Habari za Punde

Utumishi wa Umma na Utawala Bora Waahidi Kuleta Ufanisi na Kuimarisha Utawala Bora

 Na Rajab Mkasaba, Ikulu

WIZARA ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeahidi kuendelea na jukumu lake la kusimamia utekelezaji wa Watumishi wa Umma ili iweze kuwahudumia wananchi kwa kiwango cha juu katika kuleta ufanisi na kuimarisha Utawala Bora nchini. 

Hayo yalielezwa na Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Haji Omar Kheri katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa kuangalia robo tatu ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2011-2012 na kulinganisha na robo ya kwanza na ya pili pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka wa fedha 2012-2013. 


Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambao ulikuwa chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein pia, ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee. 

Waziri Kheri alieleza kuwa miongoni mwa majukumu ya Wizara hiyo ni pamoja na kusimamia, kudhibiti, kuratibu na kutathmini utekekelezaji na uongozaji wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuzingatia misingi ya mipango ya kitaifa kama vile Dira ya 2020, MKUZA II, Ilani ya Uchaguzi ya CCM na 2010-2015 pamoja na mikataba na makubaliano ya kikanda na kimataifa ambayo imeridhiwa nchini. 

Katika kuwajengea uwezo wananchi juu ya dhana nzima ya uelewa wa Utawala Bora, Waziri Kheri alisema kuwa elimu ya uraia kwa umma kupitia vipindi vya redio, semina na makongamano imetolewa mjini na vijini.  

Alieleza kuwa kwa upande wa uanzishwaji wa Bima ya Afya Zanzibar, maandiko ya msingi ya awali yenye kuonesha taswira nzima na hatua zinazohitajika kufuatwa katika uanzishwaji wa Bima ya Afya imeandaliwa kwa mashirikiano kati ya Kamati ya Wataalamu wa ndani, Wataalamu wa DANIDA na Shirika la Afya Duniani(WHO). 

Aidha Waziri huyo alieleza kuwa muongozo wa uhakiki wa wafanyakazi na mishahara umetayarishwa, muongozo huo unasaidia kuwatambua wafantyakazi halali wa Serikali na kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali kulipia mishahara hewa. 

Pia, alieleza kuwa Muongozo wa uhakiki wa Wafanyakazi na Mishahara umetayarishwa ambapo utasaidia kuwatambua wafanyakazi halali wa Serikali na kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali kupitia mishahara inayolipwa. 

 Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza kuwa katika mwaka wa fedha ujao suala zima la nyongeza za mishahara litazingatia zaidi uzoefu, elimu, uwajibikaji, nidhamu na utendaji wa kazi kwa wafanyakazi wote wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kinyume na utaratibu uliokuwa hapo kabla. 

 Aidha, alieleza kuwa Serikali itaendelea kuwasaidia watumishi wake wa umma pale hali itakaporuhusu lakini kipaumbele kitawekwa katika misingi hiyo ikiwa ni pamoja na wale wafanyakazi wenye uzoefu wa siku nyingi ambao nao watafaidika kwa kiasi kikubwa katika hatua hiyo huku akisisitiza matumizi ya Mwenendo wa Utumishi pamoja na kupandisha vyeo kwa kufuata daraja za wafanyakazi sanjari na kurejesha nyongeza kwa wafanyakazi wa muda mrefu huku akisisitiza elimu na uzoefu kupewa kipaumbele. 

Akizungumza na uongozi huo Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kusimamia vyema majukumu ya kazi zao za kila siku na mafanikio makubwa yaliopatikana nchini katika suala zima la Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini. 

Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Idara Maalum za Vikosi vya SMZ na kuipongeza Idara hiyo kwa juhudi zake katika suala zima la ulinzi wa nchi pamoja na kuendeleza kazi za maendeleo wanazopangiwa. 

Dk. Shein alieleza hayo wakati alipokutana na Uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa kuangalia robo tatu ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2011-2012 na kulinganisha na robo ya kwanza na ya pili pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka wa fedha 2012-2013. 

Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambao ulikuwa chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein pia, ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee. 

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa ametiwa moyo na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Idara hiyo Maalum za Vikosi vya SMZ na kuahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuviimarisha zaidi ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi. 


Dk. Shein alieleza kuvutiwa kwake na hatua hiyo ya kuviongezea uwezo wa kiutendaji vikosi hivyo snjari na kusisitiza juu ya upangaji wa mipango ya Bajeti kwa Idara hiyo ili iweze kuimarika zaidi. 

Nao Uongozi wa Ofisi hiyo ulieleza kufarajika kwao na juhudi anazozichukua Dk Shein katika uongozi wake ikiwa ni pamoja na kuviimarisha vikosi hivyo na jinsi ya ziara alizozifanya katika kuvitembelea, huku akiahidi kuendelea kuviunga mkono. 

Aidha, uongozi huo ulitoa pongezi kwa Dk Shein kwa kuendelea kuviimarisha vikosi vya SMZ kwa kutambua umuhimu wake katika kuimarisha amani na utulivu pamoja na sekta za maendeleo hapa nchini. 

Uongozi huo ulieleza lengo lake la kuanza kwa ujenzi wa majengo ya chuo kippya cha Mafunzo huko Hanyegwa Mchana Unguja pamoja na kuanza ujenzi wa ofisi ya Chuo cha Mafunzo Pemba na kuendelea na ujenzi wa ofisi ya zoni ya mashamba Unguja. 

Aidha, uongozi huo ulieleza azma yake ya kuendelea kuyapima na kuyapatia hati miliki mashamba ya Chuo cha Mafunzo Ubago Unguja, Kengeja, Tungamaa na Kangagani Pemba. 

Pamoja na hayo, uongozi huo ulieleza kuwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto katika vikosi hivyo lakini juhudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kuzitatua awamu kwa awamuna kuweza kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupatiwa vifaa na mafunzo. 

Kwa upande wa Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), uongozi huo ulieleza kuwa kilipatiwa vifaa vya kisasa vya uzamiaji na utaalamu wa kuvitumia vifaa hivyo pamoja na mbinu za kuzamia ambapo kwa upande mwengine, askari wa Idara Maalum za SMZ wameweza kushiriki kikamilifu katika matuki kadhaa ya uokozi baharini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.