TAARIFA MAALUM YA
WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS MHE. FATMA A. FEREJ KWA
WANANCHI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA UPIGAJI VITA MATUMIZI NA
BIASHARA HARAMU YA DAWA ZA KULEVYA DUNIANI- 25/06/2012
Ndugu Wananchi
Mabibi na Mabwana
Assallam Alleykum,
Awali ya yote ni wajibu wetu kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa
Rehema kwa kutujaalia uhai na uzima siku hii adhimu ya leo . Aidha napenda
nichukue nafasi pia kwa niaba yenu kumuomba Mola atupe na sisi pia Rehema na
Baraka zake katika maisha yetu yote na
nchi yetu kuendelea kuwa na amani, utulivu na masikilizano - AMIN
Ndugu Wananchi
Kama ilivyo kawaida yetu leo kwa
mara nyengine tena nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni
sehemu ya Jamii ya Kimataifa inaungana na mataifa mengine Duniani katika
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita
Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya.
Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa
za Kulevya Duniani (International
Day Against Drug Abuse and Illicit Trafficking) huadhimishwa kila ifikapo tarehe 26 Juni
Duniani kote na kuratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Dawa za Kulevya na
Uhalifu ( United Nations Office on Drugs
and Crimes – UNODC).
Ndugu
Wananchi
Siku hii adhimu imeasisiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (United
Nations General Assembly) mnamo mwaka 1987 na huwa ni ukumbusho kwa nchi
wanachama wa Umoja wa Mataifa na Jamii ya Kimataifa kwa ujumla juu ya azimio
lenye lengo la kuwa na jamii iliyositirika na kuwa huru na matumizi ya mihadharati.
Harakati za maadhimisho ya siku hii hulenga zaidi katika kuongeza
uelewa na kuishajihisha jamii kufahamu mafanikio na changamoto zinazoikabili
dunia juu ya tatizo la dawa za kulevya na kuandaa mikakati mbali mbali katika
kukabiliana nalo.
Ndugu Wananchi
Maadhimisho haya huja na
kauli mbiu au ujumbe mahsusi ambao huwa
dira katika ufanikishaji wa shughuli mbali mbali zenye mnasaba na siku hii
adhimu. Ujumbe wa Mwaka Huu “ Tujenge
Jamii Yenye Afya Bila ya Dawa za Dawa za Kulevya”
( Global Action – Healthy Communities
Without Drugs) unalenga zaidi katika kuhamasisha kuwepo kwa misingi
mizuri ya kijamii yenye afya njema na ushiriki wa sekta
nyengine mbali mbali katika kukabiliana
na janga la dawa za kulevya. Ujumbe unazidi kutanabahisha kwamba licha ya
changamoto zinazoikabili dunia kwa hivi sasa juu ya janga hili, misingi thabiti na imara ya kijamii, kifamilia na ushiriki wa sekta mbali mbali una nafasi
muhimu na ya kipekee katika kuleta
mabadiliko na kukabiliana kikamilifu na janga hili.
Taarifa ya taasisi ya Umoja wa Mataafa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu
inaonyesha kwamba watu karibu millioni mia mbili na kumi (210,000,000) hutumia
dawa haramu za kulevya duniani kote , matumizi ya dawa hizo huwaacha karibu watu laki mbili (200,000)
wakipoteza maisha kila mwaka. Aidha matumizi na usafirishaji wa dawa hizo
yamekuwa si tishio kwa afya za watumiaji pekee bali pia ni tishio kwa amani, usalama, ustawi wa jamii na
maendeleo kwa ujumla kwa mataifa duniani
kote.
