya kwa
kizazi kijacho. Hatuwezi kukubali Wazee
wetu waishi maisha yao, waishi maisha yetu na pia wakope maisha ya watoto wetu.
Mheshimiwa Spika, Ukiangali sura ya Bajeti ya Serikali,
inaonyesha kuwa Serikali itakopa fedha zenye masharti ya kibiashara ndani na nje yenye thamani ya Tshs. Trilioni 2.89 kwa
kipindi hiki cha 2012/13. Athari ya
mikopo ya kibiashara ya ndani ni kubwa
sana kwa watanzania, kwanza inawafanya wananchi hasa wajasiriamali wanaokopa
kushindana na Serikali yao, kwani mabenki yatashindwa kuwakopesha wafanyabiashara au
wakikopa watakopa kwa masharti magumu na hasa riba kuwa kubwa. Jambo hili
linapunguza uwezo wa wazalishaji kuongeza uzalishaji hasa viwandani kwa kukosa
mikopo ya uendeshaji. Kama tulivyoshauri hapo juu, Serikali ijiepushe na mikopo
ya masharti ya kibiashara kwa kuongeza makusanyo ya kodi.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa ya Serikali kuwa imepata Mshauri
Mwelekezi atakayeishauri katika kujiandaa kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa
na kulipa madeni. Serikali ilieleze
Bunge ni lini na kwa namna gani zabuni ya kumpata mshauri huyu ilitangazwa na
kama Sheria ya Manunuzi ilifuatwa.
Mwenendo wa Matumizi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza Bajeti ya TZS 15
trilioni(USD 8.75 Billion) katika mwaka 2012/13 kama ilivyowasilishwa na Waziri
wa Fedha na Uchumi wiki iliyopita. Uchambuzi wa vitabu vya Bajeti unaonesha
kwamba mafungu ya juu 5 yatakayoongoza kwa matumizi kwenye Bajeti hiyo ni Kama
ifuatavyo;
1. Huduma
kwa Deni la Taifa Tshs 2.7 trilioni (USD 1.69 Billion)
2. Wizara ya Ujenzi. Tshs 1 trilioni (USD 625 Million)
3. Wizara ya Ulinzi Tshs 920 bilioni (USD 575 Million)
4. Wizara ya Elimu Tshs 721 bilioni (USD 451 Million)
5. Wizara ya Nishati na Madini Tshs 641 bilioni (USD 400 Million)
Jumla TZS 5.982 Trilioni(USD 3.74 Billlion)
Chanzo: Vitabu vya Bajeti kwa Wabunge
2. Wizara ya Ujenzi. Tshs 1 trilioni (USD 625 Million)
3. Wizara ya Ulinzi Tshs 920 bilioni (USD 575 Million)
4. Wizara ya Elimu Tshs 721 bilioni (USD 451 Million)
5. Wizara ya Nishati na Madini Tshs 641 bilioni (USD 400 Million)
Jumla TZS 5.982 Trilioni(USD 3.74 Billlion)
Chanzo: Vitabu vya Bajeti kwa Wabunge
Mheshimiwa Spika, Jumla
ya mafungu haya ni sawa na asilimia 40% ya Bajeti yote, kwa hiyo asilimia 40%
ya Bajeti yote imepangwa kwa mafungu 5 tu na kati ya hayo Wizara ni nne tu za
Ujenzi, Elimu, Ulinzi na Nishati na Madini. Wizara ya Kilimo wala Afya hazimo
kabisa katika Wizara 5 zitakazopata fedha nyingi zaidi katika Bajeti. Fungu
lenye kiwango kikubwa zaidi ya Bajeti kuliko vyote ni fungu 22 ambalo ni malipo
kwa Deni la Taifa. Pia sehemu kubwa ya fedha zilizotengwa kwa Ujenzi na Nishati
ni madeni kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya miaka ya nyuma. Shilingi
bilioni 40 ambazo zimetengwa kwa ajili ya Mradi wa Kiwira katika Wizara ya
Nishati na Madini ni kwa ajili ya kulipia Madeni ya Kampuni ya TanPower
Resources ambayo iliuziwa Mgodi wa Kiwira na kushindwa kuundeleza.
Mheshimiwa Spika, Madhara ya Deni la Taifa yanaonekana hapa katika
matuumizi ya Serikali ambapo tunapokuwa tunalipa madeni tunachukuwa rasilimali fedha nyingi kutoka kwenye Miradi ya Maendeleo.
Wakati Bajeti ya Maendeleo ni shilingi trilioni 4.5, Bajeti ya kugharamia Deni
la Taifa ni shilingi trilioni 2.7 (sawa na nusu ya Bajeti nzima ya Maendeleo).
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya 2012/13 ni ya kulipa madeni zaidi kuliko
Bajeti ya kuchochea maendeleo ya Taifa letu. Bajeti hii pia yaweza pia kuwa ni
Bajeti ya kukopa zaidi maana jumla ya TZS 5.1 trilioni (USD 3.19 Billion)
zitachukuliwa na Serikali kama mikopo
kutoka vyanzo mbalimbali. Mikopo ya kibiashara ambayo ni mikopo ghali sana
itachukuliwa kwa wingi zaidi kuliko mwaka wa fedha uliopita.
Mheshimiwa Spika, Mgawanyo
wa rasilimali za nchi kwenye sekta za kipaumbele (Miundombinu ya usafirishaji
kama reli, bandari, ndege viwanja vya ndege n.k), Barabara, nishati,kilimo na
mifugo, ili kuinua uchumi zimetengewa fedha kidogo sana kuweza kuleta tija
kulingana na malengo ya Mpango wa Maendeleo kama ulivyopitishwa na Bunge lako
tukufu. Bajeti iliyotengwa kwa ajili ya nishati imeshuka kwa kiwango cha
shilingi 40 bilioni, pia kwa mwaka uliopita fedha zilizotengwa kwa ajili ya
miundombinu,reli na TEHAMA zilitengwa shilingi 2,781.4 bilioni kwa 2011/12 ikilinganishwa na shilingi 1,505.1
bilioni kwa mwaka 2010/2011,(hili lilikuwa ni ongezeko la asilimia 85). Kwa bajeti
ya mwaka huu inaonesha sekta zilezile za
vipaumbele; bajeti iliyotengwa ni shilingi 1.394.5 bilion ambayo ni pungufu ya
asilimia 49.86 kwa kulinganisha na mwaka 2011/2013.
Mheshimiwa Spika, wakati Waziri wa Fedha analiambia Bunge kuwa
ametenga shilingi bilioni 1,383 kwa ajili ya Usafirishaji na Uchukuzi, Wizara
ya Ujenzi imetengewa shilingi bilioni 1,000 kati ya hizo. Wizara ya Uchukuzi
yenye Reli, Bandari, Viwanja vya Ndege na Usafiri wa Maziwa ya Tanganyika,
Nyasa na Viktoria imetengewa chini ya shilingi bilioni 380. Serikali pia
haijasema fedha ambazo zilitengwa na Bunge katika Bajeti inayomaliza muda wake
na kuzielekeza kwenye Wizara ya Miundombinu na Wizara ya Uchukuzi zimetumikaje
maana bado wakandarasi wanadai na fedha za Reli hazikutoka zote kama
ilivyopitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Spika, wizara nyingi hazikupata fedha za Maendeleo kama
zilivyopitishwa na Bunge. Halmashauri za Wilaya ndio zilipata hali mbaya zaidi
katika kupata fedha za Maendeleo ambapo kwa wastani ni asilimia 47 tu ya Bajeti
ndio ilipelekwa katika Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa. Kutokana na
hali hii Wabunge kama wawakilishi wa wananchi walihoji Serikali kwenye Kamati
zao na kupata majibu ambayo sio ya kuridhisha hivyo kupelekea Wabunge kugomea
baadhi ya Wizara.
Mheshimiwa Spika,
Ushahidi wa hayo ni baadhi ya Kamati za
Kudumu za Bunge kukataa kukubali Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa baadhi ya
Wizara zilizo chini ya Kamati hizo. Wizara ambazo hazikupitishiwa /Kukubaliwa
makadirio yake ni pamoja na;
·
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
·
Wizara ya Uchukuzi, na (nilishangaa kumwona Waziri wa Uchukuzi
akiwaahidi wananchi pale Jangwani kwamba Reli inakarabatiwa vya kutosha ilhali
Kamati haijapitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake kwa kuwa haikupewa
fedha za kutosha)
·
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
Mheshimiwa Spika, kabla
Bunge lako tukufu halijajadili Makadirio ya Matumizi ya mwaka unaokuja ni vema Serikali itueleze kwanza fedha zilizotengwa
mwaka uliopita na hazikufika hatima yake nini?
Mheshimiwa Spika, uwiano wa bajeti iliyotengwa kwa matumizi ya kawaida ambayo ni asilimia
70% wakati bajeti ya maendeleo asilimia 30% haiwezeshi nchi kupiga hatua ya
haraka ya Maendeleo. Kama ilivyoonyeshwa na Waziri Kivuli Mipango na
nitakavyohitimisha hotuba hii, Serikali imetayarisha Bajeti hii bila kuzingatia
masharti yaliyowekwa na Mpango wa Maendeleo uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa
Katiba ya nchi yetu ibara ya 63 (3)(c) kwa kutotenga asilimia 35 ya Mapato ya
ndani ya Serikali kwenye Bajeti ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha kidogo katika miradi ya maendeleo
katika bajeti zake. Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), matumizi ya kawaida ya Serikali yanaongezeka huku matumizi katika
shughuli za maendeleo yanapungua mwaka hadi mwaka. Takwimu katika jedwali hapa chini zinaonyesha
Fungu
|
2009/2010
|
%
|
2010/2011
|
%
|
Fedha za matumizi ya kawaida (Sh)
|
6,251,629,581,428
|
73
|
7,587,424,923,903
|
77
|
Fedha za matumizi ya maendeleo (Sh)
|
2,299,010,652,135
|
27
|
2,223,684,150,465
|
23
|
Jumla
|
8,550,640,233,563
|
100
|
9,811,109,074,368
|
100
|
Chanzo: Ripoti ya CAG, uk. 21
Aidha, kwa miaka miwili iliyopita yaani 2009/2010
na 2010/2011 kumekuwa hakuna uwiano wa fedha za Maendeleo kama bajeti
zilivyopitishwa na Bunge dhidi ya fedha zinazotolewa na hazina kwa ajili ya
maendeleo katika Wizara na Idara. Tazama jedwali;
Mwaka
|
Bajeti iliyoidhinishwa
|
Fedha halisi zilizotolewa
|
Tofauti (Sh)
|
%
|
2009/2010
|
2,825,431,400,000
|
2,299,010,652,135
|
526,420,747,865
|
19
|
2010/2011
|
3,750,684,569,000
|
2,223,684,150,465
|
1,527,000,418,535
|
41
|
Chanzo: Ripoti ya CAG, uk.22
Mheshimiwa Spika, Kutokana na takwimu hizi,
jumla ya Sh. 1,527,000,418,535 au asilimia 41 ya fedha zilizoidhinishwa
kwa maendeleo hazikutolewa katika mwaka wa fedha 2010/2011, na kiasi cha Sh.
526,420,747,865 au asilimia 19 ya fedha
zilizoidhinishwa mwaka 2009/2010 hazikutolewa pia. Hii ina maana kuwa shughuli
za maendeleo za kiasi hicho cha fedha hazikutekelezwa kwa miaka husika.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inatafsiri hali hiyo kama utovu mkubwa wa nidhamu ya
matumizi ya fedha za umma kwa upande wa Serikali, Vilivile inaonesha ni jinsi
gani Serikali yetu haithamini maendeleo ndio maana kila mwaka Serikali
inazidisha matumizi yake na kuhakikisha kuwa inayapata kwa wakati huku ikipunguza
bajeti ya maendeleo na kutotoa fedha zote kama zilivyoidhinishwa na mbaya zaidi
hata zile zinazotolewa hazitolewi kwa wakati muafaka. Hii inafanya kukaa hapa
Dodoma na kupitisha Bajeti kuwe hakuna maana maana Bajeti haitekelezwi kama
ilivyopitishwa.
Mheshimiwa Spika, Kiasi kinachotengwa kwa ajili ya maendeleo kimeshuka kutoka shilingi
trilioni 4.9 katika mwaka wa fedha
2011/12 hadi kufikia kiasi cha shilingi trililioni 4.5 mwaka huu wa
fedha 2012/13. Pamoja na serikali
kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika bajeti iliyopita, bado
imeendelea kupunguza bajeti ya maendeleo
katika bajeti hii. Ni dhahiri serikali
haizingatii swala la maendeleo ya mwananchi, pia kutoona njia ya kuweka mkazo
katika maendeleo na kuendelea kupuuzia maazimio ya mpango wa maendeleo wa miaka
mitano.
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti mbadala, Kambi ya Upinzani imetenga asilimia 36.06 na
kukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kutoka katika mapato ya ndani kwa
matumizi ya maendeleo kama Mpango wa Maendeleo ya Taifa ulivyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, Tuliamua kama Taifa kwamba Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano ndio
safina yetu ya kuelekea nchi ya ahadi (middle income country). Mpango
ukapitishwa na Bunge na kuwekwa sahihi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Inasikitisha kuona kuwa Serikali inatoboa kisiri siri safina hii
wakati tupo kati kati ya maji! Ninaamini wananchi wanawaona wanaotoboa safina
yetu na watawatosa kabla hawajazamisha Taifa zima kwa kushindwa kutekeleza
Mpango unavyoelekeza.
Ubadhirifu wa fedha zinazotengwa
Mheshimiwa Spika, pamoja na fedha za maendeleo kutolewa kidogo kulinganisha na bajeti
inayopitishwa na Bunge, bado kumekuwepo na matumizi yasiyo na tija na
ubadhirifu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, upotevu wa fedha za umma umeendelea
kuwa kikwazo
kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Uchambuzi wetu juu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2010/2011 pekee, umebaini takribani jumla ya Bilioni 12.9 (12,968,168,985) za fedha za umma zimepotea kama ongezeko kutoka shilingi billion 11.9 (11,152,048,065) ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 14 ya upotevu wa fedha za Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010,hii inaonyesha kuwa Serikali inaona ni jambo la kawaida kupoteza viwango hivi vya pesa za Serikali na kambi ya upinzani kuwasisistiza wananchi kuendelea kuitathmini Serikali yao sasa ili kuweza kufanya maamuzi sahihi dhidi ya Serikali yao.
kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Uchambuzi wetu juu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2010/2011 pekee, umebaini takribani jumla ya Bilioni 12.9 (12,968,168,985) za fedha za umma zimepotea kama ongezeko kutoka shilingi billion 11.9 (11,152,048,065) ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 14 ya upotevu wa fedha za Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010,hii inaonyesha kuwa Serikali inaona ni jambo la kawaida kupoteza viwango hivi vya pesa za Serikali na kambi ya upinzani kuwasisistiza wananchi kuendelea kuitathmini Serikali yao sasa ili kuweza kufanya maamuzi sahihi dhidi ya Serikali yao.
MAPENDEKEZO YA KAMBI YA UPINZANI
SERA YA MATUMIZI
2012/13 KWA BAJETI MBADALA
Mheshimiwa Spika,
lengo kuu la Bajeti Mbadala ni kuhakikisha uchumi unakua katika maeneo ya
vijijini kwa kati ya asilimia 6 na 8 ili kuleta Maendeleo ya wananchi na
kutokomeza umasikini. Kwa njia hiyo ni
dhahiri wananchi wapatao milioni 30 waishio vijijini watanufaika na matumizi
ya raslimali zao.
Vipaumbele vya
bajeti ya Matumizi.
(i)
Kujenga Mazingira
ya Ukuaji wa uchumi vijijini (rural growth) kwa kuboresha miundombinu ya umeme,
barabara, maji na miundombinu ya Umwagiliaji. Tunapendekeza kutumia shilingi
bilioni 600 kila mwaka (bilioni 150 kwa kila sekta niliyotaja). Fedha hizi
zitasimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo Vijijini (Rural Development Authority – to
be established) itakayokuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
(ii)
Kukarabati Reli ya
Kati na matawi yake ya Tanga/Arusha na Mpanda. Tutatenga tshs 443bn kwa RAHCO
kwa ajili ya Reli. Lengo ni kuhakikisha Reli ya Kati inafikia uwezo wa
kusafirisha Tani 1.5m kwa mwaka na hivyo kulipatia Taifa fedha za kigeni katika
sekta ya usafirishaji kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Tunataka sekta ya
usafirishaji iliingizie Taifa fedha za kigeni mpaka dola za kimarekani 1.5
bilioni kutoka dola 0.5 bilioni za sasa.
(iii)
Kuboresha Elimu na
Afya hasa kwa Shule na Zahanati/Vituo vya Afya vya Vijijini kwa kutoa motisha
kwa wafanyakazi wa Sekta hizi walio kwenye Halmashauri za Wilaya. Tunapendekeza
posho za Mazingira ya Vijijini kwa Walimu, Madaktari na Manesi sawa na mara
moja na nusu ya Mishahara yao. Vile vile tutaongeza mishahara ya Walimu, Manesi
na Madaktari kwa asilimia 50, pamoja na kuboresha stahili zingine za kazi ili
kuvutia Watanzania wengi zaidi katika maeneo haya na kuboresha huduma zao kwa
wananchi.
(iv)
Kuongeza Kima cha
chini cha Mshahara kwa Wafanyakazi wa Umma mpaka Tshs 315,000 kwa Mwezi
(v)
Kuanzisha Pensheni
ya uzeeni kwa Wazee wote nchini wenye umri wa zaidi ya miaka 60.
(vi)
Kujenga Uwezo wa
Viwanda vya ndani ili Kuuza nje bidhaa za kilimo na mifugo zilizoongezewa
thamani. Tutazuia kuuza nje Korosho ghafi na Ngozi ghafi kwa kuanzia. Lengo ni
kufufua viwanda vyote vya nguo na kuanzisha viwanda vipya kwa kutoa motisha kwa
wawekezaji watakaotumia malighafi za hapa nchini.
(vii)
Kupunguza mzigo wa
matumizi ya magari ya Serikali kwa kupiga mnada baadhi ya ‘mashangingi’ na
kuweka mfumo wa kukopesha Magari kwa watumishi wote wa Umma wanaostahili Magari
kama alivyofanya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania. Katika Taarifa yake kwa
Kamati ya Fedha na Uchumi, Waziri wa Fedha alitamka, ‘….kufanya mapitio ya
stahili za aina za magari kwa viongozi wa ngazi mbalimbali na kuandaa mwongozo
wa kugharamia ununuzi wa vyombo vya usafiri ili kupunguza matumizi ya magari,
mafuta na matengenezo ya magari…’ kama hatua za kubana matumizi. Hatua hii ya
kupunguza gharama za magari Waziri hakuisema kabisa katika hotuba yake Bungeni.
(viii)
Kuendelea
kusisitiza kufutwa kwa posho za vikao katika mfumo mzima wa malipo na stahili
kwa watumishi wa Umma. Katika Taarifa yake kwa Kamati ya Fedha, Waziri wa Fedha
alitamka ‘…. Kufanya mapitio ya posho na stahili zote kwa lengo la
kuziwianisha….’ Suala hili nalo Waziri hakulizungumza kabisa katika Hotuba yake
Bungeni.
(ix)
Kuanzisha Chuo
Kikuu cha Mtwara (Mtwara University for Petroleum Studies) ili kuzalisha
wataalamu wa kutosha wa Sekta ya Mafuta na Gesi na kuliandaa Taifa kuwa na
wasomi mahiri wa maeneo hayo na hivyo kufaidika na Utajiri wa Mafuta na Gesi
uliopo nchini kwetu. Tunapendekeza shilingi bilioni 200 mwaka huu katika Bajeti
ya Wizara ya Elimu kwa ajiri ya Mradi huu.
(x)
Kutunga sheria mpya
ya Mashirika ya Umma (Public
Corporations Act) ili kujengea
uwezo Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vyema Mashirika yote ya Umma ambayo
Serikali inamiliki kwa zaidi ya asilimia 100 na kutoa nguvu za kisheria kwa
Shirika la CHC kuweza kusimamia hisa za Serikali katika Kampuni na Mashirika
ambayo Serikali inamiliki
chini ya asilimia 50.
(xi)
Kupunguza gharama
za safari za nje kwa kupunguza ukubwa wa misafara na madaraja ya kusafiria.
Eneo hili la safari za nje limekuwa likiigharimu Serikali fedha nyingi sana.
Mheshimiwa Spika,
kufuatia hatua mbali mbali za kikodi tulizozichukua Kambi ya Upinzani
inapendekeza Bajeti ya shilingi trilioni 15 ambazo zitapatikana kwa Mapato ya
ndani ya shilingi trilioni 11.9 na misaada na mikopo ya kibajeti ya shilingi
trilioni 3.2 kama ilivyopendekezwa na Serikali. Kambi ya Upinzani inapendekeza
Serikali kutokukopa kibiashara ili kudhibiti ukuaji wa Deni la Taifa.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba Serikali itatumia shilingi
trilioni 9 katika Matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 6 kama Matumizi ya
Maendeleo. Katika fedha za Maendeleo, asilimia 35 ya Mapato ya ndani
yameelekezwa huko kama ilivyoagizwa na Mpango wa Maendeleo ya Taifa
ulioidhinishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba.
SURA YA BAJETI
MBADALA YA MWAKA 2012/2013
|
MAPATO
|
SHILINGI
MILIONI
|
|
A
|
Mapato
ya ndani
|
|
11,889,078
|
|
i)mapato ya kodi (TRA)
|
|
|
|
ii)Mapato yasiyo ya kodi
|
|
|
B
|
Mapato ya Halmashauri
|
|
|
C
|
Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)
|
842,487
|
|
D
|
Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo nay a
kisekta
|
2,314,231
|
|
|
i)Misaada
|
1,465,461
|
|
|
ii)Misaada na mikopo
kisekta
|
415,137
|
|
|
iii)MCC(MCA-T)
|
433,634
|
|
|
Jumla ya Misaada na mikopo ya kibajeti
|
|
3,156,718
|
|
|
|
|
|
JUMLA
YA MAPATO YOTE.
|
|
15,045,796
|
|
MATUMIZI
|
|
|
E
|
Matumizi
ya Kawaida
|
|
9,000,000
|
H
|
Matumizi
ya Maendeleo
|
|
|
|
(i)Fedha za ndani
|
4,161,177
|
|
|
(ii)Fedha za Nje
|
1,884,619
|
|
|
Jumla
ya matumizi ya maendeleo
|
|
6,045,796
|
|
JUMLA
YA MATUMIZI YOTE.
|
|
15,045,796
|
Hitimisho
Fedha za Rada
Mheshimiwa Spika, Wakati Kamati za Bunge zilipokaa kujadili taarifa ya Serikali kuhusu
Mfumo wa Mapato na Matumizi, Waziri wa Fedha na Uchumi alitoa Taarifa kuhusu
Fedha za Rada zilizorejeshwa, jumla ya shilingi 72.3 bilioni ambazo
zilipokelewa tarehe 26 Machi, 2012. Kwa mshtuko wa Wabunge, Waziri aliiambia
Kamati kuwa mchakato wa manunuzi ya vitabu na madawati kwa kutumia fedha hizi
ulikuwa umeanza chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI. Fedha hizi hazijawahi
kupitishwa na Bunge lako tukufu. Kitendo cha Serikali kuzitumia kabla ya
kupitishwa na Bunge ni kuvunja sheria za Fedha kuhusiana na masuala ya Bajeti.
Wakati Waziri akiwasilisha Hotuba yake hakugusia kabisa suala la fedha
zilizorejeshwa kutokana na Ununuzi wa Rada!
Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inataka maelezo ya Serikali juu ya Fedha hizi na utaratibu wa kuzitumia. Kambi
inataka kufahamu vigezo vilivyotumika kuteua mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dar
es Salaam kutumia fedha hizi. Kambi pia inapenda kufahamu Deni lililochukuliwa
kununua Rada hii iliyoleta kashfa kubwa sana hapa nchini limefikia kiasi gani
kulilipa na tukililipa tutakuwa tumelipa kiasi gani kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, Uumbaji wa bajeti ya Serikali umekuwa ni ule ambao unapendelewa zaidi na
wale wavivu wa kufikiri, yaani mfumo rahisi, wataalamu wanauita Incremental Budgeting. Mfumo huu
hujikita zaidi katika kutizama ukuaji wa mapato na kugawa mapato hayo kwa
mtindo wa nyongeza ya asilimia Fulani toka katika bajeti iliyotangulia. Mfumo
huu huacha kuzingatia mambo mengi mtambuka. Mfano, tunaweza tizama sekta
mojawapo ya umeme ambapo tukifanya uumbaji wa bajeti kwa mfumo wa kiasi cha
nyongeza (incremental budget) kuna thamani halisi ambazo ukizitizama kwa bei
wazi ya soko tayari zimepaa sana ndani ya miezi kumi na miwili.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni, tukiwa ni serikali ambayo tunasubiri
kukabidhiwa dola, tunapendekeza kwamba ni vema tukaanza kutizama uwezekano wa
matumizi ya Zero Budgeting ambapo
japo ni mfumo ambao unahitaji kazi ya ziada, lakini una faida sana kwani
hutizama mipango ya matumizi kulingana na wakati uliopo huku ikifanya rejea ya
wakati uliopita.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani pia inapendekeza kwamba Bajeti za Mashirika ya Umma
ziwe sehemu ya Bajeti Kuu ya Nchi kwani kuna masuala mengi yanayotekelezwa na
Mashirika haya na Wananchi kupitia Bunge hawayajui. Ni vema katika mfumo mpya
wa Bajeti tutakaokuwa nao kufuatia mapendekezo ya Spika wa Bunge ambapo kutakuwa
na Ofisi ya Bajeti ya Bunge na Kamati ya Bunge ya Bajeti, Sheria ya Bajeti
(Fiscal Responsibility Act/Budget Act) izingatie suala la kuziweka kama
viambatisho Bajeti za Mashirika ya Umma katika Bajeti ya Nchi.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali ya mwaka huu kama ilivyowasilishwa na Waziri wa
Fedha imewasahau kabisa wananchi wa vijijini na haina mkakati wowote wa
kuwakomboa watanzania walio wengi wanaoishi huko. Mipango mingi ya kikodi
katika sera ya Mapato ya Serikali itasaidia wakazi wa mijini ambao ni asilimia
25 tu ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inapenda kuweka msisitizo kwamba Tanzania bado ni
nchi ya Wakulima maana robo tatu ya Watanzania wanaishi vijijini ambapo hawajui
hizi hadithi za Uchumi kukua tunazoimba na kupewa sifa kila siku. Hawa ni watu
milioni 30 ambao hawana Maji, hawana Umeme, mazao yao hayafiki sokoni maana
hawana barabara nzuri, shule wanazosoma watoto wao hazina walimu maana
wanakimbia mazingira magumu. Hawa Watanzania wa chini milioni 30 (The Bottom
30M) tunaowawakilisha hawana bima mazao yakiharibiwa na wala hawana pensheni
wanapokuwa wamezeeka na kupoteza nguvu za kufanya kazi. Hawa ‘The Bottom 30M’
bado wanaishi maisha walioshi babu zetu. Hawa Watanzania milioni 30
tumewasahau. Tunajenga Mataifa mawili ndani ya nchi moja, moja la mafukara
(wanavijiji) na moja la wanaojiweza (wamijini).
