Habari za Punde

Maalim Seif Atembelea Vianzio vya Maji


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Dk. Mustafa Ali Garu, akimuonesha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad namna chemchem inavyotiririka, katika chemchem ya Mtopepo walipofanya ziara ya kutembelea chemchem hiyo jana tarehe 19/06/2012.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na uongozi wa ZAWA wakiangalia upungufu wa maji katika eneo la Mtopepo alipofanya ziara ya kutembelea chemchem ya Mtopepo jana. Kuliani kwake ni Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdallah Shaaban. (Picha, Salmin Said, OMKR). 

Na Hassan Hamad OMKR

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali italazimika kutumia ukali na kuondoa muhali kwa watu wanaoendeleza vitendo vya uchafuzi wa mazingira hasa katika vianzio vya maji. 

 Amesema ni hatari kuona vitendo hivyo vikiendelea huku taifa likikabiliwa na uhaba wa maji unaotokana na uharibifu wa mazingira katika vianzio hivyo. 


Akiwa katika ziara ya kutembelea vianzio vya maji katika chemchem ya Mtopepo, Maalim Seif ametahadharisha kuwa ikiwa vitendo hivyo vitaachiwa kuendelea, kuna hatari ya taifa kuwa na upungufu mkubwa wa maji katika miaka michache ijayo.

 “Inabidi sasa tuwe wakali ili isije ikafika wakati tukawa hatuna maji katika nchi yetu”, alitahadharisha Maalim Seif. 

 Amesema katika kudhibiti hali hiyo, serikali itachukua kila aina ya tahadhari kuhakikisha kuwa vianzio vya maji haviendelei kuharibiwa kwa maslahi ya vizazi vijavyo na taifa kwa ujumla.

 Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA) Dk. Mustafa Ali Garu amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kwa sasa ni uvamizi wa ujenzi karibu na vianzio vya maji, hali inayopelekea mfumo wa uzalishaji wa maji kubadilika na kupunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha maji katika chemchem. 

 Kwa upande wake Mhandisi wa Mamlaka hiyo injinia Said Saleh amesema baadhi ya chemchem ndogo ndogo zimeanza kutoweka, na kutaka tahadhari zaidi zichukuliwe katika kudhibiti uvamizi wa vianzio hivyo. 

Amefahamisha kuwa karibu nusu ya kiwango cha maji yamepungua katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kutoka katika chemchem za Mtotopepo na Mwanyanya, huku chemchem ya Mtopepo ikiwa na upungufu mkubwa zaidi.

 Ziara hiyo pia imemshirikisha Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdallah Shaaban

2 comments:

  1. Hii kwa kweli ni hatari, serikali ianze sasa kabla kuchelewa kuwachukulia hatua watu wataobainika katika uchafuzi,ujenzi , ukataji miti karibu na vyanzo vya maji.

    Pia Serikali ianze sasa kuangalia uwezekano wa Zanzibar kuwa na mtambo wa kubadilisha maji chumvi(desalination plant) kuweza kutumika kwa matumizi ya binadamu hapo baadae, utaalamu huu upo tayari duniani na si haba tumezungumkwa na bahari.

    ReplyDelete
  2. Mimi nadhani ingali mapema kwa Z'bar kusafisha maji ya bahari, la muhimu hapa ni kuvilinda vyanzo vyetu vya maji baridi.

    SMZ haina budi kupima viwanja ktk maeneo ya uwanda na kuwapa w'nchi wenye mahitaji ili wajenge.

    Inaskitisha kuona SMZ imepima mamia ya viwanja na kuwapa watu wasio na haja ya viwanja, matokeo yake watu wanajenga ktk vyanzo vya maji huku Tunguu kunaendelea kubaki pori!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.