Habari za Punde

Kutozingatia Kanuni na Sheria Kuhifadhi Mazingira Huleta Athari Mbaya - Waziri Ferej


Na Ali Issa Maelezo 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwaza wa Rais Fatma Abdull Habib Ferej amesema pasipo kuwa na tahadhari  na utaratibu mzuri wa kuvuna maliasili zisizo rejesheka, athari mbaya za mazingira hutokea baadae  bila ya kizuiwizi na kuleta maafa makubwa katika nchi.

Hayo ameyasema leo Ofisini kwake Migombani wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani ambapo kilele chake kwa Zanzibar itakua kesha huko visiwani Pemba .

Waziri Fereji amesema  uvunaji wa mali asili zilizo mzunguka mwanadamu na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo ni suala la lazima kwa binaadamu yeyote ili aweze kuishi lakini iwapo binadamu hatozingatia sheria za mazingira kunaweza kusababisha matatizo makubwa kwa wananchi na mazingira yao.


“Uvunaji wa mali asili zilizo mzunguka mwanadamu pamoja  uwendeshaji wa shughuli za kimaendeleo ni suala la lazima kwa binaadamu yoyote ili aweze kuishi, hata hivyo   pasipokuwa  na tahadhri na  utaratbu mzuri wa kuvuna mali asili hizo ndipo athari mbaya za uharibifu wa mali asili hizo na mazingira hutokea”alisema Fereji 

 Aidha alisema kuwa miongoni mwa sababu zinazo pelekea kuwepo kwa changamoto za kimazingira ni pamoja na wadau mbalimbali kutozingatia na kufuata taratibu,kanuni na sheria zilizopo ambazo zinajikita katika kuyalinda mazingira.

Amezitaja sheria hizo kuwa ni pamoja na sheria za uvuvi ,misitu , aridhi na mazingira ambazo  zinatoa muongozo mzuri kwa matumizi bora ya ardhi endelevu na mali asili zilizopo katika visiwa vya Zanzibar na kusisitiza ufuatwaji wa sheria hizo  kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho .

Waziri huyo alitaja athari zilizopo juu ya mazingira ni pamoja na ukataji ovyo wa miti ya misitu, matunda na mikoko , ujenzi holela usio kuwa na mpangilio hasa karibu na  vyanzo vya maji.

Athari nyingine ni pamoja na utupaji taka ovyo wa taka za majumbani ,mahotelini na sehemu za biashara ,  uingizaji bidhaa chakavu  hasa za umeme, uchimbaji mchanga, kifusi udongo, mawe na kuendelea kutumia mifuko ya plastiki. 

“Mazingira ya visiwa vyetu katika hali yake ya asili kimsingi yalikuwa mazuri yenye fukwe zenye kupendeza ,bahari iliyosheheni rasilimali mbalimbali ,udongo wenye rutuba na miti na wanyama wa aina tofauti ,mambo yote haya yametuwezesha kufikia kwenye maendeleo tulionayo”alieleza Waziri Fereji.

Hata hivyo waziri alisema kumekuwa na mabadiliko ya tabia nchi ya ukame wa muda mrefu na mmong’onyoko wa fukwe athari hizo ni baadhi ya athari nyingi za mabadiliko ya tabia  nchi ambazo zimekuwa zikichangia kasi ya upoteaji wa miti katika maeneo mbalimbali ya visiwa vya Zanzibar .
Waziri huyo alisisitiza kutunza na kuhifadhi mazingira ili kuwa na uchumi endelevu kwa faida ya wananchi wote na kusema kwamba suala la kuhifadhi mazingira linahitaji nguvu na juhudi za pamoja ili kuepusha uharibifu wa mazingira na athari zake .

Maadhimisho ya siku ya mazingira duniani hufanyika kila mwaka duniani Juni 5 ambapo kwa hapa Zanziba mwaka huu kilele chake kitakuwa Pemba na ujumbe wa mwaka huu ni “Uchumi endelevu jee unakuhusu wewe?”  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.