Habari za Punde

Katiba Mpya - Muarubaini wa Kero za Muungano


Na Juma Mohammed, MAELEZO 

Wajumbe wa Baraza Wawakilishi Zanzibar wamesema muarubaini wa kero za Muungano ni kuwa na katiba mpya itakayoweka bayana mambo yatakayosimamiwa na kila upande kwa uwazi zaidi.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya kudumu ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kwa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Mwakilishi  wa Kwahani(CCM) Ali Salum Haji alisema ikiwa kutakuwa na katiba itakayobainisha na kuzitambua haki za kila upande wa Muungano anaamini hakuna nchi itakayomlaumu mwenzie.


Mheshimiwa Spika, kwa hiyo muarubaini wa matatizo au Kero za Muungano wetu ni kuwa na katiba ambayo itakayobainisha na kuzitambua haki za kila upande wa Muungano huu na kutofautisha zipi zitashughulikiwa na kila Nchi katika Muungano huu na zipi zitashughulikiwa na chombo cha Muungano hapo tunaamini hakuna Nchi itakayo mlaumu mwenzie kama aidha ni mzigo au anaonewa na mwenziwe” Alisema Mwakilishi huyo.


Mwakilishi huyo aliyewasilisha maoni hayo kwa niaba ya Mwenyekiti wake, alisema hivi sasa hali haiku hivyo kwani mamlaka moja imebeba mambo yak wake na ya Muungano ambapo mwengine anahisi kuwa kuna haki zake za msingi ananyimwa.


“Waheshimiwa Wajumbe sio kama ilivyo hivi sasa kuwa kuna Mamlaka moja imebeba mambo ya kwake na ya Muungano ambapo mwingine anahisi kuwa kuna haki zake za msingi ananyimwa na mwenzake, na hii ndio inayopelekea kuwepo kwa manung’uniko ya kila siku kwa upande mmoja ambapo yamefikia kupachikwa jina na kuitwa kero za Muungano” Alisema Mwakilishi Ali.

Mwakilishi huyo alisema  katiba ya Jamhuri ya Muungano,  Wizara za Muungano  ni chache,  lakini  kiuhalisia Mawaziri wote waliopo Tanzania Bara wanafanya kazi zao kama ni Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

“Sasa, je! tujiulize, hii ndiyo sahihi? lakini ukiangalia katika katiba ya Jamhuri ya Muungano, kwa kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Baraza letu la Wawakilishi kwa mujibu wa kifungu cha 64 cha katiba ya Muungano, mamlaka yetu yanaishia hapa hapa Zanzibar tu basi, tafsiri hiyo inabaki kuwa ni sahihi na tumekubali” Aliliambia Baraza Mwakilishi huyo.

Aidha, Kamati hiyo imesema  kama wananchi na viongozi wanahisi mambo yalivyo kwa wakati huu sio sahihi basi ni lazima warekebishe katiba  na kwa kuwa hivi sasa wananchi wako huru kuzungumza wanachokitaka, lakini kwa kufuata utaratibu na Sheria za Nchi zilizopo  hakuna wakati mwengine isipokuwa ni wakati huu.“Mheshimiwa Spika, kamati yangu inaamini hayo yote yanawezekana ndani ya Muungano wetu bila ya hata kutengana, kwani huu ni Muungano wetu sote na sitegemei kama atatokea kiongozi atakaetaka kumdhulumu mwenziwe, kikubwa hapo kila mmoja ajenge hoja, itakayomridhisha mwenziwe” Alisema Mwakilishi huyo.

Aidha, Kamati hiyo imewaomba wananchi wa Zanzibar kujiandaa vema kwa kujenga hoja za msingi katika mchakato wa kutoa maoni katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Nawaomba sana wananchi wetu wa Zanzibar wajenge hoja zao kwa kurekebisha vifungu vilivyomo kwenye Katiba na kama kuna tofauti ya mawazo basi ni vyema watu wasipikiane majungu, sijui huyu Uamsho, huyu anabururwa na CUF, huyu anabururwa na CCM, haya yote hayatusaidii kwa hivi sasa na hili ndio tatizo letu Wazanzibari, kazi yetu ni kulalamika tu sio kujenga hoja zitakazoisaidia Nchi” Alisema Mwakilishi Ali.

Aliongeza kwamba ni vizuri kwa wananchi kuzisoma katika zote mbili ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nay a Zanzibar.

“Lakini na wao wajenge hoja zao ili kuonyesha namna wanavyohisi wao, kwa hiyo ni vyema kuisoma Katiba kama ilivyoandikwa na kwa sisi Zanzibar ni lazima kuzisoma katiba zetu zote mbili na baadae kuweza kujenga hoja zetu vinginevyo tutapotea” Aliongeza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.