Mheshimiwa Spika, Kama tunataka kujibu kitendawili cha kuwa na Uchumi unaokua kwa kasi
lakini haupunguzi umasikini inabidi kuelekeza nguvu zetu vijijini walipo
Watanzania wengi. Kukuza Uchumi wa Vijijini kwa kuwekeza kwenye misingi ya
kujenga uchumi imara ndio njia pekee ya kutokomeza ufukara wa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, Bajeti Mbadala ya Kambi ya Upinzani mwaka huu ni Bajeti ya Ukombozi wa
mwananchi. Licha ya
kwamba tunahitaji ukuaji wa kasi zaidi wa uchumi. Changamoto sasa ni namna gani
ukuaji huu wa uchumi unawafikia wananchi milioni thelathini wa Vijijini na
kuboresha maisha yao.
Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano uliwasilishwa Bungeni na Serikali na kupata pongezi nyingi sana kutoka kwa
waheshimiwa wabunge lakini cha kushangaza Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi imeshindwa kuutekeleza kwa vitendo
mpango huu wa Taifa. Mwaka wa kwanza Mpango haukuwekewa fedha kwa kuwa ulikuwa
wa Mpito. Mpango unahitaji angalau shilingi trillion Nane kila mwaka ili uweze kutekelezwa. Mpango ulipata shilingi trillion moja
tu mwaka 2011/12.
Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Bunge liliazimia namna ya kuhakikisha tunapata fedha za
kuendeleza nchi yetu sisi wenyewe, naomba kunukuu ukurasa wa 92 kifungu cha 4.3.1 katika Mpango wa Maendeleo
wa miaka mitano toleo la kiswahili kama ifuatavyo ‘kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya
mpango, serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga asilimia 35 ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya
kugharamia bajeti ya maendeleo kila mwaka’ mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, KWA KUWA katika makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha
2012/13 Serikali imetenga asilimia
sifuri ya Mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia Bajeti ya Maendeleo.
Serikali hii imeshindwa kusimamia ahadi zake yenyewe kama inavyoonekana katika
mpango wa maendeleo ya miaka mitano. Serikali hii ya CCM imeshindwa kuheshimu
Uamuzi uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977.
Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(c ) madaraka ya Bunge ni pamoja
na ‘Kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi
unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya
kusimamia utekelezaji wa mpango huo”. Bunge liliidhinisha Mpango kwa mujibu wa ibara
tajwa ya Katiba.
Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Bajeti ya mwaka 2012/13 iliyowasilishwa Bungeni na Waziri wa
Fedha na Uchumi haikukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo kama ambavyo ulipitishwa
na Bunge, HIVYO BASI,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iiondoe
(withdraw) Bungeni Bajeti iliyoileta ili ikatayarishwe upya ili ikidhi matakwa
(compliance) ya Mpango wa Maendeleo kama ulivyoidhinishwa na Bunge na kusainiwa
na Rais wa nchi.
Mheshimiwa Spika Naomba Kuwasilisha
………………………………………………….
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Waziri wa Fedha na Uchumi Kivuli
18.06.2012
SURA
YA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA
2012/2013.
|
MAPATO
|
%
|
SHILINGI
MILIONI
|
|
A
|
Mapato ya
ndani
|
57.63
|
|
8,714,671
|
|
i)mapato ya kodi (TRA)
|
|
8,070,088
|
|
|
ii)Mapato
yasiyo ya kodi
|
|
644,583
|
|
B
|
Mapato ya
Halmashauri
|
|
362,206
|
|
C
|
Mikopo
na Misaada ya kibajeti (GBS)
|
5.57
|
842,487
|
|
D
|
Mikopo
na misaada ya miradi ya maendeleo na ya kisekta
|
15.30
|
2,314,231
|
|
E
|
Mikopo
ya ndani
|
10.78
|
1,631,231
|
|
F
|
Mikopo
yenye masharti ya kibiashara
|
8.25
|
1,254,092
|
|
|
|
|
|
|
|
JUMLA YA
MAPATO YOTE.
|
|
|
15,119,644
|
|
MATUMIZI
|
|
|
|
E
|
Matumizi ya
Kawaida
|
71.06
|
|
10,591,805
|
|
(i)
Deni
la taifa
|
|
2,745,056
|
|
|
(ii)
Mishahara
|
|
3,781,100
|
|
|
(iii)
Matumizi
Mengineyo
|
|
4,065,649
|
|
|
Wizara
|
|
3,311,399
|
|
|
Mikoa
|
|
49,701
|
|
|
Halmashauri
|
|
704,549
|
|
H
|
Matumizi ya
Maendeleo
|
|
|
|
|
(i)Fedha
za ndani
|
|
2,231,608
|
|
|
(ii)Fedha
za Nje
|
|
2,34,231
|
|
|
Jumla ya
matumizi ya maendeleo
|
29.94
|
|
4,527,839
|
|
JUMLA YA
MATUMIZI YOTE.
|
|
|
TOFAUTI
KATI YA BAJETI YA SERIKALI NA BAJETI MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI
Bajeti Mbadala
ya Kambi ya Upinzani2012/2013
|
Bajeti ya
Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013
|
Kukuza
uchumi vijijini.
|
Mwelekeo
na malengo ya Serikali hauleweki, hatua zilizochukuliwa ni koboresha uchumi
wa mijini.
|
Njia
mbadala zinazotekelezeka za kupunguza mfumuko wa bei.
|
Kuwa
na njia zilezile zilizoshindwa mwaka wa fedha uliopita za kupunguza mfumuko
wa bei.
|
Kunufaika
na mapato ya mitaji “Capital gains” kwa kutoza kodi kwa mali za kampuni
zilizopo nchini kwa mauzo yanayofanyika nje ya nchi na hivyo kupanua wigo wa
TRA kutoza kodi
|
Kutoza
hisa kwa mauziano ya hisa pekee kwa mauziano yanayofanyika nje. Hisa
inapunguza wigo wa TRA kutoza kodi.
|
Kupanua
wigo wa kodi ya tozo la ujuzi (SDL)kwa kuijumuisha serikali na mashirika ya
umma na kupunguza mzigo kwa sekta binafsi pekee.
|
Kupitia
upya SDL bila kuonyesha namna itakavyofanyika.
|
Kupunguza
misamaha ya kodi kutoka 3% ya sasa hadi 1% ya pato la taifa.
|
Kurudia
ahadi zilezile za mwaka jana za kupitia upya misamaha ya kodi bila kuleta
mrejesho wa kile walichokifanya.
|
Kuboresha
kodi sekta ya madini ili kupelekea taifa kupata nagalau 25% ya mazuo ya madini nje kama mapato ya
serikali.
|
Kutokuwa
na hatua yoyote ya kuongeza mapato ya Serikali kutoka katika sekta ya madini.
|
Kulipa
kima cha chini cha mshahara kuanzia shilingi 315,000.
|
Kulipa
shilingi 170,000 kama kima cha chini.
|
Kulipa
pensheni kwa wazee wote kuanzia miaka 60 na kuendelea
|
Kutokuwa
na mfumo wa pensheni kwa wote.
|
Kushusha
kiwango cha chini kodi ya mapato kwa wafanyakazi (PAYE) kutoka 14% hadi 9% ili kumpunguzia mfanyakazi makali ya maisha
na kutoza kodi zaidi kwa watu wenye kipato kikubwa
|
Kubaki
na kiwango kilekile cha chini cha kodi ya 14% na kubakiza mfumo ule ule wa
kodi ya Mapato unaomfanya Masikini alipe zaidi ya Tajiri.
|
|
|
Kuziba
mianya kwa makampuni ya simu kukwepa kutokulipa kodi ya mapato.
|
Kuongeza
ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi na hivyo kumwongezea gharama
mwananchi.
|
Kuondoa
mikopo ya kibiashara ili kulipunguzia taifa mzigo wa madeni
|
Kuendelea
mikopo na hivyo kuongeza deni la taifa. mingi ya kibiashara.
|
|
|
Kutenga
asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo kama ilivyoelekezwa kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano.
|
Kutenga
asilimia sifuri ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo
na hvyo kutokutekeleza mpango wa taifa .
|
Utegemezi
wa Bajeti 21.3%
|
Utegemezi
wa Bajeti 42.37%
|
|
|
|
|
|
|
JEDWALI LA ULINGANISHO WA ASILIMIA KWA BAJTEI
MBILI
|
UPINZANI
|
ASILIMIA
|
SERIKALI
|
ASILIMIA
|
|
Mapato ya ndani
|
78.70
|
Mapato ya ndani
|
57.63
|
|
Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)
|
5.57
|
Mikopo
na Misaada ya kibajeti (GBS)
|
5.57
|
|
Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na y
a
kisekta
|
15.30
|
Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na y
a
Kisekta
|
15.30
|
|
Mikopo
ya masharti ya kibiashara ya ndani
|
0
|
Mikopo
ya masharti ya kibiashara ya ndani
|
10.78
|
|
Mikopo
ya masharti ya kibiashara ya nje.
|
0
|
Mikopo
ya masharti ya kibiashara ya nje.
|
8.25
|
|
Matumizi ya Kawaida
|
59.22
|
Matumizi ya Kawaida
|
71.06
|
|
Matumizi ya Maendeleo
|
40.78
|
Matumizi ya Maendeleo
|
29.94
|
|
Matumizi
ya maendeleo fedha za mapato ya ndani
|
36.06
|
Matumizi
ya maendeleo fedha za ndani
|
0
|
|
Matumizi
ya maendeleo fedha za nje
|
12.39
|
Matumizi
ya maendeleo fedha za nje
|
29.94
|
No comments:
Post a Comment