Habari za Punde

Hospitali Tatu Zafungiwa na Moja yafutiwa Usajili.

Na Fatma Kassim, MAELEZO
BODI ya Ushauri wa hospitali Binafsi imezifungia hospitali tatu na kuifutia usajili hospitali moja baada ya kushindwa kutekeleza maagizo waliyopewa na bodi hiyo ya kuondosha kasoro mbali mbali zilizojitokeza katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hospitali zilizofungiwa ni pamoja Latifah Clinic iliyopo maeneo ya Kwaalinato, Kitope Roman Catholic iliyopo maeneo ya Kitope wilaya ya Kaskazini ‘B’ pamoja Changongo iliyopo maeneo ya Kwaboko mjini Zanzibar.

Msaidizi Mrajis wa Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi Dk. Shaaban Seif Mohammed ameitaja Hospitali ya Neema Clinic iliyopo maeneo ya Tomondo kuwa imefutiwa usajili kutokana na kupinga taratibu za Bodi hiyo.

Alisema kuwa hospitali ya Latifah, imefungiwa kutokana na ukosefu wa wafanyakazi wenye sifa na daktari dhamana wa Hospitali hiyo kutohudhuria jambo linaweza kuhatarisha afya za wanaofika kupata matibabu hospitalini hapo.

Aidha alisema kuwa hospitali Changongo ambayo inajishughulisha kwa tiba za magonjwa ya meno imefungiwa kutokana uchafu.

Aidha Dk. Shaaban alifahamisha kuwa kwa hospitali ya Kitope Roman Catholic hawana wafanyakazi wenye taaluma ya fani ya afya ambapo tayari huko nyuma walikwishapewa taarifa ya kutafuta wafanyakazi wenye taaluma lakini hawajatekeleza agizo hilo.

Alifahamisha kuwa Bodi pia inatoa tahadhari kwa hospitali ambazo mpaka sasa hazikakata kibali cha kuendesha huduma hizo kukata kibali haraka iwezekanavyo ili waweze kutoa huduma kama inavyotakiwa.

Alisema iwapo wamiliki hao hawatokata kibali cha kuendeshea huduma hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa na pamoja na kuzifungia kabisa hospitali zao hizo zisiweze kutoa huduma kwani zinaweza kuhatarisha afya za wananchi.

Alisema vitendo vinavyofanywa na baadhi ya hospitali Binafsi si vizuri na vinaenda kinyume na maadili ya utoji wa huduma za Afya hali inayoweza kurudisha nyuma maendeleo ya serikali katika kuimarisha huduma za afya kwa jamii.

Alisema serikali imekuwa inachukua juhudi kadhaa katika kuhakikisha hospitali binafsi zinatoa huduma zenye ubora kwa wananchi kwani zinasaidia sana katika kupunguza misongamano kwenye hospitali za serikali.

Alitoa tahadhari kwa wananchi kuwa waangalifu wanapokwenda hospitali hizo kuwa na kuacha mara moja kutotumia Hospitali ambazo zina kasoro za utoaji huduma za afya

Alifahamisha kuwa Bodi itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara hospitali hizo ili kuhakikisha zinafanya marekebisho ya kasoro walizonazo na iwapo watakaidi bodi haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuzifungia moja kwa moja na kuwapelekeka katika vyombo vya sheria.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.