Ndugu
Wananchi
Tukiwa katika harakati za maadhimisho haya wengi wetu kwa njia moja
au nyengine tumeguswa na athari za matokeo ya matumizi ya dawa za kulevya ,
tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya
nchini linadhihirishwa na ongezeko la vijana waliojitumbukuzi katika matumizi hayo ambao wamekuwa wakifika katika vituo mbali mbali na
kuhitaji huduma. Matumizi ya dawa za kwa njia ya kujidunga sindani imekuwa ni tishio na chanzo cha maambukizi mapya ya virusi vya
UKIMWI na maradhi mengine mbali mbali yanayopatika kwa njia ya damu ( blood borne infections). Hali hii
imepekela vijana wengi nchini wanaotumia dawa za kulevya kuambukwiza ugonjwa wa
UKIMWI. Utafiti uliofanywa mwaka 2005 hapa Zanzibar ulionyesha hali ya kutisha ya maambukizi hayo iliyofikia asilimia ishirini na nane (
28%) kwa wanaojidungu na kubadilishana
sindano
Ndugu
Wananchi
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Tume ya Kuratibu na
Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyopewa masuala mtambuka ikiwemo hili la
mapambano dhidi ya dawa za kulevya imetoa msukumo mkubwa katika mapambano dhidi
ya dawa za kulevya nchini. Baadhi ya maeneo ambayo yameweza kutekelezwa ni: -
a)
Kufanya mapitio ya Sheria ya
Udhibtiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar (
Sheria Nam 9,2009) iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi.
b)
Mafunzo juu ya dawa za kulevya
kwa wadau mbali ikiwemo Vyuo
vya Mafunzo, Mahkama, na Taasisi za dini.
c)
Kuendeleza programu maalum za
kuwafikia watumiaji wa dawa za kulevya katika maeneo yao ( outreach work),
taaluma kwa jamii kupitia vyombo mbali mbali na pia huduma za ushauri nasaha kwa wateja.
d)
Msukumo mkubwa katika
uanzishwaji wa huduma za makaazi za marekebisho za kuacha matumizi ya dawa za kulevya maarufu
Sober Houses.
e)
Ruzuku kwa ajili ya uendelezaji
wa huduma za marekebisho kwa vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya.
Jumla ya nyumba tisa zimepatiwa ruzuku
hiyo Unguja na Pemba.
f)
Utoaji wa taaluma kwa watendaji
wanaotoa huduma katika makaazi hayo
ya nyumba za marekebisho.
NduguWananchi
Ni jambo la faraja
kuona kwamba kuanzishwa kwa huduma za makaazi kwa vijana wanaoacha matumizi ya
dawa za kulevya (SOBER HOUSES)
zinazoendeshwa na taasisi zisizo za kiserikali zimeonyesha mafanikio makubwa
tokea kuanzishwa kwake zaidi ya miaka mitatu iliyopita. Katika kipindi cha
Julai 2011 hadi Machi 2012 jumla ya vijana 501 tayari wameweza kupata huduma kupitia
nyumba hizo Unguja na Pemba.
Ndugu Wananchi
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais iliyopewa dhamana ya uratibu na
udhibiti wa dawa za kulevya itaendelea kutoa kila aina ya msukumo kwa taasisi
zisizo za kiserikali ili kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya
nchini.
Ndugu Wananchi
Tunaendelea kushuhudia mwamko wa ukuaji wa huduma na juhudi za vijana wanaotumia dawa ya kulevya kutaka kujikwamua
na janga hilo, juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote.
Aidha, jamii inapaswa kuunga mkono harakati za vita dhidi ya dawa za
kulevya nchini na taasisi zilizopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria zinapaswa kufanya kazi zake kwa makini na kwa
uadilifu mkubwa .
Ndugu Wananchi
Kwa niaba yenu naomba nichukue nafasi hii kulipongeza tena Jeshi la
Polisi kwa nadharia iliyobuni ya Ulinzi
Shirikishi ambayo imeonyesha mafanikio makubwa katika baadhi ya shehia . Kumekuwa na mifano mizuri ya
shehia ambazo zimekuwa mstari wa mbele
katika kuchukua juhudi za makusudi za
kukabiliana na vitendo visivyoendana na maadili ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, juhudi
hizo zinapaswa kupongezwa.
Ndugu Wananchi
Napenda kutoa wito kwa shehia na jamii kwa ujumla kuona kwamba
wakati umefika sasa wa mafanikio hayo kuigwa katika shehia na maeneo mengine
ili kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini.
“ZANZIBAR BILA YA DAWA YA KULEVYA INAWEZEKANA”
